Aya 99–102: Kukutana Yusuf Na Ya’qub
Na walipoingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: “Ingieni Misr, Inshallah, mko katika amani.”
Ya’qub alihuzunika sana kwa kumkosa Yusuf, alilia sana huku akijua kuwa kilio hakitafanya kitu, lakini alikuwa akipunguza joto la kufarikiana. Huzuni yake iliendelea kwa muda mrefu sana. Kwa sababu Yusuf alikaa miaka kadha katika nyumba aliyonunuliwa, miaka gerezani, miaka ya kuwa mtumishi wa serikali, ikafuata miaka saba ya mavuno ndipo ikaja miaka ya ukame.
Kila muda ulivyokuwa ukizidi kuendelea ndipo huzuni ya Ya’qub ilivyoendelea; kama inavyoashiria kauli ya waliomwambia: “Wallah hakika wewe bado uko katika upotevu wako wa zamani.”
Tukijua kiwango cha huzuni aliyokuwa nayo Ya’qub kwa kumkosa mwanawe, ndipo tutakapojua kiwango cha furaha aliyokuwa nayo kwa kukutana na Yusuf. Kwa sababu furaha ya kupona ugonjwa inakuja kwa kiwango cha maumivu yalivyokuwa au kuzidi furaha.
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa makusudio ya wazazi wake ni baba yake na mama yake mdogo (khalat), kwa sababu mama yake alikuwa ameshakufa. Wengine wakaenda mbali, kwamba mama yake alifufuliwa kaburini, ili aone utukufu wa mwanawe na aweze kumsujudia. Wala hakuna haja ya uhakiki huu na mfano wake; isipokuwa ni kurefusha maneno tu.
Unaweza kuuliza, kuwa kifua cha Aya hakiafikiani na mgongo wake, kwa sababu kifua kinasema, Walipoingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake, na inajulikana kuwa Yusuf alikuwa Misr. Mgongo nao unasema: Ingieni Misr, wakati wao tayari wako Misr kwa Yusuf?
Imesemekana katika jawabu kuwa Yusuf, aliwajengea hema wazazi wake karibu na mpakani huko ndiko walikoingia na akawakumbatia, na walipoanza mwendo wa kutoka kwenye hema wakielekea Misr ndipo alipowaambia ingieni Misr. Jawabu hili linachukua tamko la Aya zaidi ya inavyochukulika. Sio mbali kuwa makusudio ya ingieni Misri ni kaeni humo kwa amani; kama ilivyotokea. Ambapo mfalme aliwakatia ardhi yenye rutuba na kizazi cha Ya’qub kikandelea hapo kwa muda mrefu.
Imelezwa katika Majmaul-bayan “Aliwaambia mko katika amani, kwa sababu wao hapo mwanzo walikuwa wakimuhofia mfalme wa Misr, wala hawawezi kuingia ila kwa Pasipoti yake –yaani pasi za safari kama hivi sasa – Amesema Wahab: kwamba watu wa Ya’qub waliingia Misr wakiwa ni watu 73 na wakatoka pamoja na Musa wakiwa ni watu 600570” Vilevile imeelezwa katika Majmaul-bayan kuwa baina ya Yusuf na Musa kuna miaka 400.
Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi.
Aliwakalisha kwenye kiti ambacho alikuwa akikaa yeye akiwa anaendesha mambo ya serikali, kwa ajili ya kuwaadhimisha.
Na wakapomoka kumsujudia.
Waliopomoka ni wazazi pamoja na ndugu zake na aliyesujudiwa ni Yusuf, yaani wazazi wake pamoja na ndugu zake walimsujudia Yusuf. Makusudio ya kusujudi hapa ni kiasi cha kuinama kwa kumuadhimisha na kumtukuza. Na ilikuwa kuinama ndio maamkuzi ya heshima wakati huo, kama ilivyoelezwa katika baadhi ya tafsir.
Imesekana kuwa waliyemsujudia ni inamrudia Mungu na kwamba sijda ilikuwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa sababu ya neema hii kubwa. Lakini kauli hii inapingana na dhahiri ya Aya wala haifikiani na kauli ya Yusuf katika Aya ya 4. “nimeota zikinisujudia.” Yaani kumsujidia yeye sio mwengine.
Na akasema: “Ewe baba yangu! Hii ndio tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe ya kweli.”
Anaishiria kauli yake katika mwanzo wa Sura hii, Juz. 12 : “Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja na jua na mwezi nimeo- ta zikinisujudia.” Maelezo yake na ufafanuzi uko huko.
Katika tafsir ya Razi, imeelezwa: “Wametofautiana katika kiwango cha muda baina ya kuota ndoto na kukutana. Ikasemekana ni miaka 80, wengine miaka 70 na ikasemwa ni miaka 40, na hiyo ndio kauli ya wengi; na kwamba umri wake aliishi miaka 120”
Sisi hatujui kwa yakini umri wake ulikuwa miaka mingapi alipotiwa kisimani wala muda aliokaa katika nyumba aliyonunuliwa au muda wake gerezani na kutumikia serikali.
Kwa sababu hatukupata kauli yoyote ya kutegemea kutuongoza kwenye hilo na kauli za wafasiri zimegongana, lakini wengi wamesema kuwa aliishi miaka 120.
Na Mwenyezi Mungu alinifanyia wema kunitoa gerezani na kuwaleta nyinyi kutoka jangwani.
Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humjaribu mtu kwa raha, kama anavyomjaribu kwa shida. “Akasema: Haya ni katika fadhila za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru?” (27: 40). Imam Ali (a.s.) anasema: “Hazikuadhimishwa neema za Mwenyezi Mungu na yoyote ila huzidi haki ya Mwenyezi Mungu juu yake kwa cheo”
Yusuf alipata majaribu ya tabu akavumilia, na ya raha akashukuru. Ndio hapa anazizungumza neema za Mwenyezi Mungu juu yake na kuzihesabu hisani alizofanyiwa: amenitoa gerezani, akanitukuza kwenye cheo na akawaleta watu wangu wa nyumbani, ambapo walikuwa jangwani wakifuga ngamia na mbuzi na kondoo ambao pia nao walimalizwa na ukame wakawa kwenye ardhi tupu isiyo na chochote, wakimwambia mheshimiwa: “Fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka”
Wala hakutaka kutaja kutolewa kwake kisimani kwa kuchunga hisia za ndugu zake. Vile vile uadui wao aliuelekeza kwa shetani bila ya kuuelekeza kwao moja kwa moja kwakusema:
Baada ya shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni mpole kwa alitakalo. Anawafanyia upole wema na kuwafikisha anapotaka kwenye enzi na utukufu.
Hakika yeye ni Mjuzi Mwenye hekima.
Tofauti baina ya ujuzi wake na hekima yake ni kwamba vitendo vyake vyote na hukumu zake zinakuja kulingana na hekima. “Ewe Mola wetu hukuviumba hivi bure” Juz.4 (3:919).
Ama elimu yake, haiepukani na kinachojulikana. Kwa maneno mengine ni kuwa elimu yake ni kukiambia kitu kuwa kikawa.
Ewe Mola Wangu! Hakika umenipa utawala na umenifunza tafsiri ya matukio. Ewe mvumbuzi wa mbingu na ardhi! Wewe ndiwe mtawala wangu katika dunia na akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Mwislamu na unikutanishe na watu wema.
Maana ya mvumbuzi ni kuwa ameziumba bila ya mfano mwingine uliotangulia. Ametaja mbingu kwa tamko la wingi na ardhi kwa tamko la umoja kwa vile mtu huona kwa macho yake mbingu nyingi, lakini haoni isipokuwa ardhi moja.
Maana ya wewe ni mtawala wangu ni kuwa wewe ndiye unayosimamia mambo yangu yote ya dunia na akhera. Baada ya Yusuf kutaja, neema za Mwenyezi Mungu kwake, alimwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kumshukuru kwa utawala aliompa na kumuhusisha na utume, akiwa amewakilisha kwake mambo yake yote huku akimwomba afe kwenye utifu na radhi zake Mwenyezi Mungu na pia amjumuishe na watu wema waliopita miongoni mwa wazazi wake na amjalie ni kizazi chema kilichobakia baada ya wazazi wake.
Hayo ni katika habari za ghaibuu tulizokupa wahyi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kisa cha Yusuf, alimwelekea Mtume wake mtukufu Muhammad (s.a.w.) kwa Aya hii. Lengo ni kutoa hoja kwa anayekanusha utume wake.
Ufupisho wake ni kuwa hayo tuliyoyasimulia kuhusu Yusuf, kwa ufafanuzi huu, hakuyashuhudia Muhammad (s.a.w) wala kuyasoma katika kitabu au kusikia kutoka kwa mtu yeyote, isipokuwa ni Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaojulisha ukweli wake na utume wake.
Na hakuwa pamoja nao walipoazimia shauri lao wakipanga njama.
Walioazimia ni ndugu wa Yusuf. Anayeambiwa ni Muhammad (s.a.w.). Watu wote wanajua kuwa Muhammad (s.a.w.) hakuwako wakati walipofanya shauri la kumtupa Yusuf shimoni na pia walipofanya njama kwa baba yake kusema kuwa ameliwa na mbwa mwitu.
Vilevile watu wanajua kuwa Muhammad (s.a.w.) hakusoma kitabu wala kuwa mwanafunzi wa ustadh yeyote. Kwa hiyo basi hakuna njia iliyobaki ya kuyajua hayo isipokuwa wahyi wa mbinguni.
Mfano wa Aya hii ni ile isemayo: “Hizo ni habari za ghaibuu tunazokupa wahyi. Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.” Juz.12 (11:49)
Je, Kisa Cha Yusuf Ni Cha Mapenzi?
Kwa mtazamo wa juu juu, inaweza kudhaniwa kuwa sura ya Yusuf inafanana na kisa ambacho mhusika mkuu ni mwanamke aliyetawaliwa na tabia ya kike iliyompa ashiki kwa kijana mtanashati ambaye hajapatapo kumuwaza mwingine mfano wake kwa uzuri, na kwamba kijana huyo alijizuia kwa uchaji Mungu wake na kuhofia hisabu na malipo ya Mungu, sawa na kisa cha Sallam Mughniya pamoja na Abdurrahman Al-Qass.1
Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa ingelikuwa vizuri kama kisa hiki kisingetajwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Baadhi ya waumini wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ana hekima ya ndani katika Sura hii ambayo hatuijui.
Hawa wakawa wamejichunga sana; kama walivyokosea Khawarij Maymuniya walipoikana sura ya Yusuf kwa vile ni kisa cha mapenzi jambo ambalo liliwatoa nje ya madhehebu ya Kiislamu.
Hakika tuliyoishilia nayo, wakati tukifasiri Sura hii ni kwamba mwenye kuisoma kwa kuitilia manani na kuzingatia maana yake (Tadabbur) na akagundua siri zake na malengo yake ataamini kabisa kwamba Sura hii inaeleza mfano ulio wazi zaidi kuwa mara nyingi kushikamana na msimao wa kiroho ni nyenzo ya kufaulu katika maisha haya yaliyojaa ufisadi.
Mwenye kuisoma kijujuu atasema kama walivyosema Maymuniya kuwa ni kisa cha mapenzi au walivyosema baadhi ya waumini kuwa Mungu ana hekima isiyojulikana katika kisa hiki. Ni kweli hawezi kuijua isipokuwa yule mwenye kuyazingatia vizuri (kuyafanyia tadabbur) maneno ya Mwenyezi Mungu na Aya zake.
Tutaonyesha baadhi ya uhakika ulioko kwenye sura hii unaojitokeza kwa kila mwenye kuutafuta, kama ifutatavyo:-
1. Mvutano baina ya haki na batili unaendelea daima katika maisha haya, wala haitapatikana suluhu baina yake. Natija ya kimaumbile ya hilo ni kwamba mwenye kufuata njia ya batili atapata upinzani kutoka kwa wenye haki, lakini kwa njia ya uadilifu na ukweli, sio kwa uwongo na hadaa. Kwa sababu wao hawaitaki silaha isiyokubaliwa na haki na uadilifu.
Vile vile naye mwenye kufuata njia ya haki atapigwa vita na wabatilifu, lakini kwa uzushi na kila aina ya vitimbi. Kwa sababu mwenye kung’ang’ania ubatilifu, hana silaha isipokuwa kupotoa na kuzulia. Ndio maana haki ikawa ni ghali na yenye takilifa nyingi kwa anayeifuata na kushikamana nayo.
Mwenyezi Mungu amepigia mfano wa hakika hii kwa Sura ya Yusuf. Mke wa mheshima alimtaka Yusuf, lakini akakafaa na akajihifadhi kwa sababu ya kumcha Mungu (takua).
Akamtishia kifungo kama hatafanya lakini akajizuia na wala asifanye huku akisema: “Ewe Mola wangu! Gereza linapendeza zaidi kwangu kuliko haya wanayoniitia”. Kwa hiyo akajitolea kwa thamni ghali kuliko nafsi yake kwa sababu dini ina thamani na ni ghali zaidi.
Hata hivyo wale wanaoipinga haki mwisho wanaangusha silaha chini kwa wenye haki, kama ilivyotokea kwa nduguze Yusuf na mke wa mheshimiwa.
2. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : “Kama asingeona dalili ya Molawake,”inatupaudhibitiwakiujumlanamakisiosahihiyamapambano baina ya mumin na asiyekuwa mumin. Mwenye kuitikia buruhani hii wakati wa mtihani, kama alivyofanya Yusuf, basi huyo ni katika wale ambao imani na yakini imetulizana katika nyoyo zao kwa haki na uadilifu. Na mwenye kusukumwa na matamanio na shahawa zake na akajitia hamnazo akaacha buruhani ya mola wake, basi huyo hana dini kitu.
3. Yanapotokea matatizo watu wema wanajulikana na kuwa ni tegemeo la watu, kama alivyo tegemea mfalme wa Misr kwa Yusuf akiwa yuko gerezani, ili aweze kuikinga nchi na balaa la miaka ya ukame. Hali ya ufisadi inawainua waovu na kuwaweka chini wema, lakini shida na matatizo yanadhihirisha hakika ya mambo.
4. Kuizowesha nafsi kutegemea njia ya haki kutaleta natija nzuri na bora. Yusuf alivumilia kisimani, gerezani, kuuzwa kama mtumwa na kutuhumiwa, lakini natija ikawa yeye ndiye bwana mkubwa mheshimiwa, anaambiwa na mfalme “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima mwenye kuaminika.” Na nduguze Yusuf wanasimama wakiwa wamehemewa wakitaka kuhurumiwa huku wakisema: “basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka; hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka” Na mwisho wanakuja kumsujudia. “mvumilivu hula mbivu”.
Huu ndio mtazamo wa haraka haraka wa baadhi ya mazingatio na mafundisho ya sura hii tukufu. Mwenye kutaka ufafanuzi na aisome kwa ukamilifu pamoja na tafsiri yake.
وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ {103}
وَمَا تَسْأَلُهُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ {104}
وَكَأَيِّنْ مِنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ {105}
وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُمْ بِاللَّهِ إِلَّا وَهُمْ مُشْرِكُونَ {106}
أَفَأَمِنُوا أَنْ تَأْتِيَهُمْ غَاشِيَةٌ مِنْ عَذَابِ اللَّهِ أَوْ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {107}
- 1. Kinapatikana katika Aqdulfarid Juz 7