Aya 12-15: Anayewaonyesha Umeme
Maana
Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa na huyaleta mawingu mazito.
Umeme unaokusudiwa hapa ni ule wa radi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ulimengu; ulimwengu nao una mambo yake na desturi zenye athari; ukiwemo umeme radi mawingu, vimondo na mengineyo anayoweza kuyashuhudia mtaalamu na mtu wa kawaida na pia muumin na mlahidi. Wala hajui hakika yake na umbile lake isipokuwa wataalamu wahusika.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyategemeza kwake moja kwa moja, wala hakuyategemeza kwenye sababu za ulimwengu, kwa upande wa kutegemeza kitu kwenye sababu yake ya kwanza.
Lengo ni kukumbusha kwamba Yeye ndiye sababu ya sababu zote, na kwake Yeye pekee yanarejea mambo yote.
Kauli yake kwa hofu na tamaa ni kuashiria umeme, mara nyingine unakua ni kutoa onyo la kupiga radi ya kimondo na mara nyingine ni dalili njema ya mvua. Kwa hiyo mtu anapata hofu na furaha kwenye kitu hicho hicho kimoja.
Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia.
Makusudio ya kumtakasa (tasbih) ya radi ni kufahamisha uweza na cheo chake Mwenyezi Mungu; sawa na maandishi yanavyomfahamisha mwandishi na jengo na mjengaji wake.
Hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَإِنْ مِنْ شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ{44}
Yaani kinamfahamisha. Kwa maneno mengine kila kitendo kizuri kilichofanywa kwa mpangilio mzuri kinamfahamisha aliyekifanya jinsi alivyo na kumsifia, kwa lugha ya hali.
Hakuna mwenye shaka kwamba kila kilichomo ulimwenguni kimefanywa kwa mpangilio mzuri usio na kikomo. Kwa hivyo kinafahamisha jinsi alivyo muumba wake na kumsifia.
Kauli ya kushangaza ni ile ya baadhi ya masufi wanaosema kuwa radi ni kukoroma kwa Malaika na umeme ni mapigo ya nyoyo zao.
Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye.
Unaweza kuuliza mapigo ya radi mitetemeko ni mambo ya kidhahiri ya kimaumbile na desturi yake. Ni wazi kwamba maumbile ni pofu hayachagui baina ya mwema na muovu, shari yake na heri yake inawaenea wote bila kutofautisha, lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ‘yakampata amtakaye’ inatambulisha kutofautisha?
Jibu: Makusudio ya mapigo ya radi hapa ni adhabu ya radi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa wale waliong’ang’ania shirki wakawafanyia inadi Mitume wao; kama vile kaumu ya A’d na Thamud, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنْذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ {13}
فَقَالُوا أَرِنَا اللَّهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ بِظُلْمِهِمْ ۚ {153}
Imetangulia mara nyingi kuelezwa kwamba Qur’an inajitamkia yenyewe kwa yenyewe na baadhi yake ina shuhudia baadhi nyingine.
Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu.
Wanaobishana ni washirikina. Maana ni kuwa hawa wanabishana katika uweza wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake, Mtume Muhammad (s.a.w.) na Utume wake na pia ufufuo na uwezekano wake, pamoja na kudhihiri dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, Muujiza wazi wa Utume wa Muhammad (s.a.w.) na kushuka adhabu kwa wapinzani wa ufufuo na hisabu.
Na yeye ni mkali wa hila.
Yaani ni mwenye nguvu sana za kuwakamata maadui zake na maadui wa mawalii wake. Kwa ufupi ni kuwa washirikina wanabishana kwa maneno na Mwenyezi Mungu anakamata kwa vitendo.
إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ {12}
Kwake ndio maombi ya haki. Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.
Mwenyezi Mungu ndiye haki. Mwenye kutenda kwa ajili yake na akamtegemea yeye, basi atamlipa thawabu na mwenye kuasi na akafanya jeuri atastahiki adhabu; mwenye kuomba mwenginewe, kama masanamu ,atakuwa ameomba batili isiyodhuru wala kunufaisha.
Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotovu.
Sawa na mwenye kiu akidhani moshi ni mawingu na mangati kuwa ni maji. Ananyoosha viganja vyake ili avijaze maji na anafungua kinywa chake ili aburudike, mara hamna kitu.
Na vilivyomo mbingu ni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake.
Umepita mfano wake katika Juz.3(3:83).
Na vivuli vyao asubuhi na jioni.
Kivuli ni akisi ya mwili ambao unakuwa nacho, ukitingishika nacho hutingishika; sawa na sura ya kitu kwenye kioo. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja asubuhi na jioni, kwa sababu kivuli kinarefuka katika nyakati mbili hizi.
Maana ni kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini na pia vivuli vyao vinamsujudia. Unaweza kuuliza: Kivuli si chochote isipokuwa kinafuata na kinapigiwa mfano wa kutokuwepo kitu. Vipi Mwenyezi Mungu amejaalia ni kitu na akaunganisha na mwenye kivuli hicho?
Sufi wamejibu kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini ni viwiliwili na vivuli ni roho.
Tunavyofahamu ni kuwa kivuli ni fumbo la kuenea kwenye kila kitu na kwamba kila kilichoko ulimwenguni kinamsujudia Mwenyezi Mungu; yaani kinakubali kuweko kwake, hata kivuli kingelimsujudia kama kingelikuwa ni kitu.
قُلْ مَنْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُمْ مِنْ دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنْفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ {16}