Aya 7 – 12: Au Wanasema Wameyatunga?
Maana:
Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, wale waliokufuru husema juu ya haki inapowajia: Huu ni uchawi ulio wazi.
Makusudio ya ishara zetu na haki ni Qur’an. Maana ya zilizo wazi ni kuwa Aya za Qur’an ziko wazi hazikufunganafungana. Lakini pamoja na kuwa Qur’an iko wazi na kudhihiri dalili kuwa ni haki, bado wazushi, walio mataghuti na wapenda anasa wameipa sifa ya uchawi ulio waziwazi. Si kwa lolote ila ni kwa kuwa imewafanya wao kuwa sawa na watu wengine. Umetangulia mfano wa hayo katika Aya kadhaa huko nyuma.
Au wanasema: Ameizua! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.
Je, washirikina wanadai kuwa umeizua hii Qur’an ewe Muhammad (s.a.w.)? Waambie: vipi nimzulie Mungu uwongo na hali mimi ndiye ninayemuhofia zaidi? Je, mtanikinga na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake ikiwa nitasema uwongo au kumzulia? Aliyasema haya Mtume kutegemea vile wanavyomjua yeye jinsi anavyochukia uwongo na tabia nyinginezo mbaya.
Yeye anajua zaidi hayo mnayoropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi.
Hakifichiki kitu katika kauli zenu na vitendo vyenu nanyi mtahisabiwa navyo; na Mwenyezi Mungu ananijua mimi na nyinyi, kwa hiyo anashudia ukweli na uaminifu kwangu na anashuhudia uwongo na hiyana kwenu
Na Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Atawasamehe na kuwachanganya kwenye rehema yake ikiwa mtatubia na kurejea.
Sema, mimi si kioja miongoni mwa Mitume.
Mimi si wa kwanza kufikisha ujumbe wa Mungu. Wamenitangulia mitume na manabii wengi
Wala sijui nitakavyofanywa mimi wala nyinyi.
Mtume (s.a.w.) anajua hali yake na hali ya washirikina huko Akhera. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa habari ya hilo; kama zinavyoeleza Aya kadhaa; mbali ya kuwa ilimu hii ni katika nyenzo za utume. Zimekuja Hadith mutawatir, kwamba Mtume aliwabashiria pepo watu kadhaa.
Kwa hiyo basi Maana ya Aya ni kuwa Mtume hajui yatakayowatokea katika maisha ya duniani na atawatia mtihani gani Mwenyezi Mungu. Vile vile hajui kuwa Mwenyezi Mungu atawaadhibu hapa duniani au ataahirisha adhabu yao mpaka siku ya ufufuo.
Mimi nafuata niliyopewa Wahyi tu, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji mwenye kubainisha.
Sio kazi ya muonyaji kujua ilimu ya ghaibu; isipokuwa yeye anafikisha anayopewa wahyi na Mwenyezi Mungu kuhusiana na yale yatakayowatokea washirikina.
Ieleweke kuwa Aya hii ilishuka kabla ya kushuka Aya inayosema kuwa mwisho ni wa dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wajapochukia washirikina. Au pengine ni miongoni mwa mifumo ya kutoa mwito kwa hikima na mawaidha mazuri.
Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na alishuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.
Sura hii tuliyo nayo imeshuka Makka isipokuwa Aya hii tuliyo nayo, ilishuka Madina kwa ajili ya Abdullah bin Salim, aliposilimu Madina. Yeye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa Wana wa Israil. Haya ndiyo yaliyoelezwa kwenye tafsiri nyingi.
Maana ni sema ewe Muhammad kuwaambia wale wanaodai kuwa Qur’an ni uchawi uliozushwa, hebu niambieni itakuwaje hali yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ikithibiti kuwa Qur’an ni haki na kweli na akaiamini mwana wa chuoni katika wana wa Israil; kama vile Abdullah bin Salam ambaye anatambua siri za wahyi na kushuudia kuwa mafunzo ya Qur’an ni kama mafunzo ya Tawrat iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Musa? Basi mtakuwaje mkibaki na upotevu wenu na inada yenu? Je mjidhulumu kwa hiyari yenu na kujianika kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu?
Na wale ambao wamekufuru waliwaambia wale ambao wameamini: Lau hii ingelikuwa ni heri, wasingelitutangulia.
Watu wengi walioitikia mwito wa Mtume (s.a.w.), mwanzo mwanzo wa mwito wa Uislamu, walikuwa ni miongoni mwa wanyonge. Kwa hiyo mamwinyi wakaifanya hiyo ni sababu ya kuituhumu risala ya Mtume. Kwa sababu, wanavyodai, ni kuwa haki ni ile inayokubaliwa na vigogo, wala sio kuwa watu wajulikane kwa kuwa na haki. Kila wanalolilifanya matajiri ndio haki na wanalolilifanya wengine ni batili. Hayo ndiyo madai yao, lakini kila mwenye kuipinga haki itamshinda.
Ndio maana hazikupita siku mtumwa wa kihabeshi akapanda kwenye mgongo wa Al-Ka’aba akinadi Lailaha illallah Muhammadurrasulullah (Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu). Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akayavunja masanamu na kuyatupa chini ya nyayo zake huku akisema: “Haki imefika na batili imeondoka, hakika batili ni yenye kuondoka.”
Katika Tafsir Arrazi, imeandikwa kuwa mjakazi wa Amru alisilimu na alikuwa akimpiga mpaka anachoka. Basi makafiri wakasema: “Kama Uislamu ungelikuwa ni kheri asingetutangulia majakazi wa Amru.” Lakini Amru mwenyewe alisilimu badaye, akapigana vita vya Roma na Fursi.
Na walipokosa kuongoka kwayo basi wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
Wanazungumziwa makafiri wa kikuraishi. ‘Kwayo’ ni hiyo Qur’an. Mataghuti waliisifu kuwa ya zamani, kwa vile, kwa madai yao, wanasema ni ngano za watu wa kale zilizopitwa na wakati.
Walisema hivi sio kwa lolote isipokuwa wao hawaamini isipokuwa masilahi yao na chumo lao tu, na Qur’an inapinga na kupiga vita hayo.
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa kiongozi na chenye rehema. Na hiki ni Kitabu chenye kusadikisha cha lugha ya kiarabu, ili kiwaonye wale waliodhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Qur’an ni kama Tawrat iliyomshukia Musa. Vitabu vyote hivyo viwili vinaongoza kwenye haki na ni rehema kwa mwenye kuviamini na avitumia kwa mujibu wake. Tawrat ilitoa habari za kuja Muhammad:
مَكْتُوبًا عِنْدَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ يَأْمُرُهُمْ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنْكَرِ {157}
Vile vile Qur’an inaisadikisha Tawrat hii na inatamka kwa lugha yenu, enyi waarabu, ikimuonya na adhabu yule atakayefanya uovu na kumpa habari njema za thawabu yule mwenye kufanya wema. Basi vipi mara mnasema ni uchawi na mara nyingine ni ngano za watu wa kale; mbona hamyasemi hayo kwa Tawrat?
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {13}
أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {14}
وَوَصَّيْنَا الْإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا ۖ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا ۖ وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ۚ حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَبَلَغَ أَرْبَعِينَ سَنَةً قَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَصْلِحْ لِي فِي ذُرِّيَّتِي ۖ إِنِّي تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّي مِنَ الْمُسْلِمِينَ {15}
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ نَتَقَبَّلُ عَنْهُمْ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَنَتَجَاوَزُ عَنْ سَيِّئَاتِهِمْ فِي أَصْحَابِ الْجَنَّةِ ۖ وَعْدَ الصِّدْقِ الَّذِي كَانُوا يُوعَدُونَ {16}