read

Aya 16: Kipofu Na Mwenye Kuona

Maana

Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa kila kilichomo ulimwenguni kinanyenyekea uweza wake, anawarudia washirikina na kuwauliza kupitia mdomoni mwa Mtume wake Mtukufu, kuwa ni nani aliyeumba ulimwengu ikiwemo ardhi yake na mbingu yake?

Kwa kuwa swali liko pamoja na jawabu lake; na wala aliyeulizwa hawezi kupinga, alimwamrisha Mtume wake awajibu: Sema, ni Mwenyezi Mungu.

Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara?

Mara nyingine, tena kwa kusisitiza hoja, Mwenyezi Mungu anamwamrisha Muhammad awaambie washirikina kuwa nyinyi mnaabudu mawe ambayo yenyewe hayajiwezi kujikinga na madhara wala kuleta manufaaa, je yataweza kumfaa mwingine?

Aya hii si majibu ya washirikina pekee, bali pia ni majibu ya wale wasemao kuwa akili za watu zinajitosha, hazihitajii kupelekewa mitume na kuteremshwa vitabu kutoka mbinguni. Waabudu mawe walikuwa na wanaendelea kuwa wanajiona ni wenye akili na pia watu wangine wanawaona hivyo.

Sema: Je, anaweza kuwa sawa kipofu na aonaye?

Makusudio ya kipofu ni kafiri. Kwa sababu hakuweza kutofautisha baina ya yule asiyejiweza, na mwenye kumiliki dhara na manufaa? Makusudio ya mwenye kuona ni mumin ambaye anatofautisha kati ya wawili hao (asiyejiweza na mwenye uwezo).
Au je, huwa sawa giza na nuru?

Giza ni fumbo la kufuru na nuru ni fumbo la imani. Mwenyezi Mungu anasema:

الر ۚ كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ {1}

“Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru” (14:1).

Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika, walioumba kama kuumba kwake kwa hiyo kuumba kukashabihiana kwao?

Hii ni kuwarudi washirikina. Ufupisho wake ni kuwa mawe ambayo wanayaabudu hayaumbi chochote; kama aumbavyo Mwenyezi Mungu. Sasa wamethubutu vipi kusema kuwa Mungu anaumba na masanamu yanaumba.
Ikiwa Mwenyezi Mungu anastahiki Uumbaji, basi vile vile atastahiki Uungu na ibada. Ufafanuzi ni kama ifuatavyo:

Akili Za Watu Haziwatoshelezi

Maarifa ya mtu yanagawanyika kwenye mafungu mawili: Maarifa ya kiumbile ya kidhati na maarifa ya kinadharia ya kutafuta. Ya kimaumbile hayahitaji bidii wala juhudi, bali yanapatikana kiasi cha kuleta picha tu kichwani; kama kujua kwamba nuru sio giza, kuona si upofu, urefu sio ufupi, jiwe limeumbwa na haliwezi kuumba. Katika maarifa haya anashiri kimjuzi na asiyekuwa mjuzi, na mwenye kukosea hana udhuru wowote.1

Ama maarifa ya kinadharia ya kutafuta hayapatikani kwa kuleta picha, bali inahitajika kuyafanyia kazi, juhudi na bidii; kama vile kujua kuwa maji yameshikana au yameachana? Na kujua mardhi haya yanaambukiza au la.

Kadhia hii huitwa ‘nadharia’ ambayo inatofautiana kulingana na maarifa na vipawa vya wenye nadharia hizo. kukosea katika nadharia kunasame- hewa kukiwa kumetokea baada ya bidii na juhudi. Kwa sababu kupatia katika kila kitu ni jambo zito.

Masanamu waliyoyaabudu washirikina hayana mshabaha wowote na uungu kwa njia yoyote ile ya mbali au ya karibu, kuweza kumfanya mtu aingie shaka au aone uwezekano wa kuwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake.

Itakuwaje yakiwa hayo yenyewe yanakojolewa na mbwa na vicheche? Kuyaabudu ni upumbavu zaidi kuliko kusema kuwa giza ni nuru au kipofu anaona.

Unaweza kuuliza: Ni kweli kwamba kuna aina ya maarifa ambayo ni maumbile na kwamba kuukana uungu wa mawe ni mambo ya kimsingi yaliyo wazi yasiyohitaji nadharia, lakini washirikina pamoja na akili yao ya kimaumbile wameweza kuyaabudu, wakiwa ni wenye akili timamu. Je, ni kwa nini?

Jibu: Baadhi yao waliabudu kijujuu tu kwa sababu ya chumo na masilahi fulani, wengine waliabudu kwa kuiga na kurithi. Ilivyo ni kuwa akili inadhoofika na kurudi nyuma katika kuigiza au mazoweya, hasa muda ukiwa mrefu na kurithiwa na vizazi baada ya vizazi vingine.

Ndio maana ikawa dini iliyo salimika ni dharura na lazima kwa binadamu kadiri atakavyokuwa na akili na elimu. Kuna wengi sana waliozowea mifu- mo ya elimu na njia zake za undani, hivi sasa, wanaamini mambo mengi ya upotevu. Gustave Labon, anasema katika kitabu Al-arau wal-mutaqada ( Rai na itikadi).

“Hakika wataalamu wanatokewa na mambo ya kijinga sawa na wanavyotokewa wasiojua chochote. Ni mara chache sana mtaalamu kusalimika na ujinga katika mambo yasiyokuwa fani yake.

Kwa maelezo haya ndio tunapata sababu ya wataalamu bora zaidi kuaamini mambo ya kipumbavu sana!! Kisha akatoa mifano mingi sana ya hilo; miongoni mwa mifano hiyo ni: kulikuwa na mtaalamu mmoja mkubwa katika zama zake alikuwa hawezi kutoka nyumbani kwake mpaka afunge kamba shingoni ya kumkinga na dege na uchawi.

Sema: Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na yeye ni mmoja, Mwenye kushinda.

Ni mmoja katika dhati yake, sifa zake, na kuumba kwake. Mwenye kumshinda kila mwenye inadi na mwenye kuasi hukumu miongoni mwa hukumu zake.

Katika Juz.5 (4:48) Tumetaja dalili za umoja wa muumba. Hapa tutaunganisha na maelezo yaliyo katika Kitab Difau anil- Islam (kuutetea uislam) kilichoandikwa na Laura Fisheva Gallery na kutarjumiwa na Ustadh Munir Baalbaki.

Anasema: “Mtume mwarabu alitoa mwito wa itikadi ya umoja wa Mungu (Tawhid) akapata upinzani wa wasio na mtazamo ambao ulimuongoza mtu kwenye shirk. Muhammad alitoa mwito wa kusoma kitabu cha maisha na kufikiria kwenye ulimwengu na desturi yake akiwa anaamini kuwa kila mwenye akili hana budi mwisho kuamini Mungu mmoja.

أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَابِيًا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِثْلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ ۚ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنْفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ {17}

Ameteremsha maji kutoka mbinguni na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake na mvo ukachukua mapovu yaliyokusanyika juu yake. Na katika vile wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine hutokea povu mfano wake. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano wa haki na batili. Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano.

لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُمْ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمِهَادُ {18}

Waliomwitikia Mola wao watapata wema na wasiomwitikia, hata wange-likuwa na vilivyomo ardhini vyote na mfano wake, hakika wangelivitoa kujikombolea. Hao wana hisabu mbaya kabisa na makao yao ni Jahannam, na hapo ni mahali pabaya mno.
  • 1. Baadhi wametofautisha baina ya elimu na maarifa, kwamba elimu inafunga- mana na mambo yote ya kijumla na maarifa yanafungamana na mafungu fulani. Lakini sisi hatuoni tofauti yoyote kati yake. Mwenyezi (s.w.t.) anasema: "Kila kabila ikajua mahali pake pa kunywea." Juz.1 (2:60). Ametumia neno elimu - ikajua, na wawala hakusema ikapata maarifa. Na inajulikana kuwa kunywa kwa kila kabila kulikua mahsus sio kiujumla.