Aya 15 – 19: Sifa Za Pepo
Maana
Mfano wa Pepo waliyoahidiwa wenye takuwa ina mito ya maji yasiyoharibika.
Makusudio ya mfano wa pepo ni sifa zake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawapa habari waja wake kwamba miongoni mwa sifa za pepo ni kuwa ndani yake mna mito ya maji yanayobaki na asili yake bila ya kubadilishwa na chochote.
Na mito ya maziwa isiyoharibika ladha yake wala rangi au harufu yake. Na mito ya mvinyo yenye utamu kwa wanywao. Ni tamu mdomoni wala hauleweshi. Na mito ya asali iliyosafishwa kutokana na masega na mengineyo. Na wao humo watakuwa na kila namna ya matunda yakiwemo yale ambayo hayana mfano wake duniani.
Katika baadhi ya vitabu vya kisufi imeandikwa kuwa Makusudio ya maji hapa ni ilimu, maziwa ni matendo, mvinyo ni mahaba na asali ni utamu wa maarifa na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.
Tumekwishatangulia kusema mara nyingi kwamba kila kinachokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu inapasa kukichukulia kwa dhahiri yake mpaka ithibitike kinyume kutokana na nakili au akili. Hapa akili haikatai chochote katika sifa za pepo zilizotajwa. Kwa hiyo basi ni wajibu kuchukulia dhahiri yake na kubaki hivyo hivyo.
Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja mara kadhaa katika Kitabu chake kuwa watu wa Peponi watastarehe kwa ladha za kimaana, sio za kihisia; kama vile Kupendwa na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu na kuinuliwa daraja zao kwake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِنْدَ مَلِيكٍ مُقْتَدِرٍ {55}
Na kauli yake:
سَيَجْعَلُ لَهُمُ الرَّحْمَٰنُ وُدًّا {96}
Sasa je, kuna wajihi gani wa kuchanganya Aya zile zinazofahamisha neema ya Peponi inayokuwa kwa ladha za kihisia na zile zinazofahamisha ladha ya kimaana?
Jibu: hakuna kizuizi cha kuzuia kuchanganya zote mbili na kutumia ufahamisho wote. Kwa hiyo watu wa Peponi watastarehe kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kuinuliwa daraja zao mbele yake; vile vile watastarehe na vitu vizuri katika vyakula na vinywaji.
Mula Sadra anasema katika Asfar: “Ama Pepo iko kama ilivyojulishwa na Kitabu na sunna kwa kufuatana na dalili. Ndani yake hamtakuwa na mauti wala uzee, ghamu au maradhi. Hakuna kuisha wala kuondoka.
Ni nyumba ya cheo na utukufu. Wakazi wake hawatapata tabu wala kuchoka. Humo watapata kila kinachotamaniwa na nafsi na kuburudisha macho na watadumu humo.
“Wakazi wake watakua karibu na Mwenyezi Mungu, ni mawalii wake ni wapenzi wake na ni watu wa karama yake. Na kwamba wao watakuwa na daraja bora; miongoni mwao kuna watakaostarehe kwa tasbih na takbir, na wengine watastarehe kwa ladha za hisia; kama vile aina ya vyakula, vinywaji na matunda. Pia makochi, mahurilaini na kutumikiwa na vijana. Vile vile kukaa kwenye mito na mazulia na kuvaa hariri nyepesi na nzito. Kila mmoja ataburudika kulingana na hamu yake.”
Na maghufira kutoka kwa Mola wao.
Wale wanaostarehe na anasa za dunia huko watahisabiwa hisabu nzito: Ama watu wa Peponi wao watakuwa kwenye neema wakiwa kwenye amani ya hisabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Basi je hao ni kama watakaodumu Motoni?
Hapa kuna maneno ya kukadiriwa yanayofahamika kutokana na mfumo wa maneno; kukadiriwa kwake ni je, atakayedumu Peponi ni sawa na atakayedumu Motoni? Hapana hawalingani sawa.
Na wakinyweshwa maji yanayochemka yatakayokata matumbo yao.
Vipi watakuwa sawa na hali watu wa Peponi watakunywa maji matamu, maziwa, mvinyo na asali safi; na watu wa motoni watakunywa usaha na maji moto yanayotokota matumboni?
Na wapo miongoni mwao wanaokusikiliza, mpaka wakiondoka kwako huwauliza waliopewa ilimu: Amesema nini sasa hivi?
Yaani miongoni mwa watu wanaokusikiliza wewe Muhammad wako makafiri au wanafiki na wanapotoka wanasema kwa dharau kuwaambia wale waliohudhuria katika maulama wa watu wa kitabu: ati amesemaje huyo sasa hivi? Sisi hatukufahamu. Je nyinyi mmefahamu kitu? Hii ndio tabia ya yule asiyeona chochote isipokuwa matamanio yake tu.
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, na wakafuata hawa zao.
Kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): ‘Na wakafuata matamanio yao,’ inaashiria jawabu la swali; Kwanini Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao? Ndio majibu yakawa, kwa vile hawa zao zimememea kwenye nyoyo zao mpaka ikawa kama kwamba Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu yake au amewaumba bila ya nyoyo; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُمْ ۚ {5}
Na ambao wameongoka anawazidishia uongofu.
Waumini waliutafuta uongofu kwa ukweli na ikhlas, kwa hiyo Mwenyezi Mungu amekuwa ndio muongozi na mlezi wao; akawazidishia elimu ya heri na akawapa ulinzi wake na tawfiki yake kwenye yale yaliyo na heri ya dunia yao na Akhera yao. Haya ndiyo Makusudio ya na anawapa takua yao.
Kwani wanangojea jengine isipokuwa iwafikie Saa ya Kiyama kwa ghafla?
Wanaambiwa wale waliosema kwa dharau: Ati amsema nini sasa hivi? Walisema hivi wakiwa wameghafilika kabisa na siku ambayo itawanyakuwa ghafla na wasimame mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu.
Basi sharti zake zimekwisha kuja.
Makusudio ya sharti hapa ni dalili na hoja mkataa za ufufuo. Zimekuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mdomoni mwa Muhammad (s.a.w.) kwa mifumo mbalimbali wala hazikuacha udhuru wowote kwa mkanushaji.
Na itapowajia kutawafaa wapi kukumbuka kwao?
Maana ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwakumbusha duniani, lakini wakakataa, na watakapofufuliwa na kuona adhabu watakumbuka na kujuta, lakini wakati huo hakutafaa chochote kukumbuka kwao.
Basi jua ya kwamba hapana Mola ila Mwenyezi Mungu Yeye anahuisha na kufisha na kuadhibu na kutoa adhabu. Sio mbali kuwa maana ya hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu hapa, ni lingania Mwenyezi Mungu na umoja wake.
Na omba maghufira kwa dhambi zako na za waumini wanaume na waumini wanawake.
Kuomba maghufira kwa dhambi ni jambo linalopendeza kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni jambo linalotakina hasa; ni sawa kuweko na dhambi au la.
Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi matendo ya duniani na mahali penu pa kukaa mtakapoacha matendo yenu au kwenda zenu Akhera; kama ilivyosemekana.
Vyovyote iwavyo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua hali ya waja wake duniani na Akhera na pale wanapokuwa katika harakati na wanapotulia.
وَيَقُولُ الَّذِينَ آمَنُوا لَوْلَا نُزِّلَتْ سُورَةٌ ۖ فَإِذَا أُنْزِلَتْ سُورَةٌ مُحْكَمَةٌ وَذُكِرَ فِيهَا الْقِتَالُ ۙ رَأَيْتَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ يَنْظُرُونَ إِلَيْكَ نَظَرَ الْمَغْشِيِّ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَأَوْلَىٰ لَهُمْ {20}
طَاعَةٌ وَقَوْلٌ مَعْرُوفٌ ۚ فَإِذَا عَزَمَ الْأَمْرُ فَلَوْ صَدَقُوا اللَّهَ لَكَانَ خَيْرًا لَهُمْ {21}
فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ تَوَلَّيْتُمْ أَنْ تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ {22}
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ {23}