Aya 13-17: Tutakutoa Kwenye Ardhi Yetu
Na wale ambao wamekufuru waliwaambia mitume wao: “Tutawatoa katika ardhi yetu au mrudi kwenye mila yetu.”
Mitume walitoa mwito wa haki kwa hekima na mawaidha mazuri, wala hawakumlazimisha yeyote kwenye dini na itikadi yao, kwa sabau mwito wao umesimama kwenye misingi ya kutolazimisha kwenye dini; ingawaje hali halisi ni kuwa mwito wao ni mapinduzi kwa maadui na wakandamizaji.
Ndio maana nao wakatangaza vita dhidi yao; wakawapa mambo mawili: wartadi au wawafukuze.
Umetangulia mfano wa Aya hii mwanzoni mwa Juz.9 (7:88).
Mola wao akawapa wahyi: Hakika tutawangamiza madhalimu nanyi tutawakalisha katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anayeogopa kusimamishwa mbele yangu na akaogopa kiaga changu.
Baada ya washirikina kufikia kuwatisha mitume, yakaja matakwa yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuwamaliza mataghuti na kuwarithisha waumini ardhi, majumba na mali zao.
وَأَوْرَثَكُمْ أَرْضَهُمْ وَدِيَارَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ {27}
Haki Mbadala
Itakuwa ni vizuri, kudokeza, kutokana na mnasaba huu, mambo Mawili:
Kwanza; kwamba yeye Mwenyezi Mungu, aliyemtukufu na kutuka baada ya kutaja majigambo ya wafisadi na madhalimu na kuendelea kwao kwenye upotevu, amesema kuwa mwisho wa hawa ni maangamizi, ikiwa ni natija ya uovu na upotevu wao na kwamba mwisho wa wenye takua ni ushindi na kumakinika ardhini.
Huu ndio mfumo wa Qur’an, kutaja sababu na kisababishi chake na natija pamoja na chanzo chake. Mfumo huu una faida zake; kama vile kuhimiza haki na kuikemea shari na batili. Pia kujua mtu mwisho mzuri na ushindi wa haki; hata kama watu wa batili wataishikilia kwa nguvu, wakajinaki na muda ukawa mrefu.
Wameitumia njia hii mahatibu wengi na waandishi; wanataja uovu wa mtu kisha wanafuatishia, wakiwa na uhakika kabisa, kwamba shari inamrudia mwenye kuifanya.1
Jambo la pili; kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwa matakwa yake, anaingilia kuinusuru haki kwa masharti ya kutoicha haki, kuitilia shaka au kuridhia haki mbadala na kutaka haki chache na kuridhia batili nyingi.
Majaribio yameonyesha kuwa haki mbadala haina faida isipokuwa kwa wafisadi katika ardhi na kwamba hiyo daima iko kwenye maslahi ya wabatilifu; kwa sababu aina yoyote ya kuipunguza haki ni faida kwa wanyang’anyi na ni hasara kwa haki na watu wake. Hapo ndio inakuwa siri ya Imam Ali (a.s.) kutokuwa laini katika haki na kukataa kwake haki mabadala kwa aina zake zote.
Na wakaomba ushindi na akashindwa kila jabari mkaidi ambaye nyuma yake iko jahannam atanyweshwa maji ya usaha uliochanganyika na damu.
Usaha uliochanganyika na damu ni fumbo la ugumu wa kunywa na kumeza, kutokana na harufu mbaya na uchafu wake au uchungu na ukali wake au yote.
Imesemekana kuwa waliotaka ushindi ni mitume, ikasemekana kuwa ni washirikina na pia imesemekana ni wote. Maana yote yanafaa, kwa sababu mwisho ulikuwa, kama inavyotakiwa kuwa, ni ushindi wa haki na udhalili wa makafiri. Zaidi ya hayo mitume walitaka nusura kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
قَالَ رَبِّ انْصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ {30}
Washirikina, siku ya Bdri, walisema: “Ewe Mola lipe ushindi jeshi lililo juu zaidi.” Mwenyezi Mungu akawajibu:
إِنْ تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ ۖ وَإِنْ تَنْتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَكُمْ ۖ {19}
Atayagugumia wala hataweza kuyameza, kutokana na ukirihi, uchafu, ukali, na uchungu wake.
Na yatamfikia mauti kutoka kila mahali.
Yaani sababu za mauti zitamzunguka pande zote sita: Kushotoni, kuumeni, nyuma na mbele, juu na chini yake.
Na wala yeye si maiti.
Lau angelikufa angelistarehe na kukatikikiwa na adhabu na Mwenyezi Mungu anataka awe nayo:
وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُمْ مِنْ عَذَابِهَا ۚ {36}
Na nyuma yake kuna adhabu kali.
Miongoni mwa yaliyosemekana katika tafsiri ya ukali hapa ni kuwa adhabu itakuwa inaanza upya kila baada ya kipindi fulani, na kila hali inakuwa mbaya zaidi ya ile iliyotangulia “Ewe Mola msamehe anayekuamini wewe na pepo yako na moto wako wala hajibari na maasi yako, lakini ana matumaini ya rehema yako.”
مَثَلُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ۖ أَعْمَالُهُمْ كَرَمَادٍ اشْتَدَّتْ بِهِ الرِّيحُ فِي يَوْمٍ عَاصِفٍ ۖ لَا يَقْدِرُونَ مِمَّا كَسَبُوا عَلَىٰ شَيْءٍ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ {18}
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۚ إِنْ يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍ جَدِيدٍ {19}
وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ بِعَزِيزٍ {20}
وَبَرَزُوا لِلَّهِ جَمِيعًا فَقَالَ الضُّعَفَاءُ لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًا فَهَلْ أَنْتُمْ مُغْنُونَ عَنَّا مِنْ عَذَابِ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ ۚ قَالُوا لَوْ هَدَانَا اللَّهُ لَهَدَيْنَاكُمْ ۖ سَوَاءٌ عَلَيْنَا أَجَزِعْنَا أَمْ صَبَرْنَا مَا لَنَا مِنْ مَحِيصٍ {21}
- 1. Hata filamu nyingi huwa zinaonyesha mwisho mbaya wa waovu na maharamia- Mtarjumu