Aya 28 -31: Walibadilisha Neema Ya Mungu Kwa Kufuru
Maana
Je, hukuwaona wale waliboadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru? Na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamivu? Nayo ni Jahnnam watakayoiingia ni mahala pabaya pa kukaa.
Dhamiri ya wakawafikisha inawarudia viongozi wa kufuru na upotevu. Makusudio ya neema ya Mwenyezi Mungu ni imani na uwongofu. Maana ni kuwa, je, hustajabu ewe Muhammad au ewe msikilizaji na msomaji, hali ya viongozi wa kufuru na upotevu ambao wamehiyari upotevu kuliko uon- gofu na moto kuliko neema, wakiingia humo wao na wafuasi wao, wakawa ndio kuni zake.
Mfano wa Aya hii ni kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ اشْتَرَوُا الضَّلَالَةَ بِالْهُدَىٰ فَمَا رَبِحَتْ تِجَارَتُهُمْ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ {16}
Tabariy amenukuu, katika kufasiri Aya hii, kwamba Umar bin Al-Khatab alisema: “Wale ambao wamebadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru ni koo mbili ovu katika maqurayshi: Bani Mughira na Bani Umayya. Ama Bani Mughira mliwatosha siku ya Badr na Bani Umayya watajifurahisha muda mchache tu.”
Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze katika njia yake.
Walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika, wakiwapenda kama kumpenda Mungu na kuwaabudu kama kumwabudu Mungu.
Ilivyo hasa ni kuwa wao walifanya hivyo kwa kukusudia kuongoka si kwa kukusudia kupoteza njia. Kwa hiyo neno kwa ‘ili’ hapa halina maana ya kuwa ndio lengo bali ni matokeo. Maana yanakuwa kwamba washirikina waliabudu masanamu kwa kukusudia kuongoka nayo na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, lakini natija ikawa ni kupotea, kuangamia na kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu. Neno ‘ili’ hapa liko sawa na mfano wa kusema: Amekuja mwenyewe ili afe.
Sema: Stareheni! Kwani hakika marejeo yenu ni motoni.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha mtume wake kuwahadharisha washirikina na mwisho mbaya na kuwaambia kuwa starehe za dunia ni chache hata kama zinawapendeza na Akhera ni ya mwenye takua. Lakini lugha ya haki inafaa kitu kwa wale ambao hawatingishwi na lolote zaidi ya faida na chumo?
Waambie waja wangu walioamini wasimamishe Swala ambayo mwenye kuiswali inamkumbusha Mungu na kumhadharisha na adhabu na mateso na kumkataza dhambi na makosa
Na watoe katika tulivyowaruzuku kwa siri na kwa dhahiri.
Zaka ni ndugu yake swala. Swala inamkumbusha Mungu na zaka inamkurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Umepita mafano wake katika Juz 3 (2:74).
Kabla ya kuwajia siku isiyokuwa na biashara wala urafiki.
Biashara hapa ni fumbo la fidia. Maana ni kuwa mwenye kutoa mali yake katika njia ya Mwenyezi Mungu atanufaika nayo huko akhera na mwenye kuifanyia ubakhili atakuwa na hasara na adhabu wala haitamfaa siku hiyo ambapo hakutakuwa na fidia wala urafiki. Umepita mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (13:18).
اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَكُمْ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْأَنْهَارَ {32}
وَسَخَّرَ لَكُمُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ {33}
وَآتَاكُمْ مِنْ كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِنْ تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنْسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ {34}