Aya 24 – 31:Je Hawaizingati Qur’an?
Maana
Je, Hawaizingatii hii Qur’an? Au kwenye nyoyo zipo kufuli?
Wanaambiwa wanafiki. Kwa sababu Aya hii na ilie iliyo kabla yake inawazungumzia wao. Dalili zote zilizokuja katika Qur’an, za kuweko Mwenyezi Mungu katika kuumbwa mbingu na ardhi, hoja wazi za utume wa Muhammad (s.a.w.).
Ubaya wa shirki, dhulma na ufisadi katika ardhi, yote hayo yako wazi hayakufumbwafumbwa; kuongezea athari ya mfumo wa Qur’an katika moyo wa msomaji na msikilizaji anavyopata hisia. Basi makafiri wananini hawaathiriki na muujiza huu? Je, wamekosa usikizi na macho au nyoyo zao zimefungwa na kufuli na kutu.
Kwa hakika ambao wanarudi kwa migongo yao baada ya kuawabainikia uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewachelewesha.
Neno kurudi tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu Irtaddu (kurtadi) lenye maana ya kuamini haki kisha kuikanusha. Pia kuijua haki kwa dalili mkataa kisha kuikanusha kwa matamanio ya nafsi, kunaingia katika hukumu ya kuritadi, kwa sababu kuijua haki ni sawa na kuiamini na kuichukia ni sawa na kuiritadi.
Ama mwenye kuficha ukafiri na akadhihirisha imani huyo ni mnafiki na murtadi vile vile. Ni mnafiki kwa vile amedhihirisha kinyume na yaliyo moyoni mwake na ni murtadi kwa kuwa duniani anakuwa kama mumin na Akhera anakuwa kafiri; kama kwamba yeye ni mumin na wakati huo huo ni murtadi.
Tamko la Aya limegusia aina zote tatu. Kwa sababu dalili za dhahiri zilizosimaia kwenye Tawhid, ufufuo na utume wa Muhammad (s.a.w.) ndio hoja aliyoikusuduia Mwenyezi Mungu kwa kusema: ‘Baada ya kuwabainikia uongofu,’ lakini shetani aliwadanganya kwa unafiki na kuiritadi haki na kuipinga. Akawaahidi ahadi ya uwongo na kuwatia wasiwasi wa tamaa na matamanio.
Hayo ni kwa sababu waliwaambia waliochukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu: Tutawatii katika baadhi ya mambo.
Waliosema ni wanafiki na waliochukia ni mayahudi waliokuwa majirani wa Mtume. Kwa sababu mayahudi ndio watu wanaochukia zaidi kila kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu; hasa Qur’an. Maana ni kuwa wanafiki waliwambia mayahudi: sisi tuko pamoja na nyinyi kuhusu Muhammad na tunashirikiana nanyi katika kumpiga vita; isipokuwa hali haituruhusu kutangaza uadui wetu kwake. Kwa hiyo tuacheni tujionyeshe kuwa ni waislamu na tutakuwa pamoja nanyi kwenye njama dhidi yake.
Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.
Yaani siri za mayahudi na za wanafiki, kwa sababu kwake hakifichiki chochote katika ardhi wala mbinguni.
Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao!
Wamekimbia jihadi kwa kuogopa mauti, je wataweza kuyakimbia mauti na mapigo yake? Na ufufuo na vituko vyake.
Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaadhibu wakati wa mauti na baada yake vile vile, kwa vile waliathirika na yale yanayomchukiza Mwenyezi Mungu kuliko yale yanayomridhisha.
Basi akaviangusha vitendo vyao, havitawafaa kitu.
Je, ambao wana maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?
Wanafiki walificha chuki na uadui kwa Mtume na maswahaba; wakawadhihirishia upendo na utii; wakadhani kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hatadhihirisha wanayoyaficha vifuani mwao.
Na lau tungelipenda tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao.
Kukuonyesha ni kukutambulisha na kutambua ni kuwatambua kwa alama zao. Lengo la kugawanya huku kunakofanana na kukaririka ni kusisitiza kuwa Mtume hapitwi na kitu anachofahamishwa na Mwenyezi Mungu. Lakini asiyekuwa Mtume anaweza kukosea katika kufahamu kwake.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa ilishuka kabla ya Mtume kuwafahamu wanafiki, kutokana na neno ‘lau,’ lakini Mtume (s.a.w.) aliwatambua baadae kutoka na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na bila ya shaka utawajua kwa namna ya usemi wao.
Namna ya usemi ni kule kumaanisha kwake; kama vile udhuru wa uwongo waliokuwa wakiutoa wanafiki na jinsi wanavyowalaumu watu wema na kuwasifu washari na mengineyo yanayojiachia mdomoni yanayaofahamisha ria na unafiki.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Anas: “Hakufichika mnafiki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), baada ya Aya hii.” Vile vile Nabii (s.a.w.) alikuwa akiwajuwa wanafiki kwa vitendo vyao. Walikuwa wakiikimbia jihadi na wakiona uzito kujitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.
Hili ni kemeo kwa kila anayedhihirisha heri na kuficha shari.
Na bila ya shaka tutawajaribu mpaka tuwajue wapignao jihadi katika nyinyi na wanaosubiri. Nasi tutazijaribu habari zenu.
Mwenyezi Mungu anawajua wanaopigana jihadi na walio na subira kabla ya kuwafanyia majaribio, lakini anafanya hivi kwa kuamrisha na kukataza ili amdhihirishe na amtambulishe muovu na mwema kwa vitendo ambavyo vinastahiki adhabu au thawabu.
Imeelezwa katika Nahjul-balagha: “Mwenyezi Mungu anataka mumnusuru na hali yeye ana majeshi ya mbinguni na ardhini na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima. Na anataka mukopeshe na Yeye ana hazina za mbingu na ardhi na Mwenye kujitosha Mwenye kusifiwa…Anataka kuwajaribu ninani wenu mwenye matendo mema zaidi.
Basi harakisheni matendo yenu mtakuwa jirani na Mwenyezi Mungu.”
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ وَشَاقُّوا الرَّسُولَ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَىٰ لَنْ يَضُرُّوا اللَّهَ شَيْئًا وَسَيُحْبِطُ أَعْمَالَهُمْ {32}
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ {33}
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ثُمَّ مَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَنْ يَغْفِرَ اللَّهُ لَهُمْ{34}
فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَنْ يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ {35}
إِنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۚ وَإِنْ تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا يُؤْتِكُمْ أُجُورَكُمْ وَلَا يَسْأَلْكُمْ أَمْوَالَكُمْ {36}
إِنْ يَسْأَلْكُمُوهَا فَيُحْفِكُمْ تَبْخَلُوا وَيُخْرِجْ أَضْغَانَكُمْ {37}
هَا أَنْتُمْ هَٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنْفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَمِنْكُمْ مَنْ يَبْخَلُ ۖ وَمَنْ يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَنْ نَفْسِهِ ۚ وَاللَّهُ الْغَنِيُّ وَأَنْتُمُ الْفُقَرَاءُ ۚ وَإِنْ تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُمْ {38}