Aya 24-27: Neno Jema Na Neno Ovu
Maana
Je, hukuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri, kama mti mzuri.
Imesemekana kuwa maana ya neno zuri hapa ni tamko la Tawhidi: La ilaa-ha illa llah ‘Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.’ Hapana mwenye shaka kuwa Tawhid ndio msingi wa haki na chimbuko lake.
Ni kutokana na Tawhid na ikhlasi ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio tunaweza kulifasiri neno zuri kwa kila neno linalowanufaisha watu na kuwapatia kheri na utengeneo kwa namna moja au nyingine; ni sawa liwe ni neno la dini au sharia, elimu au falsafa na hata fasihi na fani. Mtu yeyote ambaye watu watanufaika na kauli yake au kitendo chake atakuwa, kwa upande huu, anakutana na misingi ya Uislamu na dini, kwa namana yoyote atakavyokuwa.
Kauli na neno bora zaidi ni neno la mapinduzi na kelele za hasira mbele ya mtawala jeuri na wale wanaomsaidia, miongoni mwa vibaraka na wanoji- weka nyuma. Kwa sababu wao ndio asili ya ugonjwa na chimbuko la balaa.
Amesema Imam Ali (a.s.): “Haikuwa kazi yoyote nzuri na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu katika kuamrisha mema na kukataza mabaya ila ni kama upumuo katika lindi la bahari na kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu hakukurubiwi na ajali wala hakupungukiwi na riziki na bora yake kabisa ni tamko la usawa mbele ya kiongozi jeuri.”
Kwa sababu kiongozi huyo ndio chimbuko la kila uovu. Kwa hiyo mwenye kumkabili na akampinga atakuwa ameupiga vita uovu wote.
Kuna Hadith kadha za Mtume Mtukufu (s.a.w.) zenye maana ya kauli hii ya Imam Ali. Kila kitokacho kwa Ali Amirul-muminin ni miali ya jua la Muhammad bwana wa viumbe wote.
Hakuna kitu kinachofahamisha kuwa makusudio ya neno zuri ni neno lenye faida na manufaa kuliko kufananishwa kwake na mti mzuri ambao mizizi yake ni imara haungolewi na kimbunga na matawi yake yako mbinguni uko mbali na mabalaa ya dunia na uchafu wake.
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake sio kuwa mara nyingine unakuwa mkarimu na mara nyingine unakuwa bakhili; kama mfanya biashara wa nipe nikupe. Huu unatoa tu wakati wote.
Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
Hufananisha maana ya ndani kwa maana ya dhahiri ili watu wafahamu njia ya uongofu wapate kuifuata na njia ya uongofu wapate kuiepuka.
Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu.
Kila neno linalodhuru watu wala lisiwanufaishe; hilo ni lenye kulaaniwa; ni sawa liwe linatokana na Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu; awe wa hali ya juu au mlalahoi. Bali kunyamazia batili kunahisabika ni katika madhambi makubwa. Kuna hadithi inayosema: “Mwenye kunyamazia haki ni shetani bubu.”
Ghandi alimwandikia Taghore “Hakika wewe ni mshairi adhimu lakini unacheza na nyumba inaungua ... nyimbo nzuri nzuri hazimshibishi mwenye njaa wala kumponyesha mgonjwa”
Ulion’golewa juu ya ardhi, hauna uimara.
Huu ni mfano sahii kabisa wa batili na watu wake wanojifanya wakubwa na wajinga wakidhaniwa kuwa wao ni watu wazito kumbe ni kama mti tu uliosimama bila ya mizizi, mara moja unaweza ukalala chini unapopigwa na upepo.
Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera.
Makusudio ya wale walioamini sio waliosema tumemwamini Mungu na siku ya mwisho tu, kisha wasiisimamishe haki na kuipinga batili; isipokuwa makusudio ya wale walioamini ni wale aliowakusudia Mwenyezi Mungu katika kauli yake: “Hakika waumini ni wale tu walio mwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho; kisha wasiwe na sahaka na wakapigania njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao” (49:15)
Lakini wakidai tu kumwamini Mwenyezi Mungu kisha wasiizuie dhulma na ufisadi kwa ushujaa, basi hao ni wenye shaka sio waumini .
Maana ya kuwaimarisha kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewapa habari katika Kitabu chake kupitia Mtume wake kuwa wao wako katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye ndiye mlezi wao na msimamizi wao, mwenye kuwahifadhi na kuwanusuru; kama alivyo washujaisha na kuwasifu kwa ukweli na ikhlasi na mengineyo katika fadhila. Ama kuwaimarisha katika maisha ya akhera kwa kauli thabiti ni kauli YakeMwenyezi Mungu:
يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنْتُمْ تَحْزَنُونَ {68}
Na anawapoteza madhalimu kwa kufuru yao na utwaghuti wao.
Mara nyingi Qur’an hutumia neno dhulma kwa maana ya kufuru na shirki, lakini makusudio ya dhulma hapa ni kuidhulumu mtu nafsi yake kwa kufuru na kumdhulumu mwingine kwa uadui na uzushi; kama ambavyo makusudio ya upotevu hapa ni adhabu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُرْتَابٌ {34}
Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo katika kumpa thawabu mtiifu na kumwadhibu mfisadi, wala hakuna mwenye kuzuia matakwa yake.
Nikiwa kwenye tafsiri ya Aya hii, nimesoma makala katika gazeti la Al-Ahram la Misr la tarehe 2, February 1969, yenye kichwa cha maneno: “Je ubinadamu utashuhudia kummalizika vita vya Atomic na kuanza vita vya sumu?” Miongoni mwa yaliyomo katika makala hiyo ni: “ Imejitokeza silaha mpya hatari zaidi na yenye nguvu kulio silaha za nyuklia.
Silaha hiyo ni ya sumu na kwamba athari yake ni mtu anapoigusa chembe tu, basi viungo vyake vinanywea, macho yanamtoka na kufa papo hapo. Na kwamba Amerika na Uingereza tayari ina viwanda vya kutengeneza silaha hizi na kuzihifadhi mpaka pale zitakapohitajika. Wakati mataifa yakitafuta muafaka wa kummaliza silaha za nyuklia, huku mataifa mawili haya yanatafuta silaha hatari zaidi, kama badili ya mabomu ya Atomic na Haidrojeni.”
Je, imani inaweza kuwa pamoja na nia na maazimio ya kutumia silaha hizi? Je swala za wale wanaowaunga mkono wenye nia hizo na maazimio hayo zitawafaa mbele ya Mwenyezi Mungu?
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ بَدَّلُوا نِعْمَتَ اللَّهِ كُفْرًا وَأَحَلُّوا قَوْمَهُمْ دَارَ الْبَوَارِ {28}
جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا ۖ وَبِئْسَ الْقَرَارُ {29}
وَجَعَلُوا لِلَّهِ أَنْدَادًا لِيُضِلُّوا عَنْ سَبِيلِهِ ۗ قُلْ تَمَتَّعُوا فَإِنَّ مَصِيرَكُمْ إِلَى النَّارِ {30}
قُلْ لِعِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا يُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُنْفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ يَوْمٌ لَا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خِلَالٌ {31}