read

Aya 1-4: Dini Ni Nuru

Maana

Alif Laam Raa

Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:1).

Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru, kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye nguvu Mwenye kusifiwa.

Makusudo ya Kitabu hapa ni Qur’an. Msemo wa tumekuteremshia unaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Na makusudio ya idhini ni amri.

Aya inafahamisha kwa uwazi kuwa lengo la msingi la kutumwa Muhammad (s.a.w.) na kuteremshwa Qura’n ni kuziweka pamoja nguvu zote za watu na kuwa na mshikamano kwa ajili ya ubinadamu na heri yake na utulivu wake. Kwa sababu kuwatoa watu kwenye giza hakuwezi kukamilika kwa miito na Swala; isipokuwa ni kwa juhudi za pamoja, sio za mtu pekee, dhidi ya ukandamizaji, ujinga, ufisadi na uigizaji wa kipumbavu.

Na kweli Muhammad aliunganisha udugu baina ya maswahaba zake, na akawaingiza roho ya kusafiana nia, mahaba na kujitolea na akawafanya miongoni mwao - wakiwa ni washamba na wajinga-wajumbe wa heri wenye kuelimika na maendeleo.

Kwa mnasaba huu tunagundua kuwa wale matapeli wanaohimiza upotofu kwa kuupa jina la dini, kuwa ni maadui wakubwa wa Mwenyezi Mungu na mtume wake. Kwa sabu dini ni nuru na upotofu ni giza, dini ni njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kusifiwa na giza ni njia ya shetani mwenye kulaaniwa. Unaweza kuuliza, kuna Aya isemayo:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33)

Dahiri ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma Muhammad kwa lengo la kuwa dini yake iwe juu ya dini zote. Sasa kuna wajihi gani wa kuunganisha baina ya Aya hizi mbili (kushinda dini na kutoa gizani).

Jibu: kwanza, makusudio ya dini katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘ili ipate kushinda dini zote,’ ni ushirikina. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake: ijapokuwa washirikina wamechukia.

Pili, kwamba dini zote katika zama za Muhammad zilikuwa ni giza, hata zile dini za mbinguni zilikuwa zimechezewa na mikono ya wapotofu.

Tatu, Kuwa juu dini ya Muhammad ndio kuwa juu haki ambayo, siku zote iko juu wala haikaliwi. Vyovyote iwavyo ni kwamba misingi yoyote wanayonufaika nayo watu kwa namna yoyote ile, inakutana katika upande huu na dini ya Mwenyezi Mungu na mwito wa Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini

Kauli hii imekaririka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu mara kumi. Na lengo ni kukumbusha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu na ni mtawala wa vilivyo humo.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anataja malipo ya makafiri na sifa zao:

1. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali.

Hiki ni kiaga cha Mwenyezi Mungu kwa makafiri kutokana na ukafiri wao, kwamba malipo yao ni maangamizi na adhabu. Razi anasema: “Hakika amewahusu kwa ole wao, kwa sababu watakuwa katika adhabu kali wakisema ole wetu.”

2. Wale ambao wamestahabu maisha ya dunia kuliko Akhera.

Huu ndio wasifu wa kwanza wa makafiri; kwamba wao wameathirika na batili kuliko haki, dhulma kuliko uadilifu na ufisadi kuliko wema. Kila anayekuwa hivyo basi yeye ni kafiri au anakutanishwa na makafiri katika vitendo vyake, naye anastahiki laana na adhabu, kama wanavyostahiki makafiri; ajapo swali, akufunga na akahiji.

3. Na wakawazulia watu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Wanawazulia watu na njia ya haki na uongofu, wakawa kwa hilo ni wenye kupotea na wenye kupoteza, wafisadi na wenye kufisidisha.

4. Na wanataka kuipotosha, hao wamepotelea mbali.

Neno upotofu linaashiria kuwa wao wanafikia malengo yao kwa njia kombokombo na za haramu; kama vile uwongo, utapeli, njama na kusaidiana na mataghuti. Wasifu huu hauhusiki na washirikina na makafiri peke yao; kwani Waislamu wengi wanasema uwongo, wanafanya hiyana na kupanga njama pamoja na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa wananchi dhidi ya viumbe wa Mwenyezi Mungu na nyenzo zao. Hawa ni wapotevu zaidi na waliopotea njia.

Makusudio ya upotevu uliombali, ni kuwa wao wamezama kwenye upote- vu mpaka wakafikia mwisho wake.

Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia waweze kumfahamu na litimie lengo la risala yake.

Lau kungelikuwa na Lugha inayoweza kufahamika na watu wote, basi angelitumwa nayo Muhammad (s.a.w.), kwa sababu yeye ni Mtume wa watu wote sehemu zote na wakati wote.

Hata hivyo ni lazima ifahamike kuwa kuna tofauti baina ya kusema Tumemtuma kwa lugha ya watu na kusema Tumemtuma kwa watu wa lugha yake. Tamko la kwanza halizuiwii kuwa mjumbe wa wote na tamko la pili linahusika na watu wake tu. Angalia Juz. 12 (12:2).

Mwenyezi Mungu aliwatuma wajumbe wake kwa waja wake ili awaokoe kutokana na ujinga na upotevu. Basi mwenye kuwasikiliza na akatii, ameongoka na mwenye kuachana nao akaasi basi ni mpotevu. Kwa hiyo uon- gofu unapimwa kwa kumtii Mwenyezi Mungu na upotevu kwa kumwasi.

Na lau kama Mwenyezi Mungu hakuweka sharia wala kuwatuma mitume basi kusingelikuwa na twaa na maasi wala uongofu na upotevu. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ameweka sharia akatuma mitume. Kwa hiyo natija ya hayo ni twaa na maasi, uongovu na upotevu.

Kwa kuzingatia hivi ndipo ikafaa kunasibisha upotevu na uongofu kwake Yeye Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka utukufu wake Angalia Juz.1 (2:26) na Juz. 5 (4:88).

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا أَنْ أَخْرِجْ قَوْمَكَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَذَكِّرْهُمْ بِأَيَّامِ اللَّهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ {5}

Hakika tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu kuwa watoe watu wako kutoka gizani kwenda kwenye nuru. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ أَنْجَاكُمْ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ وَيُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ ۚ وَفِي ذَٰلِكُمْ بَلَاءٌ مِنْ رَبِّكُمْ عَظِيمٌ {6}

Na Musa alipowaambia watu wake: “Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, alipowaokoa na watu wa Firauni walipowapa adhabu mbaya na wakiwachinja watoto wenu wa kiume na wakiacha hai watoto wenu wa kike. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa kutoka kwa Mola wenu.”

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِنْ شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ {7}

Na alipotangaza Mola wenu: Mkishukuru nitawazidishia na mkikufuru basi adhabu yangu ni kali.

وَقَالَ مُوسَىٰ إِنْ تَكْفُرُوا أَنْتُمْ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ {8}

Na alisema Musa: mkikufuru nyinyi na waliomo duniani wote, hakika Mwenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.