Aya 9-12: Je Hazikuwafikia Habari
Maana
Je haziukuwafikia habari za walio kabla yenu: Kaumu ya Nuh na A’d na Thamud na walio baada yao? Hakuna awajuaye illa Mwenyezi Mungu.
Mfumo wa maneno unaonyesha kuwa haya ni maneno kutoka kwa Nabii Musa (a.s.) kwenda kwa wana wa Israil, sio kutoka kwa Muhammad (s.a.w.) kwenda kwa washirikina wa kiarabu au wengineo, kama ilivyosemekana.
Maana ni kuwa Nabii Musa anawaambia Waisrail kuwapa mawaidha na kuwahadharisha kuwa mumesikia tufani ya Nuh na majanga yaliyowapitia watu wa A’d na Thamud na mengineyo zaidi ya hayo ambayo hajui idadi yake isipokuwa Mwenyezi Mungu? Aliwafanyia hayo Mwenyezi Mungu kwa sababu wao waliasi Mitume na wakafanya ukaidi. Je, hamzingatii na kupata mawaidha kwa umma zilizotangulia? Musa aliwaambia haya na zaidi watu wake, lakini Israil ni ileile ya mwanzo na ya mwisho.
Waliwajia mitume wao kwa hoja zilizo wazi.
Kila mtume anayetoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa waja wake hana budi kuwa amepewa hoja mkataa zinazofahamisha utume wake; kama vile balozi anavyoleta makaratasi ya kumjulisha kutoka kwenye serikali yake iliyomchagua kuwa balozi wake. Kwa hiyo basi inafahamisha kuwa makusudio ya hoja zilizowazi ni miujiza inayofahamisha juu ya unabii na utume wao.
Wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao.
Waliorudisha ni watu wa Nuh na waliokuwa baada yao. Kurudisha mikono vinywani mwao ni fumbo la kukataa sana; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
خَلَوْا عَضُّوا عَلَيْكُمُ الْأَنَامِلَ مِنَ الْغَيْظِ ۚ {119}
Na wakasema: “Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyotumwa na hakika sisi tuna shaka kubwa ya mnayotuitia.”
Washirikina walitia shaka au walidhihirisha shaka katika ukweli wa mitume wao na hapo mwanzo walikuwa wakiwakubali kuwa ni wakweli na wenye ikhlasi. Kwanini? Si kwa lolote ila ni kuwa manabii waliwataka walazimiane na haki na uadilifu na kuacha dhulma na batili. Haya hasa ndio mantiki ya wale wanaoangalia masilahi yao tu; leo wanayakana yale waliyoyakubali jana na kinyume chake. Siri ya hilo inakuwa katika faida na chumo; wao wako pamoja nayo popote ilipo na itakapokuwa.
Mitume wao wakasema: “Je kuna shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi?
Ni ajabu ya maajabu kutia shaka mahali pa imani na kuamini mahali pa shaka. Walimpinga Muumba wao wakaamini mawe, yanayokojolewa na mambwa, na kuyaabudu.
Anawaita ili apate kuwaghufiria dhambi zenu.
Mwenyezi Mungu ametukuka! Angalia ukarimu wake na upole wake, anawaita waja wake kwenye msamaha wake na rehema yake na anawatakia yale yanayowanufaisha.
Na anawapa muhula mpaka muda uliowekwa, wala hana haraka ya kuwaadhibu, bali anawapa muda ili warejee kwenye uongofu.
Wakasema: “Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi.
Kauli hii inafahamisha fikra yao kwamba watu wa kawaida hawafai kushika uongozi wa juu, hata kama watakuwa na ikhlasi, ukweli, na kujitolea kwa kiwango cha juu.
Mnataka kutuzuwia na waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu.
Kwa hiyo baba zao ni watukufu zaidi ya Mwenyezi Mungu na kufuata kwao upotevu ni haki zaidi ya twaa ya Mwenyezi Mungu; hata kama baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawaongoki.
Basi tuleteeni hoja iliyo wazi.”
Mitume waliwajia na hoja wazi na muujiza unaofahamisha kuhusu ukweli, lakini washirikina walitaka miujiza maalum ambayo Mwenyezi Mungu aliashiria kwa kusema:
لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ كَنْزٌ أَوْ جَاءَ مَعَهُ مَلَكٌ ۚ {12}
وَقَالُوا لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنْبُوعًا {90}
wao wanataka miujiza, lakini kupitia tumboni sio akilini.
Mitume wao wakawaambia: “Sisi si chochote ila ni wanadamu kama nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu humneemesha amatakaye katika waja wake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima na kwa vile yeye ni mwenye hekima na mjuzi, basi hamneemeshi kwa risala yake ila yule aliye kufu nayo mwenye sifa za kuichukua na kutekeleza:
اللَّهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ۗ {124}
Wala sisi hatuwezi kuwaletea dalili isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.
Angalia katika Juzuu hii (13: 38), Juz.7 (6:37) na Juz.1 (2:118).
Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu na hali yeye ametuongoa kwenye njia yetu na hakika sisi tutavumlia mnayotuudhi; na kwa Mwenyezi Mungu nawategemee wenye kutegemea.”
Tunayafupiliza maana, ingawaje yako wazi, kuwa Mitume waliwaambia washirikina: sisi tunafikisha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na tunamlingania Yeye; hatujali yule atakayekataa wala maudhi yatakayotupata katika njia hii. Kwa sababu sisi tunamtegemea Mola wetu na ubainifu wa jambo letu. Swali hili la: ‘Tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu.’ linafahamisha kwamba mitume hawaoni kitu isipokuwa Mwenyezi Mungu.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِرُسُلِهِمْ لَنُخْرِجَنَّكُمْ مِنْ أَرْضِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا ۖ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ رَبُّهُمْ لَنُهْلِكَنَّ الظَّالِمِينَ {13}
وَلَنُسْكِنَنَّكُمُ الْأَرْضَ مِنْ بَعْدِهِمْ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَافَ مَقَامِي وَخَافَ وَعِيدِ {14}
وَاسْتَفْتَحُوا وَخَابَ كُلُّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ {15}
مِنْ وَرَائِهِ جَهَنَّمُ وَيُسْقَىٰ مِنْ مَاءٍ صَدِيدٍ {16}
يَتَجَرَّعُهُ وَلَا يَكَادُ يُسِيغُهُ وَيَأْتِيهِ الْمَوْتُ مِنْ كُلِّ مَكَانٍ وَمَا هُوَ بِمَيِّتٍ ۖ وَمِنْ وَرَائِهِ عَذَابٌ غَلِيظٌ {17}