Aya 1-6: Iko Wapi Dalili Ikiwa Nyinyi Ni Wa Kweli?
Maana:
Haamiim. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 25 (45:1) na Juz. 23 (39:1).
Hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda uliowekwa.
Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima, haumbi kitu ila kwa hikima, na ni muhali kuumba kwa mchezo. Ameuumba ulimwengu na yaliyomo ndani yake kwa hikima na malengo sahihi. Akauwekea muda maalum wa kwisha kwake; baada yake ni hisabu na malipo katika nyumba ya pili.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (30:8).
Na wale waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa.
Mwenyezi Mungu anawahofisha wakosefu na siku ya Kiyama na vituko vyake, na akawawekea dalili wazi, lakini wakakataa isipokuwa inadi na jeuri.
Je, mnawaona wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au wana shirika katika mbingu?
Maana ni kuwa nipeni habari enyi waabudu masanamu, ni jambo gani liliowafanya muyafanye masanamu ni miungu na kuyaabudu. Je, ni kwa kuwa yameumba kitu katika ardhi na mbinguni au yalishirikiana na Mwenyezi Mungu katika kuumba mbingu au sehemu yake?
Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki cha Qur’an; kama vile Tawrat, Injil n.k., kinachosema kuwa masanamu ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake au kuwa yanaweza kuwaombea kwa Mungu au kuwa na utajo wowote.
Au athari yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
Ikiwa hamna dalili ya nukuu yoyote, je mnayo dalili ya kiakili kusadikisha myasemayo na kuyafanya sahihi mnayoyaabudu?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (35:40).
Kuabudu Masanamu Wakati Maendeleo Ya Kufika Angani
Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametilia umuhimu sana kuwarudi wenye kuabudu masanamu na mizimu kwenye Aya hii na nyinginezo, na hali hili sio jambo zito sana na liko wazi kabisa? Kuupinga uungu wa masanamu si ni jambo liliowazi; sawa na kuukanusha upofu na uoni na giza na nuru?
Jibu: Kuyatukuza masanamu na kuyaabudu, kumekua ni sehemu ya maisha ya mtu kuanzia zama na Nuh (a.s.) mpaka zama za Muhammad (s.a.w.), ambapo baina ya wawili hao kuna maelefu ya miaka; bali mpaka hivi sasa kwenye maendeleo ya kufika angani, bado masanamu yameenea mashariki mwa ardhi na magharibi yake.
Masanamu yaliyoko kwenye nyumba za ibada, siku hizi, kwenye njia panda na kwenye vilele vya milima. Pia mapicha kwenye kuta yaliyoenea huku na huko na kwenye vitabu vya kumbukumbu si ni aina ya kuabudu masanamu?
Umetukuka ukuu wa Muhammad (s.a.w.) katika kumtukuza mtu kwa kumsafisha na ibada ya masanamu yaliyotengenezwa na mikono yake. Mshairi anasema:
Namshangaa insani mchonga jiwe ambaye
Hulifanya rahamani Mungu aabudiwaye
Huku adhani moyoni hudhuru na kumfaaye
Si aabudu mikono ilochonga hilo jiwe
Hayo si ndio maono lau ataka ajuwe
Basi na iwe mikono ya kuabudu si jiwe
Ndiyo imechonga jiwe kama anavyoelewa
Na nani mpotofu mkubwa kuliko hao wanaowaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, ambao hawatawaitikia mpaka Siku ya Kiyama, Makusudio ya kusema ‘mpaka siku ya Kiyama,’ ni milele na kutowezekana kujibu kabisa. Maana ni kuwa hakuna mjinga aliyepotea zaidi kuliko yule anayeabudu kisichosikia anayeita wala kumjibu anayeomba.
Na wala hawatambui maombi yao.
Washirikina wanaabudu masanamu, lakini masanamu hayana habari nao, wala hayana hisia yoyote.
Na watakapokusanywa watu watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.
Vile vile siku ya Kiyama wakati watu watakapofufuliwa kwa hisabu na malipo, miungu ya washirikina itajitenga nao na kuwakataa. Tazama Juz.11(10:28).
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ هَٰذَا سِحْرٌ مُبِينٌ {7}
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ إِنِ افْتَرَيْتُهُ فَلَا تَمْلِكُونَ لِي مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَا تُفِيضُونَ فِيهِ ۖ كَفَىٰ بِهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۖ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {8}
قُلْ مَا كُنْتُ بِدْعًا مِنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُبِينٌ {9}
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كَانَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ وَكَفَرْتُمْ بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {10}
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا لَوْ كَانَ خَيْرًا مَا سَبَقُونَا إِلَيْهِ ۚ وَإِذْ لَمْ يَهْتَدُوا بِهِ فَسَيَقُولُونَ هَٰذَا إِفْكٌ قَدِيمٌ {11}
وَمِنْ قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً ۚ وَهَٰذَا كِتَابٌ مُصَدِّقٌ لِسَانًا عَرَبِيًّا لِيُنْذِرَ الَّذِينَ ظَلَمُوا وَبُشْرَىٰ لِلْمُحْسِنِينَ {12}