read

Aya 29 – 32: Majini Wanasikilza Qur’an

Maana.

Na tulipokuletea kundi la majini kusikiliza Qur’an. Basi walipoihudhuria walisema: Nyamazeni! Na ilipomalizwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.

Miongoni mwa wadhifa wa akili ni kuhukumu uwezekeano wa kuweko kitu au kutokuweko. Ikihukumu uwezekano wa kuweko, basi inakimbilia kuthibitisha kuweko kwake kwa kutumia nyenzo, zinazoafikiana na maumbile ya kitu kinachotakiwa kuthibitishwa, kwa hisia na majaribio.

Kikiwa ni katika mambo ya kiakili, basi njia yake itakuwa ni akili. Na kikiwa ni katika mamabo ya ghaibu –sio kuweko Mungu – basi njia yake itakuwa ni wahyi tu. Ukielezea basi itakuwa ni lazima kukubaliana nao.

Hakuna mwenye shaka kwamba akili haikatai kuweko viumbe vilivyo mbali nasi na vinavyotofautiana na tunayoyajua na tuliyoyazoea. Bali tuna uhakika kuwa tusiyoyajua ni mengi zaidi kuliko tunayoyajua; miongoni mwa hayo ni majini. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyataja katika Aya kadhaa; kama vile:

وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ {11}

“Na hakika katika sisi wako wema na wengine katika sisi ni kinyume na hayo.” (72:11).

Mwenyezi Mungu alipeleka kundi katika hao wema kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.), wakamsikia akisoma Qur’an, wakaanza kuambiana: ‘Hebu nyamazeni na mzingatie maana yake.’ Basi wakanyamaza na kusikiliza kwa makini. Wakaona uongofu na nuru, wakamwamini Muhammad (s.a.w.). Mtume alipomaliza kusoma walirudi haraka kwa watu wao kuwaonya na kuwapa bishara ya Uislamu.

Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinachoongoza kwenye Haki na kwenye Njia iliyonyooka

Waliwaambia watu wao kuwa tumesikia Kitabu kutoka kwa Muhammad (s.a.w.) kinachofanana na kile alichoteremshiwa Musa, nacho kinasadikisha yale waliyokuja nayo manabii, ya kuamini tawhid na ufufuo. Vile vile kinaongoza kwenye usawa na kufanya heri:

فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا {1}

يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ ۖ وَلَنْ نُشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا {2}

Wakasema: hakika tumesikia Qur’an ya ajabu. Inaongoza kwenye uwongofu kwa hiyo tumeiamini na hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.” (72:1-2).

Ikiwa sisi hatujawaona majini walioathirika na Qur’an na kuiamini, lakini tumewaona wataalamau na watu wenye akili wengi wakiathirika na matamshi ya Qur’an kwa kiasi cha kusikia matamshi yake tu; tena wakaamini imani isiyokuwa na shaka kuwa inatoka kwa Mwenye hekima Mjuzi.

Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na mumwamini, Mwenyezi Mungu atawasamehe, na atawakinga na adhabu chungu.
Itikieni mwito wa haki na mumfuate anayeutoa mwito huo; Mwenyezi Mungu atawasamehe dhambi zenu na atawaingiza katika rehema yake na kuwaokoa na ghadhabu yake na adhabu yake.

Na asiyemwitikia mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hatashinda katika ardhi, wala hatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhahiri.

Hakuna kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa kwake tu wala hakuna kuokoka na adhabu yake isipokuwa kwa ikhlasi na matendo mema.

Hao wamo katika upotevu ulio dhahiri.

‘Hao’ ni hao wasioitikia mwito wa Mwenyezi Mungu, na asiyemwitikia atakuwa ameiacha njia ya haki na uongofu.

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَنْ يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ۚ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {33}

Je, hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliyeziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwa nini? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَلَيْسَ هَٰذَا بِالْحَقِّ ۖ قَالُوا بَلَىٰ وَرَبِّنَا ۚ قَالَ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْفُرُونَ {34}

Na siku makafiri watakapoonyeshwa Moto, Je, haya si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyokuwa mkikataa.

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ وَلَا تَسْتَعْجِلْ لَهُمْ ۚ كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِنْ نَهَارٍ ۚ بَلَاغٌ ۚ فَهَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الْفَاسِقُونَ{35}

Basi subiri, kama walivyosubiri Mitume wenye azma, Wala usiwahimizie. Siku watakayoyaona waliyoahidiwa, itakuwa kama kwamba hawakukaa ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa isipokuwa walio watu mafasiki?