read

Aya 33 – 35: Je, Haya Si Kweli?

Maana

Je, hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliyeziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwa nini? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

Ulimwengu huu wa ajabu unajulisha uweza wa muumba na ukuu wake. Vile vile unajulisha, tena kwa njia bora, kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ana uwezo wa kuwafufa wafu. Kwa vile sabu inayoleta mambo hayo mawili ni moja, ambayo ni uweza wa mwenye kukiambia kitu ‘kuwa’ na kikawa. Imam Ali (as) anasema: “Namshangaa anayekanusha ufufuo wa pili na hali anaona ufufuo wa kwanza!”

Maana ya Aya hii yametangulia katika makumi ya Aya na yatakuja mengine mengi; miongoni mwayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, tulichoka kwa umbo la kwanza?” (50:15). Basi tutachoka vipi na umbo la pili?

Na siku makafiri watakapoonyeshwa Moto, yaani watakapoadhibiwa na kuaambiwa: Je, haya, mliyokuwa mkiyakanusha hapo mwanzo, si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu! ni kweli.
Walikanusha duniani ambapo kunawadhuru kukana na wamekubali Akhera ambapo hakuwanufaishi chochote kukiri kwao.

Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu mlikuwa mkikataa; bali mliwadharau wale walioamini hisabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Na ungeliona watakaposimamishwa mbele ya Mola wao, Akasema: Je, si kweli haya? Watasema: Kwa nini? Tunaapa kwa Mola wetu. Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakataa.” Juz. 7 (6:30).

Basi subiri, kama walivyosubiri Mitume wenye azma,

Kwenye tafsiri nyingi imeelezwa kuwa mitume wenye azma (Ululu-azm) ni watano: Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Muhammad. Kila mmoja wao alikuwa na sharia mahususi aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu kutumiwa na viumbe wote wakati wake mpaka afike mtume mwingine kati ya hao watano.

Akija anafuta sharia ya yule aliyemtangulia katika wale watano, mpaka kufikia sharia ya Muhammad (s.a.w.), Bwana wa mitume na mwisho wa manabii. Hiyo haiwezi kufutwa hadi siku ya kiyama. Ama manabii wengine wasiokuwa hao ululu-azm, walikuwa wakitumia sharia ya waliyemtangulia katika hao watano.

Kuna riwaya za Ahlul-bayt zinazozungumzia hili na kuashirwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

شَرَعَ لَكُمْ مِنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ {13}

“Amewapa sharia ya Dini aliyomuusia Nuhu na tuliyokupa wahyi wewe, na tuliyowausia Ibrahim na Musa na Isa,” Juz. 25 (42:13)

Ambapo amewahusu kuwataja hao watano na kutaja neno sharia. Na ‘wewe’ ni wewe Muhammad.

Wala usiwahimizie adhabu. Siku watakayoyaona waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa ulimwenguni ila saa moja ya mchana.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.), na wanaoambiwa ni wale walioikanusha risala yake. Makusudio ya yale mliyoahidiwa ni adhabu ya Jahannam. Maana ni kuwa usifanye haraka ewe Muhammad (s.a.w.) ya kutaka wale waliokufuru waadhibiwe, kwa sababu itawapata tu huko Akhera. Huku kukaa kwao duniani hata kukirefuka, lakini watapoiona adhabu wataona kama kwamba ni kitambo kidogo tu.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ {197}


“Ni
starehe ndogo. Kisha makazi yao ni Jahannam ni mahali pabaya pa kushukia.”
Juz. 4 (3:197).

Imam Ali (as) anasema: “Hakika dunia ni starehe za siku kidogo, zinaondoka kama yanavyoondoka mangati au kama yanavyopotea mawingu.”

Huu ndio ufikisho!

Yaani Qur’an ni ufikisho wa risala za Mwenyezi Mungu Mtukufu, nayo ni hoja tosha ya mawaidha yake na ni ponyo kwa anayetaka mwongozo na uongofu.

Kwani huangamizwa wengine isipokuwa walio watu mafasiki?

Hapana!

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ {51}

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ {52}

“Hakika wenye takua watakuwa katika mahali pa amani. Katika mabustani na chemchem.”
Juz. (44:51-52)