Aya 5-7: Kweli Tutakua Katika Umbo Jipya?
Na kama ukistaajabu basi cha ajabu ni usemi wao: ‘Ati tutakapokuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya?’
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.) wasemaji ni washirikina waliokana utume wake. Maana ni kuwa ikiwa ewe Muhammad utashangazwa na ibada ya masanamu ya washirikina na kukanusha kwao utume wako, basi la kushangaza zaidi ni kukadhibisha kwao ufufuo.
Kwa sababu wao wanakubali kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Muumba wa ulimwengu, na mwenye kuweza hilo si anakuwa na uwezo zaidi wa kumrudisha mtu baada ya kufa kwake?
Hao ndio waliomkufuru Mola wao na hao ndio watakokuwa na minyororo shingoni mwao na hao ndio watu wa motoni. Humo watadumu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja neo ‘hao’ mara tatu kuelezea kwa ufasaha zaidi hasira zake na kuchukia kwake. Kauli yake: Hao ndio waliomkufuru Mola wao, inafahamisha kuwa Mwenye kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni muumba wa ulimwengu inamlazimu yeye, kwa hali yoyote, kuamini kuwa yeye ni muweza wa kuwafufua walio makaburini. Atakayepinga hilo atakuwa moja kwa moja amemkufuru Mwenyezi Mungu atake asitake.
Mwenye kuchanganya imani ya Mungu na kushindwa kufufua watu, atakuwa amechanganya mambo mawili yanayopingana. Washirikina wamepinga ufufuo, kwa vile, kulingana na madai yao, Mwenyezi Mungu hawezi; kama inavyojulisha kauli yao “Ati tutakapokuwa…” Kwa hiyo, ilivyo hasa, ni kuwa wao wanampinga Mwenyezi Mungu kwa ndimi zao.
Wanaoamini Maada Na Maisha Baada Ya Mauti
Wanaoamini maada wanakana kuweko Mwenyezi Mungu, sana sana wanapinga maisha baada ya mauti. Dalili yao ni moja tu haibadiliki wala haigeuki. Nayo ni kuwa kila linaloweza kuhisiwa na kushuhudiwa inapasa kuliamini na kila lisiloweza kuhisiwa inapasa kulikana na kulipinga.
Kwa hiyo, kwao, hisia ya dhahiri peke yake ndiyo dhahiri na ndiyo batini, ndiyo ya mwanzo na ya mwisho; kama wanavyosema. Vipi wataamini Bustani (Pepo) nao hawajala matunda yake, vipi wakubali kuwa kuna Jahannam na moto wake haujawafikia?
Sisi nasi, kwa upande wetu, tunauliza hivi: Mmepata wapi elimu au imani ya kuwa hisia za dhahiri pekee ndiyo njia ya haki na hali halisi, na kwamba mengineyo ni upuuzi? Mkisema hayo mmeyajua kupitia hisia, tutasema:
Sisi pia tunazo hisia na hatujamuona mwingine zaidi yenu akisema kuwa msiamini isipokuwa hisia. Ikiwa mtasema mmejua hilo kwa njia nyingine isiyokuwa hisia, basi mtakuwa mmejipinga wenye kwa kuamini kisichoshuhudiwa na hisia.
Mnamo mwaka 1962 nilitunga kitabu kuwajibu wanaoamini maada, kwa jina Falsafatul-Mabda’ (falsafa ya misingi). Kisha baadae nikasoma mambo mengi kuhusu wanavyoamini wa maada na majibu yao; miongoni mwayo ni:
1. Kwa mujibu wa wanaoamini maada ni lazima kutokuweko tofauti yoyote baina ya mtu aliye na miujiza na vidudu duni vinavyotokana na uchafu kwa vile wote hao ni watoto wa sharia ya sadfa na maumbile pofu yasiyokuwa na mipangilio yoyote .
2. Wataalamu wamepata katika ubongo wa binadamu nyuzi milioni elfu 14 zimefumwa na kupangiliwa vizuri sana kwa namna ambayo wahandisi wakuu wote hawawezi; kiasi ambacho unyuzi mmoja tu ukienda kombo basi mtu hatakuwa na utambuzi au atachanganyikiwa, sawa na umeme ukiharibika moja ya nyaya zake. Hakuna tafsiri ya hayo, kwa mwenye akili, isipokuwa kuweko mpangiliaji mwenye hekima asiyeweza kuonwa kwa jicho, kusikiwa na sikio, kuguswa kwa mkono, kunuswa na pua au kuonjwa kwa ulimi.
Kwa namna yoyote itakavyokuwa sadfa na muujiza, lakini haiwezi kufanya umeme; sikwambii kuunganisha nyuzi milioni elfu 14 zilizopangiliwa, kiufundi na kuwekwa kwenye chombo kimoja kwa idadi ya vichwa na bongo za binadamu wote; tena waweze kuhisi na kutambua.
3. Waamini maada wanasema kuwa ubongo wa binadamu ni sawa na akili ya mashine. Zote mbili zimetokana na vitu vilivyosukwa na kupangwa kuweza kuleta athari.
Mtaalamu wa kifaransa, aitwaye Caussine, aliwajibu kwa kusema: “ Iwapo gari yangu ya zamani ikianza kutoa sauti mbovu kama mtu aliyepatwa na ugonjwa wa baridi yabisi, inawezekana niseme kuwa gari yangu ina baridi yabisi? Na kabureta inapotatarika wakati ninapokanyaga mafuta, je, itafaa niseme kuwa gari yangu imepatwa na pumu?”
Nasi tunaongezea juu ya kauli ya mtaalamu huyu kwa kusema: mpangilio na utaratibu kwenye akili ya mashine umetokana na kitendo cha mtu, hilo halina shaka. Lakini ni nani aliyepangilia na akaweka mfumo kwenye ubongo wa binadamu?
Ikiwa binadamu amevumbua akili ya mashine, je akili hii ya mashine inaweza kuvumbua akili nyingine mfano wake au kitu duni kama pini? Katika kitabu Al-amal wal –Mukh (kazi na ubongo), kilichofasiriwa na Shakri Azir cha Mtaalamu wa Kirusi Yuri Bakhlov, anasema: “Wale wanaodhani kuwa kuna uwezekano wa mashine kuchukua nafasi ya akili ya binadamu wamekosea kosa kubwa sana… ubongo wa binadamu unatofautiana kabisa na chombo chochote katika utendaji kazi wake, uwelekevu na ustadi wake usio na kikomo. Ama akili ya mashine ina kikomo - kile alicho kiweka binadamu.”
4. Kuna ugunduzi mkubwa wa nyuki kuhusu vifaa vya kupunguza joto (viyoyozi). Kwamba nyuki aligundua kifaa hiki kabla ya binadamu. Joto linapozidi kwenye Masega ya nyuki kundi moja linaondoka kuleta maji kwa kutumia visiku vyao na kuyaweka kwenye tanki. Kikipatikana kiasi cha kutosha husimama kundi jengine kunyunyiza maji na kundi jingine la tatu linatengeneza tiyara ya hewa na maji yanayayuka kwa haraka; kwa myeyuko huo kiwango cha joto kinashuka.
Ni nani aliyempa nyuki akili hii? Ni sadfa? Au kuna nguvu ya hakika inayojitokeza kwenye maumbile na nidhamu yake? Nyuki na sisimizi wana masimulizi ambayo hayana tafsiri wala picha yoyote isipokuwa kuweko mpangiliaji mwenye hekima.
Turudie kauli ya Voltare ambaye huko nyuma tumewahi kumdokeza mara kwa mara, anasema: “Mbele ya fikra ya kuweko Mwenyezi Mungu kuna vikwazo lakini katika fikra ya kupinga kuna upumbavu …Namna hii binadamu anahama kutoka kwenye shaka hadi shaka nyingine mpaka anafikia kusadikisha kuwa kuweko Mwenyezi Mungu ndio jambo la karibu zaidi na kwaye zinafungamana kanuni za dharura ya ulimwengu.”
Wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa imepita kabla yao mifano.
Makusudio ya maovu hapa ni adhabu na mema ni thawabu na mifano ni mifano ya adhabu.
Mtume (s.a.w.) aliwalingania washirikina kwenye Tawhid, na akawaahidi thawabu wakiitikia mwito na kuwapa kiaga cha adhabu wakitoitikia.
Wao badala ya kuitikia mwito na kutubia shirk, waliendelea kuasi na wakajifanya jeuri, huku wakisema: Harakisha unayotuahidi ukiwa ni mkweli waliyasema haya bila ya kuzingatia umma zilizopita ziliyoyapata baada ya kuwaasi Mitume wao.
Kwa hakika mghafala huu wa kutopata funzo, hauhusiki na washirikina peke yao. Watu wengi hawazingatii yaliyowapata wenzao wala hawapati funzo; hata wenyewe wanaotoa mawaidha. Siri ya hilo ni kuwa wengi wanashindwa na tamaa na masilahi sio kwa akili wala dini.
Kuna mfano maarufu wa kimagharibi unaosema: Mwanamke kumwongoza mwana- mume kwa tumbo si kwa akili.
Na hakika Mola wako ni mwenye maghufira kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako ni mkali wa kuadhibu.
Makusudio ya maghufira hapa ni kupuuza na kutoharakisha adhabu kwa dhambi. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakika Mola wako ni mkali wa kuadhibu.” Kwa sababu maghufira hayawi pamoja na adhabu ya akhera sikwambii iliyo kali.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hamwadhibu mja mara tu anapo- fanya dhambi isipokuwa anamngojea na kumfungulia mlango wa toba ili aweze kurejea kutokana na upotevu wake, aweze kupata thawabu kwenye uwongofu wake.
Kuna tafsiri nyingine isemayo kuwa Mwenyezi Mungu husamehe dhambi za walioasi katika waislamu na anakuwa mkali wa kuadhibu kwa makafiri. Lakini tafsiri hii iko kinyume na dhahiri, tena inahimiza uasi. Usawa hasa ni yale tuliyoyasema kuongezea Aya nyingine isemayo:
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِمْ مَا تَرَكَ عَلَيْهَا مِنْ دَابَّةٍ{61}
Na husema wale ambao wamekufuru: ‘Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake?’ Hakika wewe ni mwonyaji tu. Na kila kaumu ina wa kuwaongoza.
Imepita mifano yake katika Juz.7 (6:37). Na tumefafanua kuhusu muujiza wa Mtume Muhammad (s.a.w.) na matakwa ya wenye kiburi katika Juz 1 (2:118).
اللَّهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنْثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ ۖ وَكُلُّ شَيْءٍ عِنْدَهُ بِمِقْدَارٍ {8}
عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ {9}
سَوَاءٌ مِنْكُمْ مَنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَنْ جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ {10}
لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِنْ بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنْفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُمْ مِنْ دُونِهِ مِنْ وَالٍ {11}