read

Aya 20 – 23: Utiifu Na Kauli Njema

Maana

Na wanasema wale ambao wameamini: Kwa nini haiteremshwi Sura?’ Na inapoteremshwa Sura iliyo waziwazi na vikatajwa ndani yake vita, utawaona wenye maradhi katika nyoyo zao wanakutazama mtazamo wa anayezimia kwa mauti.

Hapa kuna kukadiria maneno kuwa: Kwa nini haiteremshwi sura ya vita? Dalili ya kukadiria huku ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na vikatajwa ndani yake vita.’ Hali hii watu wa nahw wanaiita ufahamisho unaofahamishwa na wa pili. Iliyo waziwazi ni kutaja vita waziwazi. Maradhi hapa ni shaka na unafiki.

Maana ni kuwa waumini wenye ikhlasi walikuwa wakitamani Qur’an iwaamrishe jihadi ya kupigana na makafiri na waovu. Wanapoitwa walikuwa wakienda haraka kujitolea nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, huku wakiwa na furaha ya kukutana na Mwenyezi Mungu na thawabu zake.
Ama wale walio na maradhi nyoyoni mwao ambao ni wanafiki, walikuwa wakichukia sana jihadi na vita, na inapoteremshwa Aya ya vita basi mishipa inawasimama kwa hofu wakimwangalia Mtume kwa mtazamo wa hofu, kama anayeangalia mauti yakimjia.

Basi ole wao.

Wafasiri wengi wamesema maana ya neno Awla hapa ni ‘ole wao’ ambalo pia lina maana ya bora. Mfumo wa maneno unakubaliana na maana hii ya ole wao.

Utiifu na kauli njema.

Haya ni maneno yanayoanza tena. Maana yake ni kuwa kumtii Mwenyezi Mungu na kauli njema atakayoikubali Mtume ni bora kwao kuliko kukijaza kifua na unafiki na kumtazama Mtume kwa jicho la chuki na hofu.

Na jambo likishaazimiwa, basi wakiwa ni wakweli kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka itakuwa ni heri kwao.

Lau wanafiki wangelimfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na wakaitikia mwito wa Mtume inapokuja amri ya vita na ikawa ni lazima, ingelikuwa ni heri ya dunia yao na Akhera yao. Lakini walikataa isipokuwa ufisadi.

Basi yanayotarajiwa kwenu mkitawala ndio mtafanya ufisadi katika nchi na mtaukata udugu wenu?

Nyinyi wanafiki mmedhihirisha Uislamu kwa kujilazimisha na kuogopa nguvu yake. Huenda mkipata nguvu na utawala mtaijaza ardhi ufisadi kwa ibada ya masanamu na kumwaga damu, kupora mali na kuvunja udugu.

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kuwaweka mbali na rehema, na akawatia uziwi, na akawapofoa macho yao.

Walipoutilia uziwi mwito wa haki na kuufumbia macho ndio Mwenyezi Mungu naye akawatia uziwi na kuwapofua. Kwa maneno mengine ni kuwa walifuata njia ya maangamizi kwa hiyari yao ndio Mwenyezi Mungu akawaangamiza:

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِنْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ۖ{101}

“Na hatukuwadhulumu, lakini wamejidhulumu wenyewe” Juz. 12 (11:101).

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا {24}

Je, Hawaizingatii hii Qur’an? Au kwenye nyoyo zipo kufuli?

إِنَّ الَّذِينَ ارْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِهِمْ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَى ۙ الشَّيْطَانُ سَوَّلَ لَهُمْ وَأَمْلَىٰ لَهُمْ {25}

Kwa hakika ambao wanarudi kwa migongo yao baada ya kuawabainikia uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewachelewesha.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لِلَّذِينَ كَرِهُوا مَا نَزَّلَ اللَّهُ سَنُطِيعُكُمْ فِي بَعْضِ الْأَمْرِ ۖ وَاللَّهُ يَعْلَمُ إِسْرَارَهُمْ {26}

Hayo ni kwa sababu waliwaambia waliochukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu: Tutawatii katika baadhi ya mambo. Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.

فَكَيْفَ إِذَا تَوَفَّتْهُمُ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ {27}

Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao!

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ {28}

Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha. Basi akaviangusha vitendo vyao.

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ أَنْ لَنْ يُخْرِجَ اللَّهُ أَضْغَانَهُمْ {29}

Je, ambao wana maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?

وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُمْ بِسِيمَاهُمْ ۚ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ ۚ وَاللَّهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ {30}

Na lau tungelipenda, tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao. Na bila ya shaka utawajua kwa namna ya usemi Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنْكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ {31}

Na bila ya shaka tutawajribu mpaka tuwajue wapignao jihadi katika nyinyi na wanaosubiri. Nasi tutazijaribu habari zenu.