read

Aya 81-87: Hatutoi Ushahidi Ila Tunayoyajua

Maana

“Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ewe baba yetu! Hakika mwanao ameiba na hatutoi ushahidi ila tunayoyajua; wala hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.”

Hii ni kauli ya mkubwa wao akiwausia ndugu zake kuwa waseme ukweli kwa baba yao. Wampe habari kuwa wamewaona watumishi wa waziri wakitoa chombo cha kupimia cha mfalme katika mzigo wa Bin-yamin. Na kwamba waziri aling’ang’ania kumchukua. Hayo ndiyo tuliyoyashuhudia.

Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyo nyuma ya hayo. Na lau tungelijua ghaibuu, basi tusingemchukua wala kukupa ahadi ya kurudi naye. Tumefanya bidii sana. Tunaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na kwako.

“Na waulize watu wa mji tuliokuwako.

Yaani waulize watu wa Misr, jambo hili la wizi limeenea kwao.

Na msafara tuliokuja nao.

Yaani vile vile uliza msafara tuliokuja nao kutoka Misr ambao uko jirani yako katika nchi ya Kanaan.

Na hakika sisi tunasema kweli kwa haya tunayokusimulia. Mara hii walikuwa wakisema kwa kujiamini kwa sababu walikuwa na uhakika wa wanayoyasema kinyume na mara ya kwanza walipokuja na damu ya uwongo kwenye kanzu ya Yusuf.

Akasema: “Bali nafsi zenu zimewashawishi jambo fulani.

Walipomweleza baba yao aliwaambia mmefanyia vitimbi kama mlivyomfanyia ndugu yake, Yusuf.

Wafasiri wamejiuliza kuwa vipi Ya’qub aliwatuhumu wanawe kwa vitimbi kabla ya kuthibitisha na yeye ni mtume ma’asum?
Kisha wakajbu kwa njia nyingi zisizotegemea msingi wowote. Njia nzuri zaidi waliyoitaja ni ile kuwa makusudio ya Ya’qub ni kuwa nafsi zenu zimewapa picha ya kuwa Bin-yamin ni mwizi na hali yeye si mwizi.

Tuonavyo sisi ni kuwa Ya’qub aliwatuhumu na vitimbi kwa kuchukulia walivyomfanyia Yusuf, lakini yeye hakuchukulia moja kwa moja, kwa kukosa dalili ya uwongo wao. Vile vile hakuwachukulia hatua yoyote kwa dhana. Kwa sababu dhana haitoshelezi kitu.

Hiyo haipingani na cheo cha utume. Kwa sababu mtume hajui ghaibu, naye ni kama mtu mwingine anadhania na kuchukulia uwezekano. Tofauti ni kuwa kwake yeye dhana haina athari yoyote, kama afanyavyo asiyekuwa ma’sum.

Subira ni njema.

Yaani ‘subira yavuta heri.’ Haya aliwahi kuyasema zamani alipopotea Yusuf na sasa anayasema kwa Bin-yamin.

Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja.

Yaani Yusuf, Bin-yamin na kaka yao aliyebakia Misr karibu na ndugu yake. Neno ‘huenda‘ ni mwangaza wa matumaini; hasa likiwa linatoka kwa anayeamini ghaibu kikwelikweli; kama mitume na wasadikishao. Katika Nahjulbalagha imeelezwa: “Haiwi kweli imani ya mja mpaka yawe yaliyo kwa Mwenyezi Mungu ni ya kutegemewa zaidi kuliko yaliyo mikononi mwake” Kuna Hadith nyingi zenye maana haya.

Hakika yeye ni Mjuzi Mwenye hekima.

Anajua huzuni yangu na machungu yangu na anapanga mambo kwa hekima yake.

Na akajitenga nao, na akasema: “Oh! Masikitiko yangu juu ya Yusuf!”

Alijitenga na watu ili aomboleze peke yake, ambapo huzuni na kilio kilizidi kwa kumkosa mwanawe, Bin-yamin (Benjamin) na macho yake yakawa meupe kwa huzuni.

Yaliathirika kwa sababu ya kulia.

Naye akawa anaizuia.

Yaani anameza uchungu kwa mwili na mishipa yake.

Wakasema: Wallahi huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika wenye kuaangamia.”

Yaani wanawe walimwambia bado unamkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au ufe bure, kwa sababu Yusuf amekwenda harudi tena.

Akasema: “Majonzi yangu na huzuni yangu ninamshtakia Mwenyezi Mungu, sio kwenu kwa sababu ni udhalili na usafihi kumshtakia ambaye haondoi dhara. Imam Ali (a.s.) anasema: “Allah Allah! Na kumshatakia ambaye hawezi kuondoa mashaka yenu, wala hawezi kupunguza kwa rai yake yale mliyokwishayapitisha”

Na ninajua kwa Mwenyezi yale msiyoyajua.”

Yaa’qub ameteseka kwa kumkosa Yusuf, lakini wakati huo huo bado anamtegemea Mwenyezi Mungu na kumwekea dhana nzuri wala hakati tamaaa na rehema yake huku akiamini kuwa mwisho wa subra ni faraja (baada ya dhiki faraja); kama ilivyofahamisha kauli yake kuwaambia wanawe “Wala msikate tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu.”
Tukiunganisha kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu katika ndoto ya Yusuf udogoni mwake natija ni kuwa Yaa’qub ana matumaini ya uhai wa Yusuf hadi atakapokuwa mkubwa, lakini hajui yuko wapi na ana hali gani. Yuko utumwani au kwenye uhuru. Huo ndio ulikuwa wasiwasi wake.

Hakuna Kungoja Mema Yaje Yenyewe Wala Mabaya

Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye wala msikate tamaaa na faraja ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.”

Nendeni mkatafute wala msikate tamaa. Amekutanisha matumaini na kutenda. Maana yake ni kuwa. Ikiwa hakutakuwa na matendo basi Aya itakwenda kinyume; na uvivu utaambatana na kukata tamaa na yatakuwa matarajio bila ya kufanya kitu ni ujinga na upumbavu. Neno tafuteni linawajibisha kutenda kwa hisia zote dhahiri na batini.

Ndivyo alivyo mwenye akili akitokewa na janga lolote anajitahidi kuondoa visababishi vyake, ni sawa viwe ni ufisadi au uzembe.

Na anapopatwa na mazuri huhofia asijisahau akapetuka mpaka kwa utajiri au cheo kikamletea kiburi. Kwa hiyo hujikinga kwa takua:

فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ {99}

“Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.” Juz. 9 (7:99).

Kwa ufupi ni kuwa mwenye kutaraji mabaya ni yule asemaye hakuna faida ya kujisumbua, na mvivu ni yule mwenye kutaraji mazuri yaje yenyewe.

فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَيْهِ قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ مَسَّنَا وَأَهْلَنَا الضُّرُّ وَجِئْنَا بِبِضَاعَةٍ مُزْجَاةٍ فَأَوْفِ لَنَا الْكَيْلَ وَتَصَدَّقْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّ اللَّهَ يَجْزِي الْمُتَصَدِّقِينَ {88}

Basi walipoingia kwa Yusuf walisema: “Ewe mheshimiwa! Imetupata shida sisi na watu wetu na tumeleta mali kidogo, basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka; hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka.”

قَالَ هَلْ عَلِمْتُمْ مَا فَعَلْتُمْ بِيُوسُفَ وَأَخِيهِ إِذْ أَنْتُمْ جَاهِلُونَ {89}

Akasema: “Je, mnajua mlivyomfanyia Yusuf na ndugu yake mlipokuwa wajinga?”

قَالُوا أَإِنَّكَ لَأَنْتَ يُوسُفُ ۖ قَالَ أَنَا يُوسُفُ وَهَٰذَا أَخِي ۖ قَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا ۖ إِنَّهُ مَنْ يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ {90}

Wakasema: “Je, wewe ni Yusuf?” Akasema: “Mimi ni Yusuf na huyu ni ndugu yangu! Mwenyezi Mungu ametuneemesha. Hakika mwenye takua na akasubiri basi Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wafanyao mema.”

قَالُوا تَاللَّهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّهُ عَلَيْنَا وَإِنْ كُنَّا لَخَاطِئِينَ {91}

Wakasema: Wallah! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha kuliko sisi na hakika sisi tumekuwa ni wenye hatia.”

قَالَ لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ اللَّهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ {92}

“Leo hapana lawama juu yenu, Mwenyezi Mungu atawasamehe naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wenye kurehemu.”

اذْهَبُوا بِقَمِيصِي هَٰذَا فَأَلْقُوهُ عَلَىٰ وَجْهِ أَبِي يَأْتِ بَصِيرًا وَأْتُونِي بِأَهْلِكُمْ أَجْمَعِينَ {93}

Nendeni na kanzu yangu hii na muirushe usoni mwa baba yangu atakuwa ni mwenye kuona, na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.”