read

Aya 30-31: Tumekutuma Katika Umma

Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao zimekwishapita kabla yao umma nyingine, ili uwasomee tunayokupa wahyi na wao wamemkufuru Mwingi wa rehema.

Maneno yanelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Mwenyezi Mungu amepeleka mitume kabla yao kwenye umma zilizopita kwa lengo hilo hilo, sasa basi kuna kioja gani? Wao si watu wa kwanza kupelekewa mtume na yeye si mtume wa kwanza kuwasomea watu wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Sema, Yeye ni Mola wangu hakuna Mola mwengine isipokuwa yeye. Juu yake nimetegemea na kwake yeye ndio marejeo yangu.

Hii ndio imani ya Muhammad (s.a.w.) na huu ndio mwito wake, Anamwamini Mwenyezi Mungu peke yake na anamwelekea Yeye kwenye mamabo yake wala haoni mwenye uwezo mwingine zaidi yake. Anawalingania watu kwenye imani hii. Ni mwito ambao unajifahamisha wenyewe.

Fikra Ya Mataghuti

Na lau kwamba Qur’an ndiyo inayoendeshewa milima au kupasuliwa ardhi au kusemeshewa wafu (wasingeliamini) Bali amri zote ni za Mwenyezi Mungu.

Umepita mafano wa Aya hii mwanzo wa Juz. 8, na tumefafanua huko kwa anuani ya ‘Aina ya watu.’ Pia utakuja mfano wake katika Juz. 15. (17:90).

Tukiunganisha tuliyoyatanguliza ni kwamba Aya hii inaleta picha ya njia wanayoifikiria mataghuti ambao maisha yao yanasimama kwa kuwany- onya wanyonge na kuwafanya watumwa wao. Si maumbile wala akili, hisia, yanayoshuhudiwa, miujiza au chochote kile kitakachoweza kubadilisha ukaidi wa mataghuti na ulafi wao. Dawa pekee ni kuwaondoa na kuondoa misingi yao ya uporaji na unyang’anyi. PamojanayotehayoMuhammadanawatakawamkubaliyeyenaQura’n.

Lakini wapi? Ni mpaka majabali yaendeshwe na Qur’an? Au mpaka wasemeshwe wafu? Kisha ndio iweje! Watapata faida gani katika hayo? Au kumuona Mungu ana kwa ana kutaongeza faida kwenye mali zao?

Hii ndio fikra yao na hii ndiyo lugha wanayoifahamu na kuisikiliza; wala hawasikilizi lugha nyingine isiyokuwa hiyo – lugha ya uchumi na faida ya paundi na dola. Lakini haki, uadilifu, mantiki na akili ni mazungumzo ya kipumbavu, yanayosadikiwa na watoto na wajinga.

Je, baada ya hayo, mtu anaweza kuuliza kwanini mataghuti hawakumwamini Muhammad pamoja na wito wake wa uadilifu na wema?

Mwito huu unaotaka kung’oa mizizi ya dhulma na ufisadi wanauona ni kosa kubwa. Hii ndio fikra pekee wanyoifikiria wale wanaoishi kwa uny- onyaji na unyang’anyi. Alikuwa nayo fikra hii Abu Jahl na Abu Sufyan wakati wa Muhammad (s.a.w.), katika zama zetu wamekuwa nayo Hitler na Musolini na leo hii fikra hii iko kwenye dola za kiukandamizaji zikion- gozwa na Marekani.

Dalili wazi ya hilo ni Marekani. Leo inaushinikiza Umoja wa Mataifa, kwa nguvu zake zote, ijitie hamnazo kwa sula lolote la usawa na uadilifu, ikishindwa inajitokeza waziwazi kupiga vita kila taifa litakalotaka haki na uadilifu na kuisaida dhulma na utaghuti popote ulipo; ni sawa uje kwa njia ya Israil au Ureno au hata kwa serkali ya kibaguzi ya Rhodesia1 na Afrika kusini au kwengineko.
Siri ya yote hayo ni kuifagilia Marekani, kama kiongozi wa ukoloni. Lakini mwisho wa ubabe huu utakuwa kama wa Hitler. Dalili zimejionyesha wazi katika Vietnam. Ama masononeko yanayosababishwa na siyasa ya ukoloni yameena mashariki na magharibi, na masononeko haya hayatapita bure bila ya kuacha athari.

Mwanzo nilikuwa nikistaajbu kutokana na baadhi ya watu jinsi wanavyowadharau watu wema wenye ikhlasi na wasiwaheshimu, tena wanawaona ni kama watu wa kawaida; hata kama wakifanya maajabu gani na wakajitolea mhanga kuithibitisha haki!

Niliendelea kushangaa hivyo mpaka nilipofikia kufasiri Aya hii tuliyo nayo nikagundua kuwa fikra hii haiko kwa mataghuti na wafisadi tu; isipokuwa watu wengi wameondoa akilini ubora na msimamo na kuupima kwa chumo na faida tu; sawa na wale waliompiga vita Muhammad na waliosimama upande wa Israil katika Umoja wa mataifa na Baraza la usalama; isipokuwa tofauti yao hawa ni kuwa waliifuata njia ya ufisadi na utaghuti, lakini waliposhindwa basi wakabakia kwenye upinzani.

Je, hawajajua wale ambao wameamini kwamba lau Mwenyezi Mungu angelipenda bila shaka angeliwaongoa watu wote.

Neno hawajajua limefasiriwa kutoka neno Yay’as. Tabari anasema: “wametofautiana wafasiri kuhusu neno ‘yay’as… Usawa hasa ni kubainikiwa na wamenukuu tafsiri hii wengi akiwemo Imam Ali (a.s.) . Na sisi ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa watu wa nyumba ndio wanojua zaidi kilichomo humo nyumbani.”

Vyovyote iwavyo ni kuwa makusudio ya wale ambao wameamini ni maswahaba wa Mtume (s.a.w.) pale walipotamaani kuwa washirikina wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ndipo Mwenyezi Mungu aliyetukuka akwaambia, mpaka lini mtakuwa na tamaa ya kuamini washirikina?

Je, hajajua na kubainikiwa kuwa wao kivyovyote hawataamini hata kama wafu watazungumza nao au majabali yatembee. Achaneni nao na utaghuti wao! Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwaingiza kwenye imani angelifanya, lakini hekima yake Mtukufu imepitisha kumwachia mtu na hiyari yake ili kuweza kumpa uhuru na ubinadamu wake.

Lau angelimnyang’anya uhuru huu na hiyari, basi asingelikuwa ni chochote, na wala asingelistahiki kusifiwa au kushutumiwa wala thawabu au adhabu. Angalia tafsir yetu Juz. 12 (11: 118).

Wala wale ambao wamekufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyoyatenda au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao mpaka iwafikie ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya wale ambao wamekufuru ni wale waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.). Maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hawachi duniani hawa waliokadhibisha bila ya kuwatia adabu; bali anawateremshia balaa kila baada ya muda.

Hayo ni kwa sababu ya msimamo wao kwa Muhammad (s.a.w.). Au anawateremshia balaa karibu yao iwatie hofu na fazaa nyoyoni mwao. Analifuatilia hilo Mwenyezi Mungu mpaka itimie ahadi yake ya ushindi kwa Mtume wake.

Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi.

Vipi avunje miadi naye ndie mkweli zaidi wa ahadi. Maswahaba na kila mumin ana imani kuwa Mwenyezi Mungu atatekeleza ahadi na atalinusuru jeshi lake tu.

وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِنْ قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ {32}

Na hakika walifanyiwa stihizai Mitume waliokuwa kabla yako, lakini nikawapa muda wale ambao wamekufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu!

أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا لِلَّهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَمْ بِظَاهِرٍ مِنَ الْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ ۗ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ {33}

Je anayesimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi? Au ni maneno matupu? Bali wale ambao wamekufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumuongoza.

لَهُمْ عَذَابٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَقُّ ۖ وَمَا لَهُمْ مِنَ اللَّهِ مِنْ وَاقٍ {34}

Wanayo adhabu katika maisha ya dunia. Na hakika adhabu ya Akhera ina mashaka zaidi. Na wala hawana wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.
  • 1. Nchi hiyo hivi sasa inaitwa Zimbabwe.-Mtarjumu