read

Aya 35-41: Ewe Mola Wangu Ujaalie Mji Huu Uwe Wa Amani

Na Ibrahim aliposema: “Ewe Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani.”

Ibrahim na Ismail ndio waliojenga Al-ka’ba Makka. Angalia Juz. 1 (2:127).

Ibrahim na Ismail walimwomba Mola wao awajalie watu wawe na amani, na akawaitikia dua yao. Walikuwa na wanaendelea kuwa maadui wanakutana bila ya kuhofiana. Katika hili Mwenyezi Mungu ameashiria kwa kusema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ ۚ {67}

“Je hawaoni kuwa tumeifanya nchi takatifu iwe ya amani na hali watu wengine wananyakuliwa kwa majirani zao? (29:67)

Na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.

Ni muhali kabisa kwa Ibrahim kuabudu masnamu. Itakuwaje ayaabudu naye aliyavunja kwa mikono yake na akawaambia:

أُفٍّ لَكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {67}

قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانْصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ فَاعِلِينَ {68}

“Je, mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyofaa chochote wala kuwadhuru. Kefle yenu! Na mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Je, hamtii akili?” (21: 67-68),

lakini mitume wa Mwenyezi Mungu na manabii wake –pamoja na isma yao – wanaogopa maasi. Hofu hii ndiyo daraja ya juu ya utiifu. Anayejiona ni mtakatifu basi amemfungulia shetani madirisha.

Mitume Na Kuitikiwa Dua

Unaweza kuuliza kuwa Ibrahim alimuomba Mola wake kuwa watoto wake wawe waumini, asimshirikishe Mwenyezi Mungu hata mmoja wao; na inajulikana kuwa wengi katika kizazi chake walimshirikisha Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu, wakiwemo maquraish ambao wao ni katika kizazi chake?

Razi amenukuu majibu matano kutoka kwa wafasiri, lakini bado swali liko palepale linataka jawabu.

Tuonavyo sisi ni kuwa dua ni maombi na matarajio; ni sawa iwe inatoka kwa Nabii au mwinginewe. Inaweza kuwa hekima yake Mwenyezi Mungu inataka kuyakubali maombi na wakati mwingine kuyakataa. Wala hiyo haimaanishi kuwa aliyekataliwa maombi hana uzito wowote mbele ya Mungu kuweza kudhuru cheo cha utume na isma yake.

Hapana! Kwani kukataliwa maombi hakummaanishi hasira za mwenye kuombwa kwa muombaji; bali inawezekana kuwa ni mapenzi zaidi kwake na kuchunga masilahi yake. Nuhu (a.s.) alimtaka Mwenyezi Mungu kumuokoa mtoto wake kutokana na kuangamia, Mola wake akamjibu kwa kusema: “Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo” Juz.12 (11:46).

Kwa maneno mengine ni kuwa dua ya Nabii Ibrahim haina tafsiri nyingine zaidi ya hamu yake na mapenzi. Hakuna mwenye shaka kwamba manabii wana hamu na wanapendelea watu wote waamini na waongoke kwenye haki. Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu alimwambia Bwana wa mitume aliyeadhimu:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۚ {56}

“Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendae, lakini Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye” (28:56).

Lau yangehakikia kila wanayoyataka mitume basi asingelipatikana hata kafiri mmoja duniani na mitume wasingelisumbuka; hasa yule bwana wao na wa mwisho wao ambaye alisema: “Hakuudhiwa mtume kama nilivyoudhiwa mimi”

Ewe Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi.

Makusudio ya hayo ni ya masanamu. Maana ni kuwa wengi katika watu wamepotea kwa sababu ya ibada ya masanamu; sawa na kusema: mali imempoteza fulani; yaani amepotea kwa sababu yake.

Basi atakayenifuata, katika kizazi changu, hakika huyo ni katika mimi kinasabu na kidini. Na atakayeniasi basi hakika wewe ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Atakayemuasi Ibrahim (a.s.) basi yuko mbali naye sana hata kama ndiye aliyekaribu zaidi kiudugu kuliko watu wengine. Kwa sababu atakayemuasi atakuwa amemuasi Mwenyezi Mungu.

Lakini, pamoja na hayo, Ibrahim ni mpole mno mwenye kurudi kwa Mwenyezi Mungu; kama alivyomsifu yule aliyemchagua kuwa kipenzi na akamtakasa. Ndio maana hakuwatakia adhabu waasi katika kizazi chake, bali alimwachia Mwenyezi Mungu mambo yao kwa masamaha wake na maghufira yake.
Ilivyo ni kuwa akili haizuwii kusamehewa washirikina, kwa sababu adhabu ya washirikina ni haki ya Mwenyezi Mungu. Akitaka atwaadhibu na akitaka atawasamehe. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamei kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo” Juz.5 (4:48), ni dalili ya kiusikilizaji si dalili ya kiakili. Angalia tafsiri yetu huko, tumefafanua zaidi.

Ewe Mola wetu! Hakika mimi nimeweka baadhi ya dhuria zangu katika bonde lisilokuwa na mmea, kwenye nyumba yako takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swala.

Aliyasema haya Ibrahim (a.s.) pale alipomwacha Ismail na mama yake Makka, pakiwa ni bonde kavu, halina chochote, si maji wala mmea; isipokuwa nyumba tu inayosimamishwa swala ndani yake na kukaririwa talbiya. Ni kwa lengo hili Ibrahim aliiweka baadhi ya famila yake mahali hapa pa kame. Lakini binadamu haishi kwa swala peke yake, bali hana budi apate mkate vile vile, ndipo Ibrahim akasema:

Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda ili wapate kukushukuru.

Ikiwa kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu hakuna mmea wala kiwele, basi watu waelekee huko kwa ibada au biashara wakiwa na mkate na matunda, ili familia ya Ibrahim nayo ipate kula na kuweza kuswali na kushukuru.

Musa (a.s.) alisema: “Mola wangu! Hakika mimi ni muhitaji wa heri utakyoiteremsha” (28:24). Imam Ali (a.s.) anasema: “Wallahi hakumuomba isipokuwa mkate atakokula” Alisema mshairi aliye faqih: Fadhila ni za mkate lau si huo kamwe hata siku hakuna aabaduo.

Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyafichua, na hapana kitu kinachofichikana mbele ya Mwenyezi Mungu katika ardhi wala mbingu.

Baada ya Ibrahim kuuomba watu wafike nyumbani kwake wakiwachukulia familia yake mkate na matunda ili wapate nguvu na uchangamfu wa kuabudu, baada ya haya alisema maombi yangu haya si lolote ila ni unyenyekevu na kukiri kuwa wewe ni Muumba Mwenye kuruzuku. Ama haja yetu na masilahi yetu wewe unayajua zaidi kuliko sisi; tuwe tumekuomba au hatukuomba.

Kwa hiyo kauli ya Ibrahim ‘tunayofichua’ maana yake ni tunayoyaomba na maana ya ‘tunayoyaficha’ ni yale tusiyoyaomba.

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu ni mwenye kusikia sana dua.

Shukrani hii kutoka kwa Ibrahim imechanganya maombi ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa wanawe, Ismaili na Is-haq. Kwa vile Ibrahim amekwishakuwa mzee na muda wake umekurubia, ndipo akawakilisha mambo ya familia yake kwa Mwenyezi Mungu; wala hakuwabainishia kitu au kuwalimbikizia mali watoto wake ili wastarehe na kuwanyima wengine.

Ewe Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kuisimamisha Swala na kati- ka dhuria zangu pia. Ewe Mola wetu! Na utakabalie dua yangu.

Swala ya Ibrahim sio aina ya hii swala tunayoiswali sisi; bali ni katika aina ya swala amabyo Mwenyezi Mungu ameiainisha kwa kusema:

إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ ۗ {45}

“Hakika Swala huzuia mambo machafu na maovu” (29:45).

Ndio hapa mafakihi wakaigawanya swala katika mafungu mawili: Swala ya kutekeleza wajibu tu, lakini mtekelezaji halipwi kitu; na Swala ya kutekeleza wajibu na mtekelezaji analipwa. Hiyo ni ile ambayo inaleta ikhlasi katika matendo na ukweli katika kuamiliana na watu.

Ewe Mola wetu! Nighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini siku ya kusimama hisabu.

Tumetangulia kueleza katika Juz. 7 (6: 74) tofauti baina ya Sunni na Shia kuhusu imani ya baba wa Ibrahim Al-khalil (a.s.). Miongoni mwa tuliyoyasema ni kuwa mzozo huu na mfano wake ni tasa, na kwamba linalotakikana kwa Mwislamu ni kuitakidi isma ya mitume. Ama kuamini kuwa mababa zao walikuwa waumini si itikadi ya uislamu kabisa.

Lau mtu atasema mimi ninamwamini Mungu na umoja wake, mitume na isma yao na siku ya mwisho na hisabu, lakini sithibitishi wala si kanushi imani ya mababa wa Mitume, Atakayesema hivi, tutamwambia kuwa wewe ni Mwislamu, unastahiki wanyostahiki waislamu nawe unawajibu wa kuwafanyia wanayostahiki waislamu wenzako.

وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ {42}

Wala usidhani kuwa Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho.

مُهْطِعِينَ مُقْنِعِي رُءُوسِهِمْ لَا يَرْتَدُّ إِلَيْهِمْ طَرْفُهُمْ ۖ وَأَفْئِدَتُهُمْ هَوَاءٌ {43}

Nao wako mbioni, vichwa vyao viko juu, macho yao hayapepesi na nyoyo zao ni tupu.

وَأَنْذِرِ النَّاسَ يَوْمَ يَأْتِيهِمُ الْعَذَابُ فَيَقُولُ الَّذِينَ ظَلَمُوا رَبَّنَا أَخِّرْنَا إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ نُجِبْ دَعْوَتَكَ وَنَتَّبِعِ الرُّسُلَ ۗ أَوَلَمْ تَكُونُوا أَقْسَمْتُمْ مِنْ قَبْلُ مَا لَكُمْ مِنْ زَوَالٍ {44}

Na waonye watu siku itakapowajia adhabu na waliodhulumu waseme: “Ewe Mola wetu! tuakhirishe muda kidogo tutaitikia wito wako na tutafuata mitume.” Je, hamkuwa mmeapa tangu zamani kuwa nyinyi hamtaondolewa?

وَسَكَنْتُمْ فِي مَسَاكِنِ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ وَتَبَيَّنَ لَكُمْ كَيْفَ فَعَلْنَا بِهِمْ وَضَرَبْنَا لَكُمُ الْأَمْثَالَ {45}

Na mkakaa katika maskani za wale waliodhulumu nafsi zao? Na ikawabainikia jinsi tulivyowafanya na tukawapigia mifano?