read

Aya 103-107: Na Watu Wengi Si Wenye Kuamini Aya

Na watu wengi si wenye kuamini ujapopupia.

Muhammad (s.a.w.) ana ishara na miujiza inayojulisha juu ya utume wake, zikiwemo sharia na sera zake. Nyingine ni Qur’an na ufasaha wake, mafunzo yake, uhakika wake na kutolea habari mambo ya ghaibuu. Miongoni mwa ghaibuu hizo ni kisa cha Yusuf kwa ufafunuzi wake, kama tulivyotaja katika Aya 102 ya Sura hii.

Mtume Muhammad (s.a.w.) alikuwa akipupia sana watu waamini na waongoke, hasa kaumu yake ya kiquraish, lakini wengi wao hawakuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya masilahi yao binafsi; kama vile viongozi na wenye nguvu, au kwa sababu ya ujahili na kuiga; kama vile wanyonge na wafuasi.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwambia mtume wake mtukufu kuwa wewe huwezi kumwongoza umpendaye pamoja na ikhlasi yako na miujiza yako na wewe huna haja nao wala imani yao.

Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Haikuwa hii ila ni mawaidha kwa walimwengu.

Neno ‘hii’ ni Qur’an ambayo inaongoza kwenye usawa ikizielekeza akili kwenye ishara za Mwenyezi Mungu na dalili za uadilifu na umoja wake. Inaongoza na kuelekeza kupitia mdomoni mwa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.)

Ni ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia na hali ya kuwa wanazipuuza.

Kana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake, wewe tulia moyo wako wasipokuamini wewe na dalili za utume wako, kwani wao wamenikufuru mimi nikiwa muumba wao na mwenye kuwaruzuku. Nimeujaza ulimwengu dalili za utukufu wangu na uwezo wangu, lakini bado wakazipinga. Basi hakuna ajabu wakikupinga wewe pamoja na miujiza iliyodhihiri mikononi mwako.

Na wengi wao hawamwamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.

Hili ni jawabu la swali linalokadirika kutokana na Aya iliyotangulia. “Na watu wengi siwenye kuamini ujapopupia”. Swali lenyewe linakuja hivi: Vipi Mwenyezi Mungu aseme watu wengi hawaamini na inajulikana kuwa waarabu na watu wa Kitabu wanakiri kuweko muumba na wao ndio waliokuwa watu wengi wakati huo? Bali Qur’an yenyewe inakubali hilo wazi wazi pale iliposema: “Na ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema ni Mungu”(29:16).

Kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akajibu swali hili la kukadiriwa kwa kusema wengi wao kuamini kwao hakuachani na ushirikina, yaani wanamshiriksha Mungu. Wanakubali kuwa mumba yuko, lakini wengi wao wana mfanyia washirika.

Kwa mfano Mayahudi au kikundi katika wao wanasema Mungu ana mtoto anayeitwa Uzayr. Manaswara (wakirsto) nao wanasema mtoto wa Mungu ni Masih. Waarabu wanayashirikisha masanamu katika ibada wanamwambia Mwenyezi Mungu: labeka huna unayeshirikiana naye isipokuwa anayeshirikiana nawe. Kwa hiyo hakuna tofauti baina ya anayekanusha na anayeshirikisha .
Je wanaaminisha kuwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika au kuwafikia saa (kiyama) kwa ghafla na hali hawatambui?

Katika aya 103 Mweyezi Mungu(s.w.t.) alimwambia mtume wake kuwa wao hawakuamini katika 105 alimwambia wao wamenikufuru mimi hali ya kuwa ni muumba na katika 106 akasema hata wale wanaonikubali wananifanyia washirika. Ikawa ni mazoweya ya kuyafuatishia haya kwa makemeo na kiaga cha adhabu kali. Unaweza kuuliza: Kutaja ghafla hakuhitajii tena kutaja hawatambui, je, kuna lengo gani la kukaririka?

Jibu: Neno ghafla linaashiria kutokea adhabu wakiwa macho, lakini kutotambua inawezekana kuwa katika hali ya kuwa macho au kulala, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُهُ بَيَاتًا أَوْ نَهَارًا {50}

“Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu yake usiku au mchana.” Juz.11 (10:50).

قُلْ هَٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ {108}

Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa busara mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُوحِي إِلَيْهِمْ مِنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ ۗ أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۗ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {109}

Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipokuwa ni wanaume tuliowapa wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wenye takua. Basi hamtii akili?

حَتَّىٰ إِذَا اسْتَيْأَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا فَنُجِّيَ مَنْ نَشَاءُ ۖ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُنَا عَنِ الْقَوْمِ الْمُجْرِمِينَ {110}

Hata mitume walipokata tamaa na wakadhani kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusra yetu, wakaokolewa tuwatakao, na adhabu yetu haiondolewi kwa kaumu ya wakosefu.

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَٰكِنْ تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {111}

Kwa hakika katika simulizi zao mna mazingatio kwa wenye akili. Si hadithi za kuzuliwa, lakini ni kusadikisha yaliyo kabla yake na ufafanuzi wa kila kitu na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.