Aya 7 – 14: Mkimnusuru Mwenyezi Mungu Atawanusuru
Maana
Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atawanusuru ataithibitisha miguu yenu.
Kuithibitisha miguu ni kinaya cha uimara. Aya hii ni dalili wazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) yuko pamoja na watu wa haki na uadilifu; anawasaidia na kuwashika mkono. Maana ya Aya hii yako kwenye Aya nyingi; kama vile:
فَإِنَّ حِزْبَ اللَّهِ هُمُ الْغَالِبُونَ {56}
إِنَّ اللَّهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوْا وَالَّذِينَ هُمْ مُحْسِنُونَ {128}
إِنَّ اللَّهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا ۗ {38}
وَلَيَنْصُرَنَّ اللَّهُ مَنْ يَنْصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ {40}
Nusra inayotoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) iko namna nyingi; miongoni mwazo ni hizi zifutazo:
• Kuwashinda maadui kwa vita na nguvu ya silaha; kama alivyowashinda Mtume wa Mwenyezi Mungu vigogo wa kikuraishi na dhulma yao na wengineo.
• Kushinda kwa adhabu itokayo mbinguni; kama vile kimbunga tufani n.k.
• Kushinda kwa nguvu ya hoja na dalili katika mijadala.
• Kushinda kwa shani na utajo wa kudumu duniani.
• Nusra ya Akhera siku ile zitakosawijika nyuso.
وَتَرَى الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ {49}
Kwa vile katika Aya tuliyo nayo nusra haikufungwa na sifa ya aina yoyote, basi inatubainikia kuwa makusudio ya nusura katika Aya hii ni nusra yoyote. Hakuna mwenye shaka kuwa itakuwa tu, hata kama ni huko Akhera kusiko na shaka. Kwa hiyo basi hakuna nafasi ya kutaaradhi au kuuliza kuwa vipi Mwenyezi Mungu amewaahidi wenye haki nusra yake, lakini historia imejaa dhulma na ujeuri waaliofanyiwa wema na wenye ikhlasi.
Yametangulia maelezo kuhusu maudhui haya katika Juz. 17 (22:38) kifungu cha “Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini.”
Dola Ya Kiislamu
Kwa mnasaba wa Aya hii tutadokeza yafuatayo: Kuna vikundi siku hizi vinadai kusimamisha dola ya Kiislamu. Ni mwislamu gani leo, mwenye ikhlasi ya Mwenyezi Mungu anayekataa Uislamu uwe na serkali yake inayotekeleza hukumu za Qur’an na waislamu wawe na umoja utakaowaokoa na utengano?
Lakini tujiulize: Je, dola hii itapatikana kwa kiasi tu cha kusimamisha bendera na kuinua nembo? Au kwa kuweko vilemba vingi kwenye vichwa vya wajinga na wenye undani?
Je, inawezekana kuwaunganisha Waislamu milioni 700 walioenea mashariki na magharibi mwa ardhi huku wakiwa na makabila, madhehebu na siasa mbalimbali; hawa wameukumbatia ujamaa, wale ubepari na wengine wakiwa na siasa zisizofungamana na upande wowote?
Kama itapatikana dola hiyo ya waarabu au wasiokuwa waarabu je, itaweza kukabili majukumu yake na kutatua matatizo ya waislamu katika nchi nyingine. Kisha je, dola hii ni ya kisunni au kishia au ya wote wawili?
Majibu ya maswali haya tuwachie wataalamu wenye ikhlasi.1
Hakika waislamu wamepatwa na udhalili mwingi na kushindwa. Kule kushindwa mnamo tarehe 5 June inatosha kuwa ni udhalili na utwevu. Sababu ya kwanza na ya mwisho ya kushindwa huko ni utengano. Dawa pekee ya hilo ni maarufu kwa wote – kusimama safu moja dhidi ya maadui wenye ushirikiano waliojipanga na kujitokeza kwenye vita vya mwezi June.
Mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na akataka kuwanasihi waislamu kwa ukweli kabisa basi na afanye juhudi zake zote kwa ajili ya kuwasaidia waislamu kujikomboa na nguvu ya ufisadi ya ndani na nje.
Wakishajikomboa na kuwa na uhuru kamili, hapo ndipo wenye ikhlasi wanaweza kufikiria serikali ya kiislamu au nyingine yenye kuridhiwa na Mwenyezi Mungu na yenye masilahi kwa waislamu.
Ishara yetu hii inatiliwa nguvu na kauli ya Imam Ali (as): “Hakika uzushi wenye kutatiza ni maangamizi ... na katika utawala wa Mungu kuna hifadhi ya mambo yenu basi upeni utiifu wenu au Mwenyezi Mungu atawaondolea utawala wa kiislamu.”
Ikiwa utawala wa kiisalamu uliwaondokea wahenga kwa sababu ya utengano wao, je utaweza kuturudia sisi tuliotengana zaidi. Unaweza kuuliza: Je, ni kweli yanayosemwa kuwa chimbuko la fikra ya dola ya kiislamu ni uzayuni ili kuitakasa dola yake ya kidini na ya kibaguzi? Ili waweze kusema kuwa hata waislamu nao pia wanataka dola ya kidini?
Jibu: Hakika dini ya kiyahudi ni dini ya uadui wa maisha na ubinadamu. Kwa sababu, katika itikadi yao, Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kikabila, hajishughulishi na walimwengu wengine wote isipokuwa Israil peke yake, na kwamba watu wengine wote wameumbwa kuwatumikia wao; kama ilivyoelezwa katika kitabu Alkanzul marsud cha Dkt. Yussuf Hanna Naasrullah na kitabu Albaqau lilyahud cha mzayuni Rose Marine.
Ama Uislamu ni dini ya maisha, huruma na ubaindamu kwa ujumla. Hakuna kitu kinachofahamisha hivyo zaidi kuliko Aya na Hadithi zinazotangaza waziwazi kuwa uislamu unaongoza kwenye usawa zaidi na kwamba unatilia mkazo kwenye akili na maumbile na ni wajibu kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume, kwa sababu ni mwito wa maisha bora.
Maana ni kuwa Uislamu ni dini ya kilimwengu ya kiakili; yaani unajishughulisha na mtu kama mtu wa namna yeyote, hata kama ni myahudi, kwa sharti ya kutomfanyia uadui nduguye mtu.
Sasa haya ni wapi kwa wapi na dini ya Mayahudi waliojiita taifa teule la Mwenyezi Mungu?
Na waliokufuru, basi kwao ni maangamizo, hawataona isipokuwa hizaya na maangamizi na atavipoteza vitendo vyao, haitawarudia heri yoyote.
Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
Walimchukia Mtume (s.a.w.) na Qur’an si kwa lolote ila ni kwa vile aliwatakia haki na wao wanaichukia, basi wakawa ni wenye hasara. Kupotea na kuanguka kuna maana moja, nako ni kupotea na kutofaa amali. Mwenyezi Mungu amekariri ili kuashiria kuwa kuikufuru Qur’an na kuichukia ni kupotea amali.
Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa waliokuwa kabla yao?
Jinsi washirikina walivyokadhibisha risala ya Muhammad (s.a.w.), huku wakiona athari ya waliopita na wakisikia kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu walipowakadhibisha mitume?
Aya hii imetangulia kwa herufi zake katika Aya kadhaa.
Mwenyezi Mungu aliwaangamiza wao, watoto wao, wake zao na mali zao.
Na kwa makafiri hawa itakuwa mfano wa hayo.
Hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa mataghuti ni moja – ikiwa atawaangamiza wa mwanzo kwa sababu ya uasi wao, basi wengine pia atawaangamiza kwa sababu hiyo hiyo.
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walioamini. Na makafiri hawana mlinzi.
‘Hayo’ ni hayo ya kuangamizwa. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaangamiza makafiri wakiwa hawana wa kuwasaidia, lakini waumini, msimamizi wao ni Mwenyezi Mungu, akiwakinga na kuwaaneemesha.
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza ambao wameamini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake.
Maana yako wazi na imekwishatangulia katika Aya kadhaa huko nyuma.
Na ambao wamekufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makazi yao.
Wao ni sawa na wanyama, wanakula tu na wala hawafikirii chochote. Kwa hiyo mwisho wao ni Jahannam makazi mabaya kabisa.
Imam Ali (as) anasema: “Mimi sikuumbwa ili nijishughulishe na kula vizuri. kama mnyama aliyefungwa ambaye hamu yake ni lishe yake tu, au asiyefungwa ambaye shughuli yake kuu ni kuchakura majaa kwa ajili ya lishe yake na kucheza nayo anavyotaka.”
Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu uliokutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa na wa kuwanusuru.
Hili ni karipio kwa wale waliopanga njama za kumuua Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), akalazimika kuuhama mji wake wa Makka na kuelekea Madina. Tazama Juz. 9 (8:30).
Katika Tafsir Attabariy, imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Mtume alipotaka kuutoka mji wa Makka alisema: ‘’Wewe ni mji wa Mwenyezi Mungu unaopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Na wewe ni mji wa Mwenyezi Mungu unaopendeza zaidi kwangu. Lau sikuwa washirikina wamenitoa nisingelikutoka.’’ Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akateremsha Aya hii.
Je, mwenye kuwa na dalili kutoka kwa Mola wake ni kama aliyepambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata hawaa zao?
Yule mwenye kuichukua haki kutoka katika chimbuko lake na akawa na busara, hayuko sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na yule anayeipima haki kwa hawaa yake na malengo yake, huku akijiona kuwa yeye ndiye mtu mwenye matendo mema zaidi kuliko wengine.
مَثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ فِيهَا أَنْهَارٌ مِنْ مَاءٍ غَيْرِ آسِنٍ وَأَنْهَارٌ مِنْ لَبَنٍ لَمْ يَتَغَيَّرْ طَعْمُهُ وَأَنْهَارٌ مِنْ خَمْرٍ لَذَّةٍ لِلشَّارِبِينَ وَأَنْهَارٌ مِنْ عَسَلٍ مُصَفًّى ۖ وَلَهُمْ فِيهَا مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَمَغْفِرَةٌ مِنْ رَبِّهِمْ ۖ كَمَنْ هُوَ خَالِدٌ فِي النَّارِ وَسُقُوا مَاءً حَمِيمًا فَقَطَّعَ أَمْعَاءَهُمْ {15}
وَمِنْهُمْ مَنْ يَسْتَمِعُ إِلَيْكَ حَتَّىٰ إِذَا خَرَجُوا مِنْ عِنْدِكَ قَالُوا لِلَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مَاذَا قَالَ آنِفًا ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ {16}
وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ {17}
فَهَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَنْ تَأْتِيَهُمْ بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ {18}
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنْبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ {19}
- 1. Ikumbukwe mwandishi aliandika katika miaka ya 1970