read

Aya 88 – 93: Mimi Ni Yusuf

Maana

Basi walipoingia kwa Yusuf walisema: “Ewe mheshimiwa! Imetupata shida sisi na watu wetu na tumeleta mali kidogo, basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka.”

Yaa’qub aliwausia wanawe warudi Misr, wakakubali na wakarudi mara ya tatu, wakaingia kwa mheshimiwa wakiwa hoi, wakiomba wahurumiwe na wakaanza kulalamika njaa: tumepatwa na shida pamoja na watu wetu, tupe sadaka, mali yetu ni kidogo, Mungu anawapenda wanaotoa sadaka. Zama huwa zinageuka. Walisema haya wakiwa ni wajukuu wa Ibrahim (a.s.) lakini shida imewazidia mambo yakawa kwa namna ambayo hawakutegemea.

Akasema: “Je, mnajua mlivyomfanyia Yusuf na ndugu yake mlipokuwa wajinga?”

Baada ya Yusuf kusikia malalamiko ya ndugu zake na kusikia shida ya watu wake alishikwa na huruma za udugu, akawaambia kuwalaumu au kuwapa mawaidha kuwa mnakumbuka mlipomwitikia shetani mkamtupa ndugu yenu Yusuf kisimani. Baadae mkamsumbua sana mdogo wake Bin-yamin. Juzijuzi tu mlisema kuwa kama ameiba basi nduguye pia aliiba huko nyuma? Je, mjinga anaweza kufanya zaidi ya mlivyofanya?

Wakasema: “Je, wewe ni Yusuf?”

Wafasiri hapa wana maneno yasiyoafikiana na Aya, lakini yanaafikiana na maudhui na yanasaidia kuzingatia. Kwa ufupi ni haya: Nduguze Yusuf waliposikia maneno ya Yusuf, walianza kukumbuka umbile la Yusuf, uso wake, sauti yake na ishara za mikono yake.

Kwa vyovyote iwavyo wao au baadhi yao walianza kufikiria kuwa huyo ni Yusuf ndipo wakaanza kusema Je, wewe ni Yusuf? Walisema hivi wakiwa wanangoja jawabu. Basi likawa jawabu ambalo hawakulitegemea:

Akasema: “Mimi ni Yusuf na huyu ni ndugu yangu, Mwenyezi Mungu ametuneemesha.”

Namtaka msomaji asimame hapa kidogo alinganishe walikuwaje walipoambiwa hayo kulinganisha na walivyokuwa siku walipomtupa kisi- mani wakiwa hawana dini wala huruma ya udugu?!

Hakika mwenye takua na akasubiri basi Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wafanyao mema duniani na Akhera.

Makusudio ya wafanyao mema ni wale waliofanya na wakavumilia na kuwa na subira kwenye misukosuko waliyoipata na wakawa mara kwa mara wanazidiwa na waovu, lakini mwisho ni wa wacha Mungu. Ushahidi wa hilo hauanzii kwenye zama za Namrud na kuishia kwa Hitlar tu.

Binadamu leo anakabiliwa na mitihani ya Uzayuni na ukoloni wa Amerika ambao ndio washari wakuu na wafisadi. Hatuna shaka kwamba mwisho wa wote hao utakuwa kama mwisho wa mataghuti waliotangulia.

Hatusemi hivi kwa ushabiki, isipokuwa hiyo ni hali halisi ya kihistoria. Haki ina wenyewe wanaoitafuta na kujitolea mhanga na kwamba heri ina nguvu inayoisaidia, na iko siku itashinda dhidi ya dhulma na utaghuti.
Wakasema: “Wallah! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha kuliko sisi na hakika sisi tumekuwa wenye hatia.”

Walikiri kuwa Mwenyezi Mungu amemfadhilisha kuliko wao kimali, elimu, akili, uzuri na hatimae kwa cheo na heshima. Wakakiri makosa na kuomba msamaha. Yusuf mkarimu na mwana wa mkarimu alisema:

Leo hapana lawama juu yenu, Mwenyezi Mungu atawasamehe

Yusuf alisamehe yaliyopita bila ya nguvu wala lawama na akawaombea Mungu awasamehe waliyoyakosea naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wenye kurehemu, kwa yule anayetubia na akarudi nyuma. Katika Nahjul balagha imesemwa: “Hasira hazimfanyi kuacha huruma wala huruma hamufanyi kuacha kuadhibu”.

Kuna hadith Mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba alipopata ushindi wa kuiteka Makka aliwaambia makuraish: “Je, mnadhani nitawafanya nini?” Wakasema: “Sisi tunadhania heri tu, ndugu mkarimu na mwana wa ndugu mkarimu.” Akasema: “Basi nendeni zenu nimewaachia huru, leo hapana lawama juu yenu; kama alivyosema ndugu yangu Yusuf.”

“Nendeni na kanzu yangu hii na muirushe usoni mwa baba yangu atakuwa ni mwenye kuona na mje nao watu wenu wote wa nyum- bani.”

Hebu turudi nyuma kwenye Aya 18 ya Sura hii iliyoko Juz. 12, ili tulinganishe kati ya kanzu ya kwanza na hii ya pili: Ya kwanza ilimletea Ya’qub balaa na ugonjwa. Ya pili ikamletea raha na dawa. Vile vile tulinganishe baina ya hali ya wanawe walipoleta ya kwanza walijiomboleza na walipoleta ya pili walikuwa na furaha.

Kama mtu atauliza: iweje kanzu irushwe usoni na kuponyesha? Tutajibu kuwa hatupati tafsiri nyingine isipokuwa muujiza; sawa na moto wa Ibrahim, fimbo ya Musa na kuzungumza kwa Isa akiwa mchanga.

وَلَمَّا فَصَلَتِ الْعِيرُ قَالَ أَبُوهُمْ إِنِّي لَأَجِدُ رِيحَ يُوسُفَ ۖ لَوْلَا أَنْ تُفَنِّدُونِ {94}

Na ulipoondoka msafara, baba yao alisema: “Hakika mimi ninasikia harufu ya Yusuf, lau kama hamtanipuuza.”

قَالُوا تَاللَّهِ إِنَّكَ لَفِي ضَلَالِكَ الْقَدِيمِ {95}

Wakasema: Wallah hakika wewe bado uko katika upotevu wako wa zamani.”

فَلَمَّا أَنْ جَاءَ الْبَشِيرُ أَلْقَاهُ عَلَىٰ وَجْهِهِ فَارْتَدَّ بَصِيرًا ۖ قَالَ أَلَمْ أَقُلْ لَكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ مِنَ اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {96}

Alipomfikia mbashiri aliirusha kanzu usoni pake akarejea kuona. Akasema: “Je, sikuwaambia kuwa mimi ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua?”

قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ {97}

Wakasema: “Ewe baba yetu! Tuombee maghufira kwa dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa ni wenye hatia.

قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {98}

Akasema: “Nitawaombea msamaha kwa Mola wangu. Hakika yeye ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.”