read

Aya 42-45: Dhalimu Anajisahau Lakini Hasahauliwi

Wala usidhani kuwa Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho.

Dhulma ni aina nyingi: Kufru na shirki ni dhulma na kuikeuka haki miongoni mwa haki za watu ni dhulma; ni sawa iwe ni haki ya kitu au hali; hasa ikiwa anayenyanganywa haki yake ni dhaifu.

Kwa sababu kumdhulumu dhaifu ni uovu mbaya zaidi. Na mwenye kumsaidia dhalimu, kuridhia vitendo vyake au kumnyamazia na huku uwezo anao angalau kumtangaza, basi huyo atakuwa mshirika wake. Ni kwa ajili hii ndio Mwenyezi Mungu haghafiliki na wanayoyafanya madhalimu.

Tumezungumzia dhulma katika kufasiri mwanzo wa Juz.6 (4:148). Tukiunganisha tuliyoyasema huko na hapa ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutuma mitume wala kuteremsha Vitabu isipokuwa ni kwa kupiga vita dhulma na madhalimu. Mwenyezi Mungu amejisifu katika Kitabu chake kuwa Yeye ni mwenye kuadhibu. Lau si dhulma, wasifu huu usingekuwa na athari yoyote.

Kadiri dhulma inavyozidi muda wake ndivyo adhabu yake inavyokuwa kubwa na kali zaidi. Imam Ali anasema: “Mwenyezi Mungu atamwadhibu mwenye kudhulumu tonge kwa tonge na tamaa kwa tamaa”. Mwenye kumdhulumu mtu kwa neno moja tu malipo yake ni makomeo ya chuma, basi itakuwaje kwa yule aliyeigeuza ardhi kuwa moto na akaweka kambi ya jeshi kila mahali na maghala ya silaha za maangamizi?
Nao wako mbioni, vichwa vyao viko juu, macho yao hayapepesi na nyoyo zao ni tupu.

Wamekodoa macho kwa sababu ya mshangao na wanafanya haraka kuitikia mwito wa anayeita, wamenyanyua vichwa kwa mshangao. Ama nyoyo zao hazina hisia kutokana na hofu. Hivi ndivyo itakavyolipwa kila nafsi kutokana na iliyoyachuma.

Na waonye watu siku itakapowajia adhabu na waliodhulumu waseme: “Ewe Mola wetu! tuahirishe muda kidogo tutaitikia wito wako na tutafuata mitume.”

Mwenyezi Mungu aliwatuma manabii na mitume wake kwa waja wake watoe bishara ya thawabu na watoe onyo la adhabu. Watu walikuwa na wakati mwingi wa kupewa bishara na onyo, lakini watu wengi walikataa na kupinga, wakawaambia mitume wao: kweli, kuna kufa, kufufuliwa, kisha kukusanywa! Hizi ni ngano tu za watu wa kale. Mpaka watakaposimama mbele ya Mola Mwenyezi Mungu na pazia likiwafunukia watasema: ewe Mola wetu tupe muda kidogo tuweze kuwasikiliza mitume wako na tuwatii. Watasema haya ikiwa hakuna wakati tena.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha mtume wake Muhammad (s.a.w.) kuwapa hadhari washirikina na kuwaonya na siku hii, ambayo haina kuahirisha wala kurudi nyuma, kabla haijawafikia.

Na kuwapa habari ya matokeo kama wakiendelea na inadi; na kwamba wao watamwambia Mwenyezi Mungu: Tuahirishie ili tuitikie wito wa mitume, lakini wapi! Mtume amekwishatekeleza ujumbe wa Mola wake akawapa bishara na akawahadharisha, lakini manufaa na tamaa iliwashinda, wakawa miongoni mwa watu waliohasirika.

Je, hamkuwa mmeapa tangu zamani kuwa nyinyi hamtaondolewa? Na mkakaa katika maskani za wale waliodhulumu nafsi zao? Na ikawabainikia jinsi tulivyowafanya na tukawapigia mifano?

Maneno haya yote Mwenyezi Mungu kesho atawaambia wale waliokadhibisha ambao watamwambia Mwenyezi Mungu turudishe mara ya pili duniani ili tuwafuate mitume. Atawajibu, Yule ambaye limetukuka neno lake, kwa kuwauliza swali la kusuta, kuwa nyinyi si mliapa duniani kuwa hakuna kuondoka katika maisha ya dunia kwenda maisha ya Akhera na kwamba hakuna pepo wala moto.

Ameyadokeza hayo Mwenyezi Mungu katika Aya nyingine kwa kusema:

وَأَقْسَمُوا بِاللَّهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ ۙ لَا يَبْعَثُ اللَّهُ مَنْ يَمُوتُ ۚ {38}

“Na wanaapa ukomo wa viapo vyao kwamba Mungu hatamfufua afaye” (16:38).

Baada ya swali hili au masuto haya, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaendelea kuwaambia kuwa mnajua hali ya mwanzo jinsi tulivyowaangamiza walioasi, tukawahadharisha msifate vitendo vyao na tukawapigia mifano yao wala hamkuwaidhika na mkazingatia.

Hivi sasa ambapo hakuna kurejea wala kuakhirishwa, sasa mnasema tungojee kidogo, ni mantiki gani haya? Je si Mwenyezi Mungu aliwaletea mitume mkawachezea mpaka mrudishwe mara ya pili na mtumiwe mitume wengine wapya?

وَقَدْ مَكَرُوا مَكْرَهُمْ وَعِنْدَ اللَّهِ مَكْرُهُمْ وَإِنْ كَانَ مَكْرُهُمْ لِتَزُولَ مِنْهُ الْجِبَالُ {46}

Na kwa hakika wamekwishafanya vitimbi vyao na vitimbi vyao viko kwa Mwenyezi Mungu, ingawa vitimbi vyao vinaweza kuondosha mlima.

فَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّهَ مُخْلِفَ وَعْدِهِ رُسُلَهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ ذُو انْتِقَامٍ {47}

Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi yake mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushinda, Mwenye kulipiza kisasi.

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ {48}

Siku itakapobadilishwa ardhi kuwa ardhi nyingine na mbingu (pia). Nao watahud- huria mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja, Mwenye nguvu.

وَتَرَى الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ {49}

Na utawaona wahalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo.

سَرَابِيلُهُمْ مِنْ قَطِرَانٍ وَتَغْشَىٰ وُجُوهَهُمُ النَّارُ {50}

Nguo zao zitakuwa za lami na moto utazigubika nyuso zao.

لِيَجْزِيَ اللَّهُ كُلَّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ {51}

Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

هَٰذَا بَلَاغٌ لِلنَّاسِ وَلِيُنْذَرُوا بِهِ وَلِيَعْلَمُوا أَنَّمَا هُوَ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ وَلِيَذَّكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ {52}

Hii (Qur’an) ni ujumbe wazi kwa watu iwaonye na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.