read

Aya 32 -34: Na Akateremsha Maji Kutoka Mbinguni

Maana

Ayazotehizitatuumepitamfanowakekamaifuatavyo:

Kuumbwa mbingu na ardhi: Juz. 7 (6:73).
Kutermshwa maji kutoka mbinguni: Juz. 1 (2:22) na Juz. hii tuliyo nayo (13:18).
Kupita majahazi: Juz. 2 (2:164).
Kunufaika na Jua na Mwezi: Juz. hii (13:2). Usiku na mchana Juz. 11(10: 67).

Mwenyezi Mungu ameweka idadi ya neema nyingi kwa waja wake katika Juz. hii na Juz. 8 (6:143144) na nyinginezo nyingi zilizokwisha tangulia pamoja na tafsiri yake na ufafanuzi wake. Mwenyezi Mungu amerudia hapa au kuzidokeza kwa mnasaba wa kubadilisha neema kwa kufuru.

Kwa ufupi Aya hizi tatu zinamaanisha kuwa neema za Mwenyezi Mungu hazihisabiki; kama vile kuumbwa mbingu na ardhi, kuteremshwa maji kuenda majahazi faida za jua, mwezi, usiku na mchana. Vile vile kuwafadhili watu kwa waliyoomba na wasiyoomba, lakini pamoja na neema zote hizo wengi wanamkufuru na kuzikufuru neema zake huku wakiabudu yasiyowanufaisha wala kuwadhuru.

Je Mtu Ana Maumbile Ya Hatia?

Kwa mnasaba wa kauli yake Mwenyezi Mungu: Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru, tunadokeza kwamba wataalamu wa saikolojia wametofautiana kuhusu binadamu, kuwa je, ana maumbile ya kufanya hatia, kwamba yeye amezaliwa kumfanyia uadui ambaye hajamfanyia uadui na kukufuru neema za aliyemfanyia wema (hana shukrani)

Mnamo mwaka 1832 watalamu 528 walikutana huko Amerika wakilijadili suala hili. Wengi wakaonelea kuwa hakuna dalili kuwa mwanadamu anaweza kuepuka kufanya makosa, lakini kundi jingine likapinga.

Sisi tunaamini kuwa binadamu hakuzaliwa kuwa ni mwenye kufanya makosa; vinginevyo angelikuwa hana taklifa yoyote na kuhisabiwa kwake na kuadhibiwa ingelikuwa ni dhulma na uonevu. Vile vile dini na sharia ingelkiuwa ni upuzi na mchezo; kama vile unyoya kwenye mavumo ya upepo. Isipokuwa anakuwa ni mwenye hatia kwa sababu nyingine za nje; kama vile njaa inayofanya awe mwizi, hadaa zinazomfanya awe na hiyana na kuwa kibaraka n.k.

Hapa ndio unapata tofauti baina ya watu katika nafsi zao. Wengine wanakuwa dhaifu mbele ya hadaa na kushindwa na matamnio; kama vile mwenye chakula lakini bado anataka ziada tena kwa hali yoyote; au mwenye mke anayemtosheleza, lakini anazini; au anayeificha haki kwa kupupia cheo au manufaa yoyote katika starehe za dunia. Hakuna mwenye shaka kwamba huyu amefanya dhambi kwa kutaka kwake sio kwa maumbile yake. Hayo ndiyo aliyoyakusudia Mwenyezi Mungu aliposema:
‘Hakika mtu ni dhalimu mkubwa mwingi wa kukufuru.’

Ni wazi kuwa kupondokea haramu hakuifanyi kuwa ni halali, madamu iko nafasi ya kuweza kufanya subira na kushinda mapondokeo haya. Tumetangulia kueleza yanayoambatana na utafiti huu katika kufasiri Juz. 12 (11:9).

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَنْ نَعْبُدَ الْأَصْنَامَ {35}

Na Ibrahim aliposema: Ewe Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.

رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِنَ النَّاسِ ۖ فَمَنْ تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ۖ وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {36}

Ewe Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi atakayenifuata, hakika huyo ni katika mimi na atakayeniasi basi hakika wewe ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

رَبَّنَا إِنِّي أَسْكَنْتُ مِنْ ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِنْدَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُمْ مِنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ {37}

Ewe Mola wetu! Hakika mimi nimeweka baadhi ya dhuria zangu katika bonde lisilokuwa na mmea, kwenye nyumba yako takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda ili wapate kukushukuru.

رَبَّنَا إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِي وَمَا نُعْلِنُ ۗ وَمَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ {38}

Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyafichua, na hapana kitu kinachofichikana mbele ya Mwenyezi Mungu katika ardhi wala mbingu.

الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ ۚ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاءِ {39}

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu ni mwenye kusikia sana dua.

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِنْ ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ {40}

Ewe Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kuisimamisha Swala na katika dhuria zangu pia. Ewe Mola wetu! Na utakabalie dua yangu.

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ {41}

Ewe Mola wetu! Nighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini siku ya kusimama hisabu.