Aya 2-4: Ameinua Mbingu Bila Ya Nguzo
Maana:
Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona.
Yaani mnaziona hizo mbingu. Maana ni kuwa hakika Mwenyezi Mungu ameziinua mbingu kwa amri yake nazo zimeinuliwa hasa kama mnavyoziona bila ya nguzo.
Katika Mustadrak Nahjul-balagha imeelezwa kuwa Imam Ali (a.s.) alizisifu mbingu kwa kusema: “Ameinua mbingu bila ya nguzo – yaani kihalisi na kidhahiri – na akaitandika ardhi hewani bila ya nguzo”.
Kisha akatawala kwenye arshi.
Hili ni fumbo kuwa yeye anamiliki ulimwengu na kupangilia mambo yake kwa elimu yake na hekima yake, kama alivyosema: ‘Anayepanga mambo.’ Jumla hii imekwishapita katika Juz. 8 (7:54) na katika Juz. 11 (10:3).
Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa.
Kwa nidhamu, kama yaonavyo macho yetu na kwa lengo maalum kama zinavyotambua akili zetu.
Jua linapita kwenye falaki yake katika mwaka, na mwezi nao unapita kwenye falaki yake kwa muda wa mwezi mmoja. Vilikuwa hivyo tangu mamilioni ya miaka iliyopita na vitaendelea hivyo mpaka atakapotaka Mwenyezi Mungu.
Hakuna mwaka unaotofautiana na mwingine wala muda unaotofautiana na muda mwingine. Hii ni dalili mkataa ya kuweko mjuzi mwenye hekima. Ama sadfa inabatilishwa na nidhamu na kukaririka mambo.
Anayapanga mambo yote bila ya kubakisha, yakiwemo kulitiisha jua na mwezi, kutuma mitume kuteremsha vitabu n.k.
Anazipambanua ishara. Anabainisha dalili za kupatikana kwake. Kwa nini anafanya hivyo?
Ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Mola wenu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ulimwengu na akaupanga kwa ukamilifu katika njia zote. Akili iliyosalama inatambua mipangilio hii na kupata dalili kwayo ya kupatikana mzingatiaji mwenye hekima na uweza wake wa kurudisha viumbe.
Kwa sababu mwenye kuweza kuuleta ulimwengu uliokuwa hauko na akaupangilia pamoja na vilivyomo ndani yake, zikiwemo nyota na sayari nk, kwa mpangilio wa kiuhakika, basi bila shaka atakuwa na uwezo zaidi wa kuukusanya pamoja baada ya kutawanyika.
Ukithibiti kwa akili uwezo wa kuurudisha, na mkweli mwaminifu akautolea habari kwa wahyi, basi kutokea kwake ni kwa lazima.
Baada Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja mbingu ametaja ardhi na lengo ni moja - kuwatanabaisha walioghafilika kwenye dalili za kiulimwengu za kupatikana Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
Na kwamba mwenye kuumba ulimwengu huu mkubwa pamoja na ardhi yake na mbingu yake anaweza kutuma mitume na kuteremsha vitabu, kufufua wafu.
Dalili hizo miongoni mwake ziko za mbinguni; kama vile kuinua mbingu bila ya nguzo, kulitiisha jua na mwezi n.k. Na nyingine ni za ardhini; kama zile alizoziashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli zifuatazo:
1. Na yeye ndiye aliyeitandaza ardhi yaani aliyeitandika.
Mahali pengine Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَاللَّهُ جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ بِسَاطًا {19}
وَالْأَرْضَ بَعْدَ ذَٰلِكَ دَحَاهَا {30}
Inavyoonyesha ni kwamba kutandazwa ardhi na kutandikwa pamoja na upana wake, hakuna uhusiano wowote na kuwa ardhi ni mviringo au ni bapa. Kwa sababu kitu kikiwa kikubwa sana, kama ardhi, kila upande wake unakuwa umeenea kwa upana na urefu, hata kama kiko mviringo.
Kwa hiyo basi Aya haizuii kuwa ardhi ni mviringo, jambo ambalo halina shaka. Razi anasema katika kufasiri Aya hii: “Hakika imethibiti, kwa dalili kwamba, ardhi ni tufe na ardhi ni kitu kikubwa na tufe likiwa ni kubwa sana basi kila sehemu yake inaonekana kama bapa.”
Wataalamu wa Kiyunani (kigiriki) katika enzi za Aristatle, waliafikiana kuwa ardhi ni mduara, lakini wakasema kuwa imetulia.
2. Na akaweka humo milima.
Neno milima limefasiriwa kutoka na neno Rawasi lenye maana ya kila kitu kilichothibiti mahali, lakini neno hili limetumika zaidi kwa milima, kiasi ambacho likitajwa tu bila ya nyongeza, inafahamika kuwa ni milima.
Hekima ya kupatikana hiyo milima ni utulivu wa ardhi na uthabiti wake, Mwenyezi Mungu anasema: “Je, hatukuifanya ardhi kuwa ni tandiko na milima kuwa ni vigingi?” (78:7).
3. Na mito.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekutanisha kutaja milima na mito kwa sababu mito inachimbuka kutoka humo milimani. Anasema:
وَجَعَلْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ شَامِخَاتٍ وَأَسْقَيْنَاكُمْ مَاءً فُرَاتًا {27}
4. Na katika kila matunda akafanya humo viwili viwili–dume na jike.
Kila aina ya matunda ina dume na jike katika aina zake kwa dhahiri, kama vile mtende dume mtende jike, au kwa undani, kama mimea mingine.
Sheikh Al-Maraghi, katika tafsiri yake, anasema: “Imethibitisha elimu hivi sasa kwamba mti na mmea wowote hauzai matunda isipokuwa kwa ushirikiano baina ya wa kike na wa kiume. Aghlabu mbegu zinakuwa katika mti mmoja kama ilivyo miti mingi, au katika miti miwili tofauti, kama ilivyo kwa mtende.”
Katika jarida la Al-ulum la Lebanon toleo la Juni 1967 kwenye kichwa cha maneno “Vipi uhai unakuwa katika vitu”, imeelezwa kuwa vidudu vinachukua mbegu za uzazi kwenye mwili wake kupeleka kwenye makole ya maua bila ya kukosea, na kwamba ndege wanachukua mbegu za uzazi za yungi yungi kwenye midomo yao. Hakika ni muujiza.
Katika vita kuu vya ulimwengu vya pili walifika wapiganaji huko Corse. zaituni ikapata magonjwa na matunda yakapungua. Amerika ikataka kusaidia kutatua tatizo hilo. Kwa hiyo wakanyunyizia miti dawa ya DDT. Vidudu vya maradhi vikafa, lakini vikafa na vidudu vingine. Katika mwaka uliofuatia natija ikawa ni kutopatikana chochote! Si zaituni si limao wala lozi.
Kwa hiyo inatubainikia kuwa mimea haiwezi kuzaa matunda isipokuwa kwa kukutana mbengu za kike na za kiume.
5. Huufunika usiku kwa mchana.
Imepita tafsiri yake katika Juz. 8 (7:54).
Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaofikiri.
Katika ulimwengu huu ambao unakwenda kulingana na kanuni thabiti zisizotetereka kwa hali yoyote ile. Lau si uthabiti wake, isingeliwezekana kwa wataalamu kuuchunguza na kuuelewa. Ilivyo ni kwamba linalodumu linapinga sadfa. Na kwa ajili hii wataalamu wengi wa maumbile wameamini kuweko Mungu.
Na katika ardhi mna vipande vilivyokaribiana.
Ardhi imeungana, lakini kuna sehemu kadhaa zinazotofautiana, kuna tambarare, milima na mabonde. Pia kuna udongo mgumu na mchangatifu, changarawe na utelezi, weusi na weupe n.k. Siri ya hilo ni amri ya Mwenyezi Mungu na upangiliaji wake katika kuumba.
Na zipo bustani za mizabibu na mimea mingine na mitende ichipuayo kwenye shina. Ni mitende ya aina moja.
Na isiyochipua kwenye shina moja ni ile mitende inayotokana na mashina tofauti. Amehusisha kutaja mizabibu na mitende kwa sababu ndiyo matunda yanayopatikana sehemu nyingi au ndio yenye chumo na pengine ndiyo iliyokuwa muhimu wakati huo. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَاضْرِبْ لَهُمْ مَثَلًا رَجُلَيْنِ جَعَلْنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيْنِ مِنْ أَعْنَابٍ وَحَفَفْنَاهُمَا بِنَخْلٍ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمَا زَرْعًا {32}
Inanyweshwelezwa maji yale yale; kama vile mvua, kisima au mto. Pia sehemu ni moja kwa kukarubiana, lakini matunda yanatofautiana kirangi, ukubwa, harufu na hata ladhaa. Siri ya hilo ni upangiliaji wake Mwenyezi Mungu na hekima yake.
Na tunaifanya bora baadhi yake kuliko mingine katika kula pamoja na kuwa nyezo za kumea kwake ni aina moja.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotia akilini (mambo).
Yaani tofauti hii inayopatikana katika nyezo za aina moja, yakiwemo maji na hewa, ni dalili wazi ya kuweko mpangiliaji mambo vizuri, kwa yule ambaye haamini kitu ila baada ya kufikiri na kutia akilini.
Miongoni mwa kauli ya Imam Ali: “Hakuna elimu kama kufikiri wala hakuna fahari kuliko kunyeyekea”.
Sayyid Afghani Na Wanaomkana Mungu
Ufafanuzi mzuri wa Aya hii kwa ujumla ni majibu ya Sayyid, Jamaluddin Al-Afghani, kwa wale wanaokana kuweko Mwenyezi Mungu anasema: “Akiulizwa Darwin kuhusu miti iliyoko katika misitu wa India na mimea inayozaliana humo tangu zama za kale sana ambazo historia haijui muda wake, isipokuwa kudhania tu.
Mashina yake yote yako katika uwanja mmoja matawi yake yote yanakwenda kwenye anga moja. Sasa ni kitu gani kinachofanyika mpaka mmoja ukatofautiana na mwingine katika umbile lake, majani yake, kimo chake na ukubwa.
Vile vile maua yake, matunda yake na hata ladha yake? Ni, kitu gani cha nje kilichoathiri mpaka ikapatikana tofauti katika makuzi ya aina moja, maji na hewa ya aina moja? Nadhani hawezi kupata jibu la hayo
Akiulizwa kuhusu hawa samaki wa mto Oural na wa bahari ya Qazwini (Caspian sea) wanashirikiana katika vyakula, lakini wanatofautiana kabisa kimaumbile, je kuna sababu gani ya kutofautiana huku? Sioni kama ataweza kuwa na majibu isipokuwa kushindwa.”
Unaweza kuuliza kuwa Darwin anaweza kumjibu Sayyid Afghani kwamba wataalamu wa mimea wanajua sababu ya kutofautiana huku na wanaweza kuifichua kwa kila anayetaka na kupendelea. Kwa hiyo basi, hakuna dharura, katika hali hii, kulazimika kuweko mpangiliaji?
Jibu: Tuchukulie kuwa wataalamu wa mimea wanajua sababu ya hilo, lakini ujuzi wao utakuwa na kiwango cha kujua sababu ya karibu ya hilo.
Na kama wakiulizwa sababu ya mbali iliyosababisha hii ya karibu hawatapata isipokuwa moja ya sababu mbili: Ama sadfa au kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Sababu ya kwanza itakuwa batili kwa sababuu sadfa haikaririki wala kudumu. Kwa hiyo itabaki sababu ya pili.
Mara kadhaa tumebainisha kuwa ni desturi ya Qur’an kutegemeza matukio yote ya kimaumbile kwenye sababu yake ya kilimwengu.
Hilo ni katika kukitegemeza kitu kwa mtendaji wake wa kwanza, kwa lengo la kukumbusha kuweko Mwenyezi Mungu na kwamba yeye ndiye muumba wa ulimwengu wote pamoja na ardhi yote na mbingu yake.
Unaweza kusema tena: Wakana Mungu nao wanaweza kuuliza: Kuna sababu gani ya kuweko mpangiliaji mambo?
Jibu: Hakika swali hili sio la msingi kwa sababu kuweko mpangiliaji hakuna sababu na kwamba yeye ndiye msabibishaji sababu. Kuuliza sababu ya kuweko msababishaji ni sawa na kuuliza: Nina ni aliye muumba Mungu baada ya kufaradhia kuwa yeye ni muumba sio muumbwa.
Au kuuliza sababu ya kusadikisha jicho lilichokiona na sikio lilichokisikia na huku tunaamini kuwa hiyo ni hoja mkataa ya kila shaka na kila shubha.
وَإِنْ تَعْجَبْ فَعَجَبٌ قَوْلُهُمْ أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۗ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ۖ وَأُولَٰئِكَ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ ۖ وَأُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {5}
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِمُ الْمَثُلَاتُ ۗ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ لِلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ ۖ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ الْعِقَابِ {6}
وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِنْ رَبِّهِ ۗ إِنَّمَا أَنْتَ مُنْذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ {7}