read

Aya 17-18: Povu Halidumu

Maana

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amefananisha baina ya mumin na kafir, akapiga mifano miwili: Kwanza, baina ya kipofu na mwenye kuona - kumfananisha kafiri na upofu na mumin na kuona. Pili, baina ya giza na nuru - kumfananisha kafiri na giza na mumin na nuru.

Katika Aya tuliyo nayo hivi sasa, amefananisha haki na batili akaleta mifano miwili vile vile: Kwanza, baina ya maji yanayokaa ardhini na kuwapatia watu heri na uhai. Pili, mapovu ambayo yanashuka kwenye maji kisha yanachukuliwa na mumbu na kwenda na upepo. Amefananisha haki na maji yenye kunufaisha, na batili akifananisha na mapovu yasiyokaa. Haya ndiyo aliyoyakusudia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliposema:

Ameteremsha maji kutoka mbinguni na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake na mvo ukachukua mapovu yaliyokusanyika juu yake.
Makusudio ya kadiri yake ni kwamba kila bonde linachukua maji ya mvua kwa kiasi chake cha upana na kina yanayozidi yanaminika kwengine.

Ama mfano mwingine wa haki na batili alioufananisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni madini yanayoyeyushwa motoni ili yatengenezwe vipambo kama dhahabu na fedha au vifaa kama chuma risasi na shaba na povu linazimika kwenye madini yaliyoyeshwa ambayo yanapotea; kama yanavy- opotea mapovu yanayochukuliwa na mvo. Kwa hiyo haki ni kama myeyuko wa madini ulio na manufaa na batili ni povu linalotokana na myeyuko ambalo halina manufaa. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake:

Na katika vile wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine hutokea povu mfano wake.

Yaani kwenye madini pia hutokea povu lisilokuwa na manufaa sawa na povu la mvo.

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano wa haki na batili.

Yaani Mwenyezi Mungu analeta mfano na picha ya haki kwa ubainifu kati- ka picha ya maji na madini ambayo hupatiwa manufaa na batili katika picha ya povu lisilokuwa na manufaa.

Ama povu ambalo linachukuliwa na mvo au kuzimika kwenye madini yanapoyeyeshwa linakwenda bure bila ya manufaa.

Ama kinachowafaa watu kukaa kwenye ardhi nayo ni maji na madini hukaa ardhini kwa ajili ya heri na uhai

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano ya haki na batili na mingineyo.

Mara nyingi maana yanakuwa magumu kufahamika na watu wengi. Mifano ni nyenzo nzuri ya kufafanua na kuweka wazi, mbali ya kuwa mfano unaongezea uzuri wa ubainifu.

Mwenyezi Mungu amepiga mifano mingi katika Aya nyingi za ubainifu; kama vile ukafiri na imani kuupigia mfano wa giza na nuru au upofu na uoni. Vile vile mfano wa haki, katika Aya hii, kwa maji na madini, na wa batili kuwa povu.

Aya hii inaleta picha halisi ya Uislamu. Au kwa ufasaha zaidi, inaleta picha ya Mwislamu wa kweli, kuwa ni yule ambye watu wananufaika naye kwa manufaa yenye kudumu; sawa na yule aliyeihuisha ardhi baada ya kufa; na kama madini magumu yanayojengewa viwanda na viwanda vinazalisha zana na vifaa mbali mbali na kuleta maendeleo, vya mbali vikaletwa karibu. Kukawa na majeshi, wakatembea angani, ardhi ikalimwa na dunia ikajaa heri, amani na raha.

Natija ya hayo ni kwamba kila mwenye kunufaisha, akaleta utengeneo na katenda kwa ajili ya maisha ya binadamu mwenzake awe na uhuru, amani na raha, hakika mtu huyo atakuwa kwenye malengo ya Uislam, hata kama si Mwislamu. Kwa sababu yeye ni sawa na madini aliyoyatolea mfano wa haki Mwenyezi Mungu. Na kwamba kila mwenye kutenda kwa ajili ya uovu wa mtu. Yeye hana uislamu kitu, hata kama atafunga maisha na kuunganisha swala za usiku na alfajiri.

Waliomwitikia Mola wao watapata wema.

Yaani watapata wema kwa sababu ya kumwitikia Mola wao kwenye mwito wa kutenda kwa ajili ya manufaa ya watu na kwa ajili ya maisha bora. Ama makusudio ya wema ni ujira na thawabu na kwamba watu wa haki watanufaisha, kama maji yanavyonufaisha ardhi.

Na wasiomwitikia - nao ni wale wasiokuwa na maana, kama mapovu- hata wangelikuwa na vilivyomo ardhini vyote na mfano wake, hakika wangelivitoa kujikombolea. Hao wana hisabu mbaya kabisa na makao yao ni Jahannam, na hapo ni mahali pabaya mno.

Umetangulia mfano wake katika Juz.3 (3:91) na Juz.11(10:54).

أَفَمَنْ يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ {19}

Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wako ni haki, ni sawa na aliye kipofu? Wanaozingatia ni wenye akili tu.

الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّهِ وَلَا يَنْقُضُونَ الْمِيثَاقَ {20}

Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu wala hawavunji maagano.

وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّهُ بِهِ أَنْ يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ {21}

Na wale ambao huyaunga aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe na humwogopa Mola wao na huihofu hisabu mbaya.

وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنْفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ {22}

Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao na wakasimamisha Swala na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika vile tulivyowaruzuku na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakaopata malipo ya nyumba.

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَنْ صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِمْ مِنْ كُلِّ بَابٍ {23}

Nayo ni Bustani (Pepo) za Milele wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao wake zao na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia kila mlango.

سَلَامٌ عَلَيْكُمْ بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ {24}

(wakisema): Assalaam alaykum kwa sababu ya mlivyosubiri. Basi ni mema mno malipo ya nyumba.

وَالَّذِينَ يَنْقُضُونَ عَهْدَ اللَّهِ مِنْ بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّهُ بِهِ أَنْ يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۙ أُولَٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ {25}

Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuifunga na wanakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe na wanafanya ufisadi katika nchi. Hao ndio walio na laana na wana nyumba mbaya.