Aya 46 - 52: Walifanya Vitimbi Vyao
Maana
Na kwa hakika wamekwishafanya vitimbi vyao na vitimbi vyao viko kwa Mwenyezi Mungu, ingawa vitimbi vyao vinaweza kuondosha mlima.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutuma Mtume ila alifanyiwa vitimbi na kupangiwa njama na watu wafisadi na wapotevu, kuanzia enzi za Nabii Nuh mpaka kwa Muhammad (s.a.w.):
وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنْسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ {112}
Sababu za uadui huo haziko tu baina ya kupingana imani na ulahidi na baina ya shirki na Tawhid, hapana, uadui huu ni matokeo ya maana ya kiujumla, ambayo ni uadui baina ya haki na batili kila mahali na kila wakati. Au kwa maneno ya kisasa ni uadui baina ya mapinduzi na kupinga mapinduzi.
Sababu yoyote ya vitimbi na njama itakavyokuwa na kwa namna yoyote itakavyokuwa na nguvu hata kuweza kusogeza mlima kutoka mahali pake, basi Mwenyezi Mungu anaijua na atawalipa wahusika wanayostahiki.
Kwa mnasaba huu tunadokeza kuwa wanaume wengi wanawasifu wanawake kuwa wana vitimbi na hadaa kwa kutoa ushaidi wa Aya isemayo:
إِنَّ كَيْدَكُنَّ عَظِيمٌ {28}
Wanawake nao wanaweza kuwajibu wanaume kuwa vitimbi vyao vinaondosha mlima na watoe ushahidi kwa Aya hii.
Zaidi ya hayo ni kwamba wasifu wa wanawake kuwa wana vitimbi umekuja katika Qura’n kupitia kwenye ulimi wa waziri, lakini wasifu wa wanaume kuwa wana vitimbi umekuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja.
Jambo la kushangaza ni kuwa badhi ya wanaume wanatoa dalili ya vitimbi vya wanawake kwa Aya hii inayowahusu wanume kwa kuweka dhamir ya wanawake (Hunna) mahali pa dhamiri ya wanaume (hum).
Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi yake mitume wake kwa kuinusuru haki na watu wake na kuidhalilisha batili na wasaidizi wake. Mwenyezi Mungu anaishiria ahadi yake kwa mitume kwa kusema:
كَتَبَ اللَّهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي ۚ {21}
Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushinda, Mwenye kulipiza kisasi.
Anawalipizia kisasi wenye haki kwa wenye batili.
Siku itakapobadilishwa ardhi kuwa ardhi nyingine na mbingu (pia).
Hiyo ni kwa kugeuzwa ardhi kuwa vumbi kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
فَكَانَتْ هَبَاءً مُنْبَثًّا {6}
Ama nyota za mbinguni ni kuwa zitapukutika na kuanguka kama ilivyoelezwa katika Sura ya, 75, 71 na 82.
Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja Mwenye nguvu mahali wazi hakuna mlango wala nguo. Miongoni mwa maelezo ya mahali watakapokusanyika na sifa zake ni kuwa ni uwanja mweupe ulio mtupu, hauna miti wala wala mabonde na milima, ardhi nyeupe kama fedha, haijamwagikiwa na damu, wala kufanywa makosa. Mbingu itakuwa kama shaba iliyoyeyuka, Jua, mwezi na nyota zitaondoka, na mlima itakuwa kama sufi.
Jahnnam Na Silaha Za Maangamizi
Na utawaona wahalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo. Nguo zao zitakuwa za lami na moto utazigubika nyuso zao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja picha kadhaa za watu wa motoni. Kuzisoma kunaleta kitisho katika nafsi na manywele na damu kusisimka, sikwambii huyo atakyeionja atakuwaje.
Miongoni mwa picha hizo ni kuwa wahalifu watafufuliwa wakiwa wamefungwa minyororo, kivazi ni cha aina inayoshika moto na kwenye nyuso zao mna kifuniko cha moto. Ama chakula chao kinatokana na mti wa zakkum na kinywaji chao ni usaha uliochanganyika na damu. Zaidi ya hayo watakuwa kwenye Jahannam ambayo haibakishi wala haisazi, inatupa cheche kama majumba na milima.
Unaweza kuuliza kuwa aina hii ya adhabu haipingani na upole wa Mwenyezi Mungu na rehema yake? Kweli binadamu aliye dhaifu wa nyama na mifupa na damu anaweza kutosha kwenye adhabu hii?
Baadhi wamejibu swali hili, kwamba aina ya adhabu na picha zake alizozitaja Mwenyezi Mungu si za uhakika; isipokuwa alitaka kuwahofisha watu na makosa.
Mwenye majibu haya lau atairejea Qura’n tukufu atakuta kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alikwishajua kwamba wengi katika waja wake watapitiwa na swali hili katika mawazo yao, hivyo akawajibu kimbele. Amebainsha hakiki hii katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni le aliyoitaja mara tu baada ya kutaja kifungo cha minyororo na kivazi cha lami, akasema moja kwa moja:
ili Mwnyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyoyachumma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
Nyingine ni hizi zifuatazo:
هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {147}
وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا {49}
وَأَنَّ اللَّهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِلْعَبِيدِ {182}
وَمَنْ جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {160}
وَالَّذِينَ كَسَبُوا السَّيِّئَاتِ جَزَاءُ سَيِّئَةٍ بِمِثْلِهَا {27}
فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ ۚ {194}
Maana ya Aya hizi kwa ujumla ni kuwa uhalifu na maovu yako aina nyingi: kuna yale madogo na makubwa na kwamba yeye Mwenyezi Mungu ameliwekea kila kosa na adhabu yake kwa misingi ya haki na uadilifu bila ya kuzidisha; pengine kupunguza kulingana na hekima yake itakavyotaka. Kauli yake Mwenyezi Mungu “Hatalipwa isipokuwa mfano wake,” inaliweka wazi hilo.
Naam! Kuna swali ambalo kila mwenye akili anapaswa kujiuliza, nalo ni nani basi anayestahiki adhabu hiyo kali kiasi hicho? Je, kuna kosa linalowajibisha aina yote hii ya mateso ambayo yana mwanzo lakini hayana mwisho? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: “Na wale ambao wamekufuru watakuwa katika moto wa Jahannam, hawatahukumiwa wapate kufa wala hawatapunguziwa adhabu yake” (35:36).
Jibu, ndio wako watu wanostahiki aina hiyo ya adhabu kali na zaidi ya hiyo. Miongoni mwao ni wale wanaoipiga vita haki au kuificha na huku wanajua; ni sawa haki hii iwe ni ya Mwenyezi Mungu au ya watu.
Na wenye hatia kubwa zaidi katika watu ni wafanya biashara wa vita ambao wanandaa kumwaga damu na kuharibu maisha kwa silaha za maangamizi; kama vile mabomu ya atomiki, haidrojeni na silaha za sumu ambazo zinaua mamia, bali hata mamilioni katika dakika chache.
Adhabu yoyote watakayopewa wauaji hawa haiwatoshi. Minyororo na nguo za moto si chochote kulinganisha na kuvunja miji, kuwafukuza watu kwenye miji yao na kuwaua kwa maelfu.
Kisha Je, cheche za moto wa Jahannam ni mbaya zaidi kuliko bomu la atomic lililotupwa Hiroshima? Na inajulikana hivi sasa mabomu wanayomiliki wauaji, ni mara elfu zaidi kulinganisha na hayo ya Hiroshima.
Je, chakula cha Zakkum na maji ya usaha uliochanganyika na damu unamaliza watu kuliko silaha za sumu wanazozitumia maadui wa Mwenyezi Mungu hivi sasa huko Vietnam na kabla yake Korea?
Yametangulia maelezo katika kufasiri Aya ya 8, ya Sura hii kwamba kuna silaha ambazo mtu ikimgusa chembe tu, basi viungo vyake vinanywea, macho yanamtoka na kufa hapo hapo.
Baada ya yote haya, mwenye akili anaweza kuwa na shaka kwamba kuwahurumia wanaomiliki silaha hizi ni dhulma na dhambi? Na kwamba wao lau wataadhibiwa na adhabu kali zaidi ya Jahannam ingelikuwa adhabu yao ni haki na uadilifu?
Je, adhabu yoyote itaonekana ni zaidi kwa yule ambaye ana kiu cha damu ya maelfu wala hashibi isipokuwa kwa kunyonya chakula cha wanyonge na kuiba mali zao?
Lau kusingelikuwa na dalili yoyote ya kufufuliwa watu isipokuwa kupatikana madhalimu hawa, ingelitosha; kwamba lau dunia ingelikuwa ndio kila kitu na kusiweko ulimwengu mwingine ambao haki itarudishiwa wenyewe na apate kila dhalimu stahiki yake, basi ingelikuwa mauti ni bora kuliko uhai na dhulma ni bora kuliko uadilifu.
Hii ni ujumbe wazi kwa watu iwaonye na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu mmoja na wapate kukumbuka wenye akili.
Hii ni ishara ya Qur’an na yaliyomo ndani yake miongoni mwa makemeo na ahadi. Makusudio ya ujumbe wazi ni kutosheleza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameteremsha Qur’an kwa nabii wake ikiwa ni tosha na yenye kutekekeleza kila mahitaji ya watu katika mambo ya dini yao na dunia yao. Vile vile inawafundisha ummoja wa Mungu na uadilifu wake na kuwaonya wasihalifu amri Yake na makatazo Yake.