read

Aya 32-34: Mitume Walifanyiwa Stihzai

Maana

Na hakika walifanyiwa stihizai Mitume waliokuwa kabla yako, lakini nikawapa muda wale ambao wamekufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu!

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwambia Mtume wake, vumilia na uendele na mwito wako na achana nao wale wanokukejeli na jiweke mbali na maoni yao kwako. Walikwishafanya waliokuwa kabla yako, nikawaacha kisha nikawaadhibu adhabu isiyowezekana. Huu kwa hakika ndio mwisho wa wakadhibishaji.

Mwenyezi Mungu hakumtuma mtume ila anampa mambo mawili: Ujuzi wa dalili za kilimwengu na za kiakili juu ya kuweko Muumba na umoja wake. Na muujiza unaojitokeza mikononi mwake utakaojulisha utume wake. Jambo hilo la kwanza ni kwa ajili ya kuwakinahisha watu na Tawhidi (umoja wa Mungu) na la pili ni kwa jili ya kuwakinaisha watu kuwa yeye ni mtume wa Mwenyezi Mungu.

Wale wasioamini isipokuwa manufaa yao na chumo lao tu walikuwa wakiwakejeli Mitume na kuwafanyia maskhara pamoja na dalili zao na miujiza yao. Mwenyezi Mungu naye huwapa muda ili warudi kwenye uongofu na awaonye kwa kuwapa muda, kama alivyowaonya kwa hoja.

Je anayesimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma.

Anaichunga nafsi na kuilinda na kudhibiti kila kitu, kisha kuilipa thawabu ikifanya mema na adhabu ikifanya uovu. Mwenye sifa zote hizi anafanywa kuwa wenzake ni mawe? Na wawemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Mwenyezi Mungu anasema:

أَفَمَنْ يَخْلُقُ كَمَنْ لَا يَخْلُقُ ۗ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ {17}

“Ati anayeumba ni kama asiyeumba? Basi hivi hamkumbuki?” (16:17).

Sema watajeni.

Yaani enyi washirikina tajeni angalau sifa moja tu inayostahiki kuabudiwa masanamu yenu. Hii ni dharau na dhihaka, sawa na mwoga kusema: Mimi ni shujaa, kisha aambiwe: tutajie ushahidi mmoja wa ushujaa wako.

Au ndio mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi?

Mwenyezi Mungu anasema hana mshirika na nyinyi manasema ana washirika wengi. Maana yake ni kuwa wao wanajua zaidi na Mwenyezi Mungu hajui.
Ametakaka Mwenyezi Mungu na hayo kabisa; kama wase- mavyo watu wa mantiki: kikipatikana chenye kulazimiwa ndio umepatikana ulazima na kikikosekana chenye kulazimiwa ndio umekosekana ulazima – likipatikana jua ndio umeptikana mchana na likikosekana jua ndio umekosekana mchana na ukikosekana mchana ndio hakuna jua.

Kwa hiyo ikiwa kuna mshrika, kwa vyovyote Mwenyezi Mungu atamjua. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hamjui mshirika huyo basi hayupo; vinginevyo Mungu atakuwa halijui hilo, jambo ambalo haliwezekani.

Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja ardhi pamoja nakuwa Yeye hana mshirika ardhini na mbinguni, kwa vile mazungumzo yanahusiana na masanamu yaliyoko ardhini.

Au ni maneno matupu.

Hilo ni tamko la kufahamisha maana ya kupatikana. Maneno yoyote yasiyofahamisha kitu halisi basi ni maneno matupu. Na neno washirika hapa ni majina yasiyokuwa na wenyewe:

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ بِهَا مِنْ سُلْطَانٍ ۚ {23}

“Hayo hayakuwa ila ni majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote” (53:23).

Umepita mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:710 ) na katika Juz. 12 (12:40).

Bali wale ambao wamekufuru wamepambiwa vitimbi vyao.

Maana ya vitimbi ni hadaa. Washirikina walihadaliwa na masanamu, wakayadhania ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake na wakajipambia wenyewe hadaa hii.

Na wamezuiliwa njia kwa kuchukulia lisilojulikana.

Yaani lile walilojipambia limewazuilia wao na haki na imani ya Mwenyezi Mungu na umoja wake.

Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumuongoza. Tazama Juz. 5 (4:88).

Wanayo adhabu katika maisha ya dunia kwa kupata hizaya na utwevu.

Na hakika adhabu ya Akhera ina mashaka zaidi, kwa sababu kila kitu duniani kusikiwa kwake ni kukubwa kuliko kuonekana kwake na kila kitu katika Akhera kuonekana kwake ni kukubwa kuliko kusikiwa kwake; kama asemavyo Imam Ali (a.s.).

Na wala hawana wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu naadhabuyake.

مَثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى الَّذِينَ اتَّقَوْا ۖ وَعُقْبَى الْكَافِرِينَ النَّارُ {35}

Mfano wa Bustani (Pepo) waliyoahidiwa wenye takua inapita mito chini yake, matunda yake ni ya daima na pia kivuli chake. Hiyo ndio mwisho wa wale wenye takua. Na mwisho wa makafiri ni moto.

وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَفْرَحُونَ بِمَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ ۖ وَمِنَ الْأَحْزَابِ مَنْ يُنْكِرُ بَعْضَهُ ۚ قُلْ إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّهَ وَلَا أُشْرِكَ بِهِ ۚ إِلَيْهِ أَدْعُو وَإِلَيْهِ مَآبِ {36}

Na wale ambao tumewapa Kitabu wanafurahia uliyoteremshiwa. Na katika makundi mengine wapo wanayoyakataa baadhi yake. Sema: Nimeamrishwa nimwabudu Mwenyezi Mungu wala nisimshirikishe. Ninalingania kwake Yeye, na marejeo ni kwake.

وَكَذَٰلِكَ أَنْزَلْنَاهُ حُكْمًا عَرَبِيًّا ۚ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُمْ بَعْدَمَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا وَاقٍ {37}

Na ndio kama hivyo tumeiteremsha Qur’an kuwa ni hukumu kwa Kiarabu. Na kama ukifuata hawaa zao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na msimamizi wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِنْ قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَنْ يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ ۗ لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ {38}

Na hakika tulikwishawatumma mitume kabla yako na tukawajalia wawe na wake na kizazi. Na haiwi kwa Mtume kuleta muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila muda una kitabu.