Aya 19-25: Yaliyoteremshwa Kutoka Kwa Mola Wako Ni Haki
Maana
Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wako ni haki, ni sawa na aliye kipofu? wanaozingatia ni wenye akili tu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kufananisha ukafiri na upofu, tena akafananisha haki kwa maji na batili kwa povu, sasa anafananisha mwenye kumwamini Muhammad na kuona na mwenye kumkana kwa upofu.
Mwenyezi Mungu ameeleza uhakika huu kwa njia ya swali ili kumsuta na kumtahayariza.
Wanaozingatia ni wenye akili tu wanasikiliza sauti kwa akili na yule asiyetia akilini isipokuwa yanayoafiki hawaa yake, ni sawa na asiye na akili.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja sifa za wenye akili ambazo zinafahamisha makusudio ya wenye akili kuwa ni waumini wenye takua; kama ifuatavyo:
1. Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu.
Kila lililo na dalili basi hilo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu na ni juu ya binadamu kutekeleza, lakini maibilisi wanapotosha uhakika kwa mapenzi yao kisha wananasibisha hawa zao hizi za kishetani kwa Mwenyezi Mungu na haki. Mwenyezi Mungu ametakata na yale wanayomzushia.
Wala hawavunji maagano. Hii ni kutilia mkazo kauli yake ‘wanatimiza’ ambapo wanalazimiana na utekelezaji ahadi bila ya kuvunja.
2. Na wale ambao huyaunga aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe.
Wafasiri wametaja kauli kadhaa katika kufasiri aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe. Kauli iliyo karibu zaidi ya roho ya Uislamu na misingi yake, ni ile ya yule aliyesema: Makusudio ya aliyoamrisha yaungwe, ni msaada wa mtu kwa nduguye mtu, kusaidiana naye kuondoa madhara na kuleta manufaa kwa karibu au mbali.
3. Na humwogopa Mola wao na huihofu hisabu mbaya kimatendo sio kinadharia na kimaneno. Imam Ali anasema: “Mambo mema yanafahami- ka kwa imani na imani inafahamika kwa mambo mema.”
4. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao. Wanapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanavumilia majeraha na maumivu; hawataki malipo wala shukrani isipokuwa radhi ya Mwenyezi Mungu peke yake.
5. Na wakasimamisha Swala ambayo mwanzo wake ni Takbira ihram: Mungu ni mkubwa zaidi (Allahu akbar) hakuna mkubwa zaidi yake vyovyote atakavyo kuwa. Na Mwisho wake swala ni Tahlil na Salaam: Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu (lailalaha illallah) Hakuna anayeabudiwa isipokuwa Yeye; hakuna mali wala jaha au hisabu zinazoweza kuabudiwa wala hakuna nguvu inayonyenyekewa isipokuwa nguvu yake Mwenyezi Mungu pekee yake bila ya kuwa na mshirika.
6. Na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika vile tulivyowaruzuku. Mali ndiyo ugomvi. Angalia tulivyoielezea katika mwanzo wa Juz.4 (3:92).
7. Na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakaopata malipo ya nyumba.
Makusudio ya wema hapa ni msamaha na uovu ni haki maalum inayokuwa baina ya wawili; kama kisasi. Mwenyezi Mungu anasema: “Mmeandikiwa kisasi katika waliouawa; muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa mtumwa na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ni kufuatana kwa wema na kulipa kwa ihsani.” Juz.2 (2:178)
Ama haki ya Mwenyezi Haina kusameheana,
وَلَا تَأْخُذْكُمْ بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ {2}
Nayo ni Bustani (Pepo) za Milele wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao wake zao na vizazi vyao.
Wema wote wataingia peponi. Iwapo duniani walikuwa na udugu na upenzi basi furaha itazidi kwa kuunganishwa tena na kukumbuka enzi zao walipokuwa duniani. Iwapo matendo yao yatatofautiana, basi udugu na urafiki utakatika siku hiyo:
فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ {7}
Na Malaika wanawaingilia kila mlango (wakisema): Assalaam alaykum kwa sababu ya mlivyosubiri. Basi ni mema mno malipo ya nyumba.
Maana ya Assalaamu alykum! Ni: Amani iwe juu yenu. Kauli yake Mwenyezi Mungu kwa sababu ya mlivyosubiri, inaashiria kwamba Pepo ni haramu isipokuwa kwa mwenye kufanya jihadi akasubiri, akavumilia tabu na mashaka ya jihadi, Imam Ali (a.s.) anasema: “Pepo imezungukwa na machukivu na moto umezungukwa na matamanio. Na jueni kuwa hakuna yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu ila hujiwa na machukivu. Na hakuna yeyote aliyemwasi Mwenyezi mungu ila hujiwa na matamanio.”
Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuifunga.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwataja wema na sifa zao na malipo mema aliyowaandalia, sasa anawataja wafisadi. Kwa ibara ya kuunganisha ni kuwa baada ya kutaja wanamapinduzi dhidi ya ufisadi anataja wapinzani wao.
Ni kawaida makundi mawili hayo kupingana. Watenda mema hutekeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wakatenda kulingana na akili na dhamiri na kila linalofahamishwa na dalili. Wafisadi wanavunja ahadi yake Mwenyezi Mungu na hutenda kulingana na mawazo ya kishetani wakiichanganya haki na batili na wakiificha haki na hali wanajua
Na wanakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe.
Wanawatawalisha mataghuti wakosaji na kuwasaidia kuwakandamiza watu wema kinyume na aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na kuyakataza.
Na wanafanya ufisadi katika nchi kwa kuidhihirisha dhulma na kuleta fitina vurugu, kuwapoteza wasio na hatia, kuleta utengano, kuleta maangamizi na kila aina ya ufisadi na upotevu.
Hao ndio walio na laana na wana nyumba mbaya.
Ikiwa matendo yao ni kinyume cha watendao mema, basi vile vile ni kawaida malipo yao yawe tofauti. Wema watapata pepo na nyumba yenye neema na waovu watapata Jahannam na mahali pabaya.
اللَّهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا مَتَاعٌ {26}
وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِنْ رَبِّهِ ۗ قُلْ إِنَّ اللَّهَ يُضِلُّ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ {27}
الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُمْ بِذِكْرِ اللَّهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ {28}
الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ {29}