read

Aya 21 -28: Hud

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekitaja kisa cha Hud, katika Juz. 8 (7:65-72), Juz. 12 (11:50 -60), Juz. 19 (26: 123-140) na katika Juzuu nyinginezo zilizopita na zitakazofuatia. Kwa hiyo hapa tutaja kwa ufupi tu, kwa kutegemea yaliyokwishapita.

Na mtaje ndugu wa kina A’di, alipowaonya watu wake kwenye vilima vya mchanga.

Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Hud na watu wake, ili wapate mawaidha na mazingatio. Walikuwa ni waarabu kama watu wako, walikuwa na nguvu zaidi na mali, na nyumba zao zilikuwa karibu na mji wako, kwa vile waliishi kwenye vichuguu vya mchanga – sehemu ya Yemen iliyoshikana na Hijaz; kama ilivyosemekana.

Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake.

Makusudio ya waonyaji ni mitume. Maana ni kuwa waambie ewe Muhammad, kuwa vile vile Hud hakuwa Mtume wa mwanzo wala wa mwisho, bali Mwenyezi Mungu alituma mitume wengi kabla ya Hud na baada yake. Na alikuwa akiwaonya watu wake kwa maneno yale yale ya kila Nabii:

Kuwa msimwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu, ikiwa mtabakia na upotevu na shirki mliyo nayo.

Wakasema: Je, umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

Yaani wewe Hud unataka tuache kuabudu masanamu na tuabudu Mungu mmoja, si ni jambo la ajabu hili! Tena unatuhofisha na adhabu, si utuletee haraka basi ikiwa vitisho vyako ni vya kweli?

Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Mimi ninawafikishia niliyotumwa, lakini ninawaona kuwa nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

Mola wangu ameniamarisha niwaonye na adhabu, basi nikatii amri, nikawaonya. Ama kuwa lini itatokea adhabu hiyo, ni ya aina gani au ikoje, anaiujua Mwenyezi Mungu tu, mimi sijui lolote katika hayo. Isipokuwa nina uhakika kabisa kuwa nyinyi ni watu mliozama kwenye ujinga na upotevu.

Basi walipoliona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili ni la kutunyeshea mvua!

Waliidhania adhabu kuwa ni mawingu, wakafurahi kuwa watanyeshewa mvua, Kwa hiyo wakabashiriana kupata rutuba na mavuno.

Basi Hud akawaambia au hali halisi ikaonyesha:

Kumbe, haya ni hayo mliyoyahimiza, ni upepo ndani yake imo adhabu chungu! Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake.

Wakaona mawingu angani ambayo dhahiri yake ni rehema na undani wake ni adhabu, wakadanganyika na dhahiri na wakaghafilika na yanayojificha yanayokuja ghafla. Basi adhabu ikawanyakua wakiwa wamelewa amani na matamanio. Huu ndio mwisho wa mwenye kuyatii matamanio yake.

Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu amabazo zimekuwa ni makaburi ya miili yao. Mwenye akili ni yule anayepata mawaidha na mfano wa watu hawa, akahofia mashiko ya Mwenyezi Mungu wakati wa nema na raha na akatarajia rehema yake wakati wa shida na karaha.
Hivyo ndivyo tunavyowalipa watu wakosefu duniani na Akhera au Akhera peke yake kulingana na inavyotaka hikima yake.

Na hakika tuliwamakinisha, sio kama tulivyowamakinisha nyinyi.

Tuliwaangamiza akina A’d walipoasi na kupetuka mipaka, na tulikuwa tumewapa nguvu na mali kwa namna ambayo hatukuwapa nyinyi mfano wake enyi vigogo wa kikuraishi. Hivi hamuogopi kuwapata yaliyowapata A’d na wengineo katika uma zilizopita?

Na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo; kama tulivyowapa nyinyi, na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao, kwa sababu hawakunufaika nayo, bali walikuwa kama wendawazimu, viziwi, mabubu na vipofu kwenye ukumbusho na hadhari.

Basi enyi watu wa Makka msighurike na masikio, macho na akili zenu. Kwani yote hayo hayawatafaa kitu itakaposhuka adhabu.

Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yakawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.

Waliipinga haki pamoja na dalili zake na wakaidharau na watu wake. Wakaingia kwenye uovu na upotevu; malipo yao yakawa ni maangamizi na kuvunjika.

Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tuliziainisha Ishara ili wapate kurejea.

Maneno yanaelekezwa kwa washirikina wa Makka. Makusudio ya miji ni watu wa miji hiyo ambao ni akina A’d na Thamud na wanaopakana nao.

Kuzianisha Ishara ni kuwabainishia aina za dalili na mawaidha, na walihadharishwa kwa kauli na vitendo ili wawaidhike na wakome, lakini wakakataa isipokuwa ukafiri, basi ikawathibitikia adhabu na wakabomolewa kabisa.

Basi mbona wale waliowashika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa wawakurubishe, kwa Mwenyezi Mungu, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na hivyo ndio uwongo wao na waliyokuwa wakiyazua.

‘Hivyo’ ni hivyo kutookoa masanamu na kwamba hayamsaidii aliyekuwa akiyaabudu wakati wa dhiki. Maana ni kuwa kauli ya washirikina kuwa sanamu ni muombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu na muokozi wetu, ni uzushi.

وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنْصِتُوا ۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِمْ مُنْذِرِينَ {29}

Na tulipokuletea kundi la majini kusikiliza Qur'an. Basi walipoihudhuria walisema: Nyamazeni! Na ilipomalizwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.

قَالُوا يَا قَوْمَنَا إِنَّا سَمِعْنَا كِتَابًا أُنْزِلَ مِنْ بَعْدِ مُوسَىٰ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهِ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ وَإِلَىٰ طَرِيقٍ مُسْتَقِيمٍ {30}

Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinachoongoza kwenye Haki na kwenye Njia iliyonyooka.

يَا قَوْمَنَا أَجِيبُوا دَاعِيَ اللَّهِ وَآمِنُوا بِهِ يَغْفِرْ لَكُمْ مِنْ ذُنُوبِكُمْ وَيُجِرْكُمْ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ {31}

Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na mumwamini, Mwenyezi Mungu atawasamehe, na atawakinga na adhabu chungu.

وَمَنْ لَا يُجِبْ دَاعِيَ اللَّهِ فَلَيْسَ بِمُعْجِزٍ فِي الْأَرْضِ وَلَيْسَ لَهُ مِنْ دُونِهِ أَوْلِيَاءُ ۚ أُولَٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {32}

Na asiyemwitikia mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hatashinda katika ardhi, wala hatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhahiri.