read

Aya 35-38: Mfano Wa Bustani

Mfano wa Bustani (Pepo) waliyoahidiwa wenye takua inapita mito chini yake, matunda yake ni ya daima na pia kivuli chake.

Mwenyezi Mungu alipomaliza kutaja malipo ya makafiri, sasa anataja malipo za wenye takua, kama kawaida yake ya kutaja kitu na kinyume chake. Malipo ya wenye takua ni Bustani (Pepo) pamoja na nema yake ya kudumu – mito, matunda na vivuli.

Hiyo ndio mwisho wa wale wenye takua.

Hiyo ni ishara ya Pepo. Wenye kumcha Mungu ni wale wanoilinda haki na watu wake na kupambana na batili na watu wake. Kuna Hadith isemayo : “Hakika imani iko juu ya Uislamu na kumcha Mungu kuko juu ya Imani na yakini iko juu ya kumcha Mungu” Makusudio ya yakini ni kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye.

Na mwisho wa makafiri ni moto.

Makusudio ya makafiri hapa sio tu wale wanaomkana Mwenyezi Mungu au kumshirikisha; isipokuwa makusudio ni kila anayeipinga haki, huku akiwa anajua. Zimeleza Hadith nyingi kuwa unafiki ni ukafiri n ria ni shirk. Mwenyezi Mungu amewasifu na ukafiri madhalimu, aliposema:

فَأَبَى الظَّالِمُونَ إِلَّا كُفُورًا {99}

“Lakini madhalimu hawataki ila ukafiri” (17:99);

kama ambavyo amewasifu makafiri na washirikiana kwa dhulma katika Aya kadhaa.

Shia Imamiya Na Swahaba

Wamezowea baadhi ya wanaolipwa walio wajinga kuleta fitna na ghasia baina ya Waislamu ili kuuchafua umoja wao na kuwagombanisha. Wamezoya sana hilo kwa njia ya kutia doa na kuleta uzushi kwa Shia kwa kuwazulia kuwatukana maswahaba; kumfanya Mungu Ali, kuwa Qur’an imepotolewa, jambo ambalo linaitingisha Arsh, na mengineyo miongoni mwa uwongo na uzushi.

Nimeandika makala ndefu katika kuwajibu vibaraka na wafanya propaganda hizi. Kisha nikayaweka kwenye vitabu: Mashia al-imamiyya, Ashia wal-hakimun, Al-ithnaashariya wa Ahlulbayt, na Ashia wat tashayyu’ ambacho ni kikubwa kuliko vyote.

Lengo langu la kwanza la makala na tungo hizi ni kuuweka wazi uhakika kwa yule anayetaka kuujua na kuubatilisha uongo na uzushi uliosemwa na unaosemwa juu ya taifa hili.

Hapa nimedokeza niliyoyaandika na kuyatunga kuhusiana na maudhui haya kwa mnasaba wa Aya hii tuliyo nayo, kama ifuatavyo:

Na wale ambao tumewapa Kitabu wanafurahia uliyotermshiwa.

Amesema Abu Hayan Al-andalusi, Zamakhshari, Sheikh Al-maraghi, Al-baydhawi na wengineo katika maulama wa kisunni kuwa makusudio ya wale ambao wamepewa Kitabu ni Myahudi na Manaswara wale waliomwamini Muhammad (s.a.w.).

Na akasema Tabrasiy, katika Tafsir Majmau’lbayan, ninamnukuu: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakusudia maswahaba wa mtume (s.a.w.) ambao walimwamini na kumsadikisha, wakapewa Qur’an na kuifurahia kushuka kwake” Tabrasiy ni miongoni mwa maulama wakubwa wa kishia (alikufa mwaka 548 AH).

Kwa hiyo basi wanchuoni wengi wa kisunni wamefasiri Aya hii kuwa ni waliosilimu katika Mayahudi na manaswara; na wa kishia wamefasiri kuwa ni Mswahaba wa Mtume mtukufu (s.a.w.). Ikiwa wao wanawatukana maswahaba angelielekea Sheikh wao Tabrasiy, katika kufasiri Aya hii kwenye njia ya maswahaba. Hapa unatubainikia uzushi uliowekwa kwenye kundi hili.

Aban bin Taghlab ni mmoja katika wanafunzi wakubwa wa Imam Jafar As- Sadiq (a.s.), kiasi ambacho Imam alikuwa akiwaamuru Shia kuchukua dini kutoka kwake. Siku moja aliulizwa na mtu mmoja anayeitwa Abul-bilad kuhusu Shia, akamwambia: ni wale ambao wakitofautiana watu kuhusu riwaya iliyopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.) basi huchukua riwaya ya Ali aliyoipokea kutoka kwa Mtume na wanapotofautiana watu katika riwaya ya Ali huchukua kauli ya Jafar As-Sadiq aliyoipokea kutoka kwa Ali.

Kwa hiyo basi, kwa Shia, kadhia ni mategemezi ya riwaya kutoka kwa Muhammad (s.a.w.) sio kadhia ya kutukana na kushutumu maswahaba wa Muhammad. Siri ya mategemezi yao Shia kwa Ahlu bayt (watu wa nyum- ba ya Mtume) ni Hadith kadhaa zilizothibiti, zinazohimiza hilo. Miongoni mwazo ni ile allyoipokea Muslim katika Sahihi yake kutoka kwa Mtume, kwenye mlango wa Fadhail Ali bin Abi Twalib (Ubora wa Ali bin Abi Twalib), kwamba mtume amesema:

“Mimi ni mtu, mjumbe wa Mwenyezi Mungu anakurubia kunijia nimwitikie; nami ninacha kwenu vizito viwili, cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu ndani yake mna uongofu na nuru, basi kichukueni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na shikamaneni nacho”

Akahimiza kuhusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukipen- dekeza, kisha akasema: “Na Ahl bayt yangu (watu wa nyumba yangu) ninawakumbusha kwa Mwenyezi Mungu kuhusu Ahl bayt wangu. Alilikariri hilo mara tatu.”

Na katika makundi mengine wapo wanayoyakataa baadhi yake.

Makusudio ya makundi mengine ni watu wa mila na dini nyingine; kama vile mayahudi, manaswara na wengineo wanaoyakataa yale yanayokhalifiana na mapenzi yao na wakayakubali yanayoafikiana na mapenzi yao katika Qur’an.

Ilivyo ni kuwa kupinga kwao hawa na kukubali kwao ni sawa tu, kwa sababu kukubali ni kwa kuafikiana na hawaa zao sio kwa sababu ya Qur’an.

Sema: Nimeamrishwa nimwabudu Mwenyezi Mungu wala nisimshirikishe. Ninalingania kwake Yeye, na marejeo ni kwake.

Huu ndio Uislamu: Hakuna Mola mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu ni wake ufalme na mwito wa kuabudiwa ni kwake Yeye tu, na mwisho marejeo ni kwake yeye.

Na ndio kama hivyo tumeiteremsha Qur’an kuwa ni hukumu kwa Kiarabu.

Makusudio ya hukumu ni Qur’an, kwa sababu ndio hukumu ya Mwenyezi Mungu, isiyokuwa hiyo ni hukumu ya kijahili; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّهِ حُكْمًا لِقَوْمٍ يُوقِنُونَ {50}

“Je wanataka hukumu za Kijahiliya. Na ni nani aliye mwema zaidi kwa hukumu kuliko Mwenyezi Mungu, kwa watu wenye yakini.” Juz. 6 (5:50).

Kama ambavyo Mwenyezi Mungu, alimtuma kila mtume kwa lugha ya watu wake, vilevile alimtuma Muhammad. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ رَسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ {4}

“Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia (14:4)

Tumefafanua sababu za kushuka Qur’an kwa kiarabu, pamoja na kuwa Muhammad ametumwa kwa watu wote, katika Juz. 12 (12:2).

Na kama ukifuata hawaa zao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na msimamizi wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Wanaokusudiwa katika neno hawaa zao ni watu wa mila nyingine isiyokuwa Uislamu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa Nabii hafuati wala hatafuata hawaa na matamanio yao. Lengo la ukatazo huu ni uthabiti na kuendelea kuilingania haki, wala asiogope lawama ya mwenye kulaumu. Tumeelza mara kwa mara kuwa amri ikitoka kwa mkubwa hakiangaliwi cheo cha mdogo vyovyote kilivyo

Na hakika tulikwishawatuma mitume kabla yako na tukawajalia wawe na wake na kizazi.

Asiye na haki akishindwa huanza kuzungusha maneno na kupima mambo kwa mawazo na njozi zake. Na hivyo hasa ndivyo ilivyokuwa kwa washirikina na Muhammad (s.a.w.). Aliwaletea hoja na dalili, wali- poshindwa kuzijibu wakanza kusema: itakuwaje ni nabii naye ana mke na watoto.

Mantiki hii inafanana kabisa na mantiki ya wanaoamini utawa. Mwenyezi Mungu amewajibu kwa kuwambia kuwa Muhammad ni kama Nuh, Ibrahim, Ismail na wengineo katika mitume ambao wana wake na watoto, sasa kuna ajabu gani katika hilo?

Kuna hadith iliyopokewa kutoka kwa mtume, amesema: ”Ama mimi ninafunga, ninafungua, ninalala, ninaamka, ninakula nyama na ninaoa. Mwenye kujiepusha na desturi yangu basi yeye si katika mimi”

Na haiwi kwa Mtume kuleta muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Haya vilevile ni majibu kwa washirikina ambao walimpendekezea mtume miujiza ile waitakayo. Njia ya majibu ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu swt) amemsheheneza mtume wake kwa dalili zinazotosheleza kujulisha juu ya utume wake, kwa yule mwenye kuzingatia na kuitafuta haki kwa njia ya haki. Ama kuitikia mapenzi ya mwenye inadi na kiburi hakukubaliwi na akili wala desturi. Anaachiwa Mwenyezi Mungu na hekima yake.

Kila muda una kitabu.

Yaani kila kitu kina muda wake, kiwe ni muujiza, adhabu, au chochote kile. Na muda umeandikwa hautangulizwi wala kucheleweshwa nao umefichwa, haujui isipokuwa Mwenyezi Mungu.

يَمْحُو اللَّهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِنْدَهُ أُمُّ الْكِتَابِ {39}

Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo na kwake kuna mama wa Kitab.

وَإِنْ مَا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ {40}

Na ikiwa tutakuonyesha baadhi ya tuliyowaahidi au tukakufisha, basi ni juu yako kufikisha na juu yetu ni hisabu.

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنْقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَاللَّهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ {41}

Je hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza janibu zake. Na Mwenyezi Mungu huhukumu, hapana wa kupinga hukumu yake; na Yeye ni mwepesi wa kuhisabu.

وَقَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ فَلِلَّهِ الْمَكْرُ جَمِيعًا ۖ يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ ۗ وَسَيَعْلَمُ الْكُفَّارُ لِمَنْ عُقْبَى الدَّارِ {42}

Na wamekwisha fanya vitimbi waliokuwa kabla yao na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye vitimbi vyote. Anajua inayoyachumma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho.

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَسْتَ مُرْسَلًا ۚ قُلْ كَفَىٰ بِاللَّهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِنْدَهُ عِلْمُ الْكِتَابِ {43}

Na wale ambao wamekufuru wanasema wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi na yule mwenye elimu ya Kitabu.