read

Aya 8-11: Mwenyezi Mungu Alijua

Maana:

Mwenyezi Mungu anajua mimba aibebayo kila mwanamke na kinachopungua na kuzidi matumboni.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya iliyotangulia ametaja kuwa washirikina walimtaka Muhammad (s.a.w.) muujiza zaidi unao fahamisha kuhusu utume wake.

Katika Aya hii anasema kuwa Yeye anajua kilicho katika matumbo ya uzazi awe ni mtoto wa kiume au wa kike mmoja au zaidi upungufu au ukamilifu. Basi mwenye kujua yote hayo, anajua kwamba kutaka muujiza zaidi ni inadi na kiburi tu, si kutaka kuongoka.

Wameafikiana Waislamu wote kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua viumbe vyote vikubwa kwa vidogo. Kwa sababu kila kiumbe kinajulikana mbele yake. Kwa ibara ya Muhyiddin bin Al-arabi:

“Hakika hakuna chochote kilichopo ulimwenguni ila kina wajihi maalum kwa yule aliyekifanya kiweko.”

Kisha wanafalsafa wakatofautiana na ulamaa wa elimu ya Mwenyezi Mungu ambao wanasema kuwa Mwenyezi Mungu anajua mafungu yote; kama vile aina ya wanyama, mimea na vitu vingine kwa ujuzi wa moja kwa moja bila ya kuweko kitu chochote kati yake. Wanafalsafa nao wanasema anajua kupitia sababu zake na kinachozalikana nacho.

Sisi hatuoni faida yoyote ya tofauti hii. Kwa sababu ni juu ya Mwislamu kuamini kuwa elimu ya Mwenyezi Mungu imeenea kwenye kila kitu, kiujumla na kimafungu; hata mapigo ya moyo na pepesi za akilini. Ama kuamini elimu yake kwa namna hii au ile si chochote katika dini.

Kuna hadithi zinazokataa kuifikiria dhati ya Mwenyezi Mungu na kuamuru kufikiria kuumba kwake na utengenezaji wake.
Na kila kitu kwake ni kwa kipimo haumbi kimchezomchezo na bila ya misingi; bali kila kitu kina kiwango chake na nidhamu yake katika kipimo cha mafungu, mihimili athari na mahusiano yake. Vile vile kinamna kitakavyokuwa na sura, mahali, wakati, sababu na desturi yake. Yote hayo ni kulingana hekima na masilaha.

Analoweza binadamu ni kuona, kuchunguza, kupima na kukisia. Kwa hivyo anaweza akapatia au kukosea. Kwa sababu elimu ya mtu inatokana na kutafuta, kwa hiyo inahitaji msababishaji.

Mara nyingi sana kuna yanayodhaniwa kuwa ni sababu ya jambo fulani, kumbe sivyo kabisa. Ama elimu Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ya kidhati na hali halisi.

Ni mjuzi wa ghaibu na yanayoshuhudiwa, Mkubwa aliyetukuka.

Makusudio ya ukubwa sio ukubwa wa umbo na utukufu sio mahali panapohisiwa, bali hayo ni mafumbo ya utukufu wa dhati Yake na sifa Zake. Mjuzi wa ghaibuu ni kujua yale tusiyoyajua, yaliyo ughaibuuni kutokana na elimu yetu na yanayoshuhudiwa ni yale tunayoyaona na kuyashuhudia.

Hakika ulimwengu umejaa viumbe jinsi na aina mbali mbali za hali ya juu na za chini. Kuanzia vidudu hadi binadamu na Malaika, madini hadi mimea na wanyama, mpaka kufikia maji na hewa na mengineyo yasiyokuwa na ukomo.

Mtume anaweza kujua upande moja tu wa baadhi ya vitu vya ulimwengu lakini ujuzi wake, kadiri utakavyokuwa si chochote kulinganisha na asiyoyajua. Mengi yanayofichuka yanaficha siri nyingi.

Wala hajui yaliyoko ulimwenguni isipokuwa muumba wa ulimwengu huo tu. Yeye peke yake ndiye ambaye, kwake, siri na dhahiri ni sawa tu.

وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا {85}

“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” (17:85)

Ni sawa anayeficha kauli kati yenu na anayeidhihirisha na anayejibanza usiku na anayetembea mchana.

Umepita mfano wake katika Juz. 7(6:3) na Juz.10 (9:78).

Ana yanayomfuatilia mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Anayefuatiliwa ni binadamu na yanayomfuatilia ni fumbo la hisia na silika zake ambazo zina athari katika kuwa kwake na kuhifadhi utu wake. Hayo yametokana na riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq (a.s.).

Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya yanayomfuatilia ni Malaika, na tafsiri nyingine zinasema kuwa Mwenyezi Mungu hupeleka Malaika kumi mchana kumlinda binadamu na jua linapozama wanaondoka hao na kuja wengine kumi wa zamu ya usiku; na kwamba kila mtu anakuwa hivyo. Iblisi naye zamu yake ya kuwapoteza watu ni mchana na usiku ni zamu ya watoto wake.

Mbali ya kuwa maelezo hayo yako mbali na tamko linavyofahamisha, lakini akili pia inayakataa. Tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ya yanayofuatilia ni hisia zinazomhifadhi mtu; kama tulivyotangulia kueleza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mtu, akampa masikio, macho, utambuzi na mengineyo, ili yamlinde na kumchunga.

Maana haya, ingawaje yako mbali na tamko la Aya, lakini yanaafikiana na hali halisi wala hayapingani na mfumo wa Aya. Ni kwa utambuzi, mtu ana mapambano kati ya manufaa na madhara, ni kwa macho anaweza kufuata njia iliyosalama na ni kwa kupenda dhati ndio atajihifadhi na maangamizi.

Habadilishi Mpaka Wajibadilishe

Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao.

Wafasiri wamesema: Aya hii inafahamisha kuwa watu wanaoishi katika neema ya mali, amani na jaha, Mwenyezi Mungu hawezi kuwaondolea madamu wanaswali na kutoa Zaka, lakini wakiasi basi anawaondolea neema hii.

Ama sisi tutafasiri Aya hii katika mwelekeo wa mafunzo ya kiislamu na maana yanayochukuliwa na tamko la Aya.

Katika mafunzo ya Uislamu, yaliyo muhimu ni wajibu wa jihadi ya nafsi ikiwa inapondokea kwenye haramu na maangamizi au kuridhia udhalili na ufukara. Vile vile jihadi ya nafsi na mali katika njia ya uadilifu na kujikomboa kutokana na dhulma na utumwa.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kupinga udhalili, akapuuza uhai na kukataa kila kitu isipokuwa heshima yake au mauti, basi Mwenyezi Mungu atamshika mkono kumpeleka kwenye matakwa na malengo anayoyakusudia.

Na mwenye kubweteka kwenye raha na uvivu, vyovyote itakavyokuwa Mwenyezi Mungu atamdhalilisha na kumwachia udhaifu wake wala hatamwangalia au kumsikiliza; hata kama ataijaza dunia kwa unyenyekevu, vilio, na dua.

Kwa hivyo basi inatufunukia kuwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “ Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao,” ni kuwa Yeye ambaye imetukuka heshima yake, atambakisha mtu kwenye udhalili ikiwa amekaa tu bila ya kujikwamua na kuipinga batili.

Ndio! Mwenyezi Mungu hawezi kutuondolea ufukara mpaka tuamini kuwa ufukara umetoka ardhini sio mbinguni, na mpaka tupigane jihadi dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji na mpaka tujenge viwanda na tulime mashamba.

Mwenyezi Mungu hatubadilishii ujinga mpaka tujenge mashule na vyuo vikuu. Mwenyezi Mungu hatubadilishii utumwa mpaka tulete mapinduzi dhidi ya dhulma. Na Mwenyezi Mungu hatatubadilishia matatizo mbalimbali mpaka tuzisafishe nyoyo zetu na tuondoe pingamizi na vikwazo vilivyo baina yetu.

Mwenyezi Mungu akiwatakia watu uovu hakuna cha kumzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.

Makusudio ya uovu hapa ni adhabu. Wakati wowote Mwenyezi Mungu anapomtakia mtu au kundi jambo lolote, basi hakuna wa kuzuwiya, na Yeye ni mwadilifu, hamtakii isipokuwa analostahiki. Ulinzi ni katika sifa za Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye analinda mambo na huyasimamia kwa mipangilio iliyo kamili.

هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنْشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ {12}

Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.

وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَنْ يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ {13}

Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu; na yeye ni mkali wa hila.

لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِنْ دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُمْ بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ ۚ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ {14}

Kwake ndio maombi ya haki. Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.

وَلِلَّهِ يَسْجُدُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُمْ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ۩ {15}

Na vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake na vivuli vyao asubuhi na jioni.