Aya 39-43: Mwenyezi Mungu Hufuta Na Huthibitisha Ayatakayo
Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo na kwake kuna mama wa Kitab.
Mama wa kitabu ni fumbo la ujuzi wake Mwenyezi Mungu wa yaliyokuwa na yatakayokuwa.
Lau ingekuwa inafaa kufasiri matamshi kwa muonjo na kupendeza, basi tungelifasiri kitabu ni ulimwengu na mama ni siri zake; kwa sababu Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: kimoja kinatamka kwa lugha ya hali nacho ni ulimwengu na kingine kinatamka kwa lugha ya maneno nacho ni Qur’an.
Ama kufuta na kuthibitisha, Tabrasi amenukuu katika maana yake kauli nane, iliyokaribu zaidi na maana ni kuwa makusudio ya kufuta ni kufuta sharia za zamani au kufuta baadhi ya hukumu zake; kama vile kufuta hukumu ya kuelekea Baytil-maqds. Ama kuthibitisha, makusudio yake ni kuthibitisha hukumu mpaka siku ya Kiyama.
Kwa hiyo maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anafuta au kuthibitisha sharia zote au baadhi, vile masilahi na hekima yake inavyotaka. Na Yeye ambaye umetukuka utufu wake anajua yaliyo na maslahi kwa waja na yaliyo na uharibifu. Kwa hiyo anawamrisha hili na kuwakataza lile, daima au kwa muda, kulingana na vile elimu yake inavyojua muda wa madhara na manufaa. Tumezungumzia kuhusu kufuta hukumu katika Juz.1 (2:106).
Na ikiwa tutakuonyesha baadhi ya tuliyowaahidi au tukakufisha, basi ni juu yako kufikisha na juu yetu ni hisabu.
Aya hii ianungana na Aya 31 ya Sura hii. Njia ya kuungana ni dhahiri: Kule amemwambia mtume wake kuwa Yeye kwa vyovyote atamteremshia adhabu yule anayemkadhibisha; hapa anasema kama tutakuonyesha adhabu yao au tutakufisha kabla ya hiyo adhabu, basi umuhimu wako wa kwanza na wa mwisho ni kufikisha tu, mengine tuachie sisi.
Je hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza janibu zake.
Ardhi ni tufe, lisilokuwa na ncha, lakini ni pana linaloweza kukaliwa na mamilioni ya aina mbali mbali ya viumbe. Nayo hubadilika daima. Binadamu anaweza kuona au kusikia kuwa ardhi hii ni nzuri kukaliwa na watu itakuwa na maendeleo na ardhi ile haifai ni njangwa. Mara ile iliyoonekana inafaa inakuwa haifai na ile iliyokuwa jangwa isiyofaa inakuwa bustani yenye mito.
Watu wa ardhi pia ni hivyo hivyo, maendeleo yanakuwa hai na mengine yanakufa; ufalme unasimama na mwingine unaanguka.
Hivi ndivyo ilivyo dunia ‘kigeugeu.’ Hakuna ubaya wala neema inayoweza kudumu hapa ardhini. Imam Ali (a.s.) anasema: “Tahadharini na dunia ina ghururi na inahadaa, inatoa na kuzuia, inavika na kuvua. Haidumu raha yake wala tabu yake haiishi.” Kauli yake Mwenyezi Mungu: Tukiipunguza janibu zake, inaashiria maana hii na kwamba mwenye akili anapata funzo kwa mageuko haya:
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۗ {109}
Na Mwenyezi Mungu huhukumu, hapana wa kupinga hukumu yake.
Na amekwisha hukumu kuwaangamiza wenye makosa na amekwishaipitisha hukumu hiyo.
Na wamekwisha fanya vitimbi waliokuwa kabla yao na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye vitimbi vyote.
Makusudio ya vitimbi vya Mwenyezi Mungu ni kupangua vitimbi. Angalia Juz.3 (3:53).
Anajua inayoyachuma kila nafsi. Kwa sababu yeye ni mwenye wasaa aliye mjuzi.
Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho. Siku ile watakaporudi kwa Mola wao na kusema leo ni siku nzito.
Na wale ambao wamekufuru wanasema wewe hukutumwa.
Waliukana utume wa Muhammad pamoja na dalili zote, kwa vile huo ni vita dhidi ya dhulma na utaghuti na jambo lolote linalozuia uhuru wa mtu, amani yake na wema wake
Raha Ya Dhamiri Na Mawazo
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi na yule mwenye elimu ya Kitabu.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anamwamrisha mtume wake awaambie: ikiwa mnakanusha utume wangu, basi Mwenyezi Mungu anshuhudia kuwa mimi ni mtume kutoka kwake, vile vile wenye kuchunga haki katika maulama wa Tawrat na Injil wanashuhudia hilo.
Haya ndio maana ya dhahiri na ndio makusudio yake na ndiyo waliyoeleza wafasiri na sisi tuko pamoja nao, lakini zaidi ya hiyo tunagusia maana kubwa zaidi inayofungamana na kila mwenye kuiamini haki akaitumia na akapingwa na wenye kufanya ufisadi katika ardhi na yakampata yaliyowapata.
Muhtasari wa maana haya makubwa na matukufu ambayo yanaashiriwa na Aya ni kuwa kila ambaye dhamiri yake inalionea raha jambo na kushuhudi- wa na mawazo yaliyo salama, basi Mwenyezi Mungu, Malaika wake na wenye kuchunga haki pia wanalishuhudia kuwa ni haki, awe ni Mtume au sio Mtume. Unaweza kuuliza: Ni wakati gani mtu anakuwa na raha ya dhamiri na kushuhudiwa na mawazo salama?
Jibu: Hakika binadamu hawezi kuwa ni katika mwenye dhamiri hai na mawazo salama ila ikiwa anaamini msimamo wa kibinadamu; kama vile uadilifu, uhuru, ukweli, uaminifu na mengineyo ambayo heri yake inawarudia wote. Pale tu, mtu atakapoamini msimamo huu na ukaoana na vitendo vyake, basi atakuwa amestarehe dhamiri, na kushudiwa na mawazo yake.
Na wakati wowote, vitendo vyake na imani yake vitakapotengana, atakuwa ameitia utumwani dhamiri yake na itamsuta yeye mwenyewe.
Watu wa dhamiri na mawazo hawatilii umuhimu isipokuwa misimamo yao mbele ya dhamiri zao na mbele ya watu wema mfano wao ambao wanashirikiana nao kwa kuonyesha mfano na msimamo wa kibinadamu.
Lakini msimamo wao unakuwa hauna thamani mbele ya asiyekuwa na dhamiri ambaye haoni isipokuwa nafsi yake na masilahi yake tu.
Mimi nina yakini kwamba watu wema zaidi ni wale wenye misimsmo ya haki ambao hawajui starehe yoyote isipokuwa ile inayotuliza dhamiri zao.
Unaweza kuuliza kuwa watu wengi wanaona raha wanapo pata yale wanayoyataka, ingawaje wao hawamini misingi wala misimamo yoyote; je, hiyo si inamaana wema na raha ni kupata mtu atakacho na ubaya ni kukosa atakacho?
Jibu, kwanza, mazungumzo yetu tangu mwanzo ni juu ya watu wenye dhamiri, na hawa unaowasema hawana dhamiri yoyote.
Pili, watu wengi wanaojionyesha kuwa wanapinga misimamo, huwa kiundani, wanaikubali ndani ya nafsi yao; lakini uovu ulipowashinda walijaribu kuficha kwa kukana yale wanayoyaamini, huku wakijidanganya kwa kusema:
Lau kungelikuwa na msimamo wowote tungelilazimiana nao; sawa na mwenye makosa kukana makosa yake, huku anajua kuwa yeye ni mwenye hatia.