read

Aya 32 – 38: Msibatilishe Amali Zenu

Maana

Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wakakinzana na Mtume baada ya kuwabainikia uwongofu, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote, na ataviangusha vitendo vyao.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alilingania kwenye Uislamu kwa dalili na ubainifu; wakakaukataa watu wa masilahi na wakawazuia watu wasiukubali Uislamu kwa kutumia nguvu, mali na propaganda za uwongo.

Lakini Mwenyezi Mungu alimpa nguvu Mtume wake, akaidhihirisha dini yake na akaviangusha vitendo vya wahaini.

Hadi leo Uislamu na waislamu wanakabiliana sana na nguvu za shari. Zilizo hatari zaidi ni baadhi ya dola zinazobeba jina la Uislamu huku zikishirikiana na adui mkubwa zaidi, mkoloni wa kizayuni. Umefika wakati, sasa, waislamu waondoe vumbi la chuki na mfarakano ili waweze kuungana pamoja dhidi ya adui yao mwenye ushirikiano na wenzake.

Enyi ambao mmeamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume; yaani fanyeni mambo kwa imani yenu.

Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Mtiini Mwenyezi Mungu,’ baada ya kusema: ‘Enyi ambao mmeamini,’ ni sawa na kauli yake:

فَمَنْ كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا{110}

“Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake basi naatende matendo mema.” Juz. 16: (18:110).

Wala msiviharibu vitendo vyenu kwa shirki na unafiki wala kwa masimbulizi na udhia au kwa maovu ambayo huondoa mema. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

 إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ {27}

“Hakika Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu.” Juz. 6 (5:27).

Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu hakubali matendo ila kwatakua.” Imam Ali (as) anasema: “Kwenye matendo, kuweni ni wenye kujishughulisha zaidi na kukubaliwa matendo.”

Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria huko Akhera. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawafufua watu kulingana na walioyofia na atawahisabu kulingana na walivyomaliza uhai wao kwenye ukafiri au imani.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:161) na Juz. 3 (3:91).

Qur’an Na Siasa Ya Vita

Basi msilegee na kuita kwenye suluhu.

Matukio yamethibitisha kwamba mwenye kulegea mbele ya adui yake na akaogopa kumkabili basi ndio amempa silaha atayompigia na kujifanya mnyonge kwake. Imam Ali (a.s.) anasema: “Kuogopa ni kuvunjika moyo na kuona haya ni kusumbuka.”

TazamaJuz.22(33:59-62)kifunguVitavyanafsi.’

Siasa nzuri ya vita ni kuwa mkakamavu mtu mbele ya adui yake, vile vile asipuuze nguvu za adui, bali ajiandae vizuri na amkabili kwa uimara kabisa bila ya kujali mashaka na tabu atakayoipata.

Qur’an imeandika siasa hii kwa kusema: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu.” Yaani msilegee mbele ya adui mkasalimu amri kwenye nguvu zao na utaghuti wao.

Pia kauli yake: “Na waandalieni nguvu vile muwezavyo.” Juz. 10 (8:60). Yaani msidharau nguvu zao; mjifunge kibwebwe kwa kila nguvu mliyo nayo ya watu na ya kiuchumi.

Na hali nyinyi ndio mko juu; yaani mtashinda, lakini mpaka muungune na kuwa safu moja kumkabili adui wenu na adui wa Mwenyezi Mungu; vinginevyo mtashindwa na haitabakia hata harufu yenu; kama inavyosema Qur’an katika Juz. 10 (8:46).

Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi, mkiitikia mwito wake wa jihadi kwa hali na mali, ili tamko la Mwenyezi Mungu liwe juu ili neno la haki liwe juu na neno la batili liwe chini. Ama yule mwenye kupenda raha na akasalimu amri kwenye nguvu ya upotevu na ufisadi, basi Mwenyezi Mungu ataachana naye na kumwachia aliyejisalimisha naye

Wala hatawanyima malipo ya vitendo vyenu kuanzia nafsi, watu au mali iliyotoka kwa ajili ya dini, nchi au haki yoyote. Muhanga huu hauwezi kwenda burebure; bali ni heshima ya dini na nchi katika maisha ya duniani na ni akiba Akhera mbele ya Mwenyezi Mungu.

Unaweza kuuliza: Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu na hali nyinyi ndio mko juu,” si inajulisha waziwazi kwamba mwenye nguvu anafaa kumdhibiti mnyonge bila ya kuwa na huruma naye wala kuwa na suluhu naye? Bila shaka hili linapingana na ubinadamu na uadilifu, wala haliafikiani na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً{208}

“Enyi ambao mmeamini! Ingieni kwenye usalama nyote” Juz. 2 (2:208)?

Jibu: kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu na hali nyinyi ndio mko juu,” maana yake ni ikiwa mtapata balaa ya adui aliye mnyama asiyekuwa na kipimo cha haki wala uadilifu wala hajilazimishi na kanuni wala ahadi na pia hafahamu lugha yoyote isipokuwa nguvu. Mkifikiwa na adui wa aina hii basi nilazima mkabiliane; msimwogope wala msiwe na huruma katika haki. Kummaliza adui huyu ni kuimaliza shari na kuleta heri ya wote.

Ajabu ya sadfa! Imetokea wakati nikiandika maneno haya leo hii 8 April 1970, Israil, ikitumia ndege aina Phantoum ya Amerika na makombora yake, imeshambulia shule ya msingi ya Bahrul-baqar katika Jamhuri ya Umoja wa Kiarabu1, na kuua watoto 47, na kujeruhi kadhaa, wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 12.

Bila shaka U.S.A. ndiyo inayobeba majukumu ya kuuliwa watoto wadogo wasiokuwa na hatia yoyote. Na pia majukumu ya mashambulizi ya mfano huo yaliyotokea katika kiwanda cha Aba Za’abal yaliyowaacha wahanga 33majeruhinawaliouawa.

Amerika ndio yenye majukumu, kwa vile ndiyo iliyoisheheni Israil kwa silaha na mali na ikaamrisha iwafanyie waarabu; kama hiyo yenyewe inavyoifanyia Vietnam. Vyombo vya habari vimenukuu kuwa jeshi la Amerika limesambaratisha mji mzima katika Vietnam. Hakuokoka katika mji huo mtoto wala mwanamke. Mji huu na mashule yake unahusiana vipi na vita?!

Je, usalama utakuweko na wanyama hawa? Jamani! Pengine labda maana ya usalama yawe ni kusalimu amri kwa madhalimu na waasi!

Hakika uhai wa duniani ni mchezo na upuzi kwa mwenye kuipondokea na akahadaika na ubatilifu wake; bali ni shari hasa kwa mwenye kuanzisha vita kwa ajili ya dunia. Na ni nyumba ya heri kwa mwenye kuwaidhika nayo na akaifanya ni maandalizi ya Akhera yake.

Na mkiamini na mkawa na takua atawapa ujira wenu.

Kuunganisha takua na imani kunafahamisha kuwa kuamini tu na kusadikisha hakuna malipo mbele ya Mwenyezi Mungu; bali hapana budi kuweko na vitendo pamoja na imani. Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا {30}

“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri.”Juz. 15 (18:30)

Wala hawaombi mali zenu. Na akiwaomba hizo na akiwashikilia mtafanya ubakhili, na atatoa chuki zenu.

Makusudio ya hawaombi ni hawataki mtoe mali yote wala kutoa mali nyingi ya kuwadhuru. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejaalia fungu la mafukara katika mali ya matajiri na akachunga kiwango cha kutosheleza mahitaji na vile vile masilahi ya watowaji wasidhurike.

Lau kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hekima yake, angeliwataka matajiri zaidi kiwango hiki na akawahimiza kutoa, basi wangelizuia na wangekua na chuki na Uislamu na Nabii.

Ehee! Nyinyi mnaitwa mtumie katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa Makusudio ya njia ya Mwenyezi Mungu ni jihadi. Usahihi ni kuwa inakusanya kila lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi ya watu kwa namna moja au nyingine.

Na wapo katika nyinyi wanaofanya ubakhili. Na anayefanya ubakhili basi anajifanyia ubakhili mwenyewe.

Bakhili anamnyima Mwenyezi Mungu na kujilimbikizia mwenyewe, lakini natija inakuwa kinyume na anavyotaka; pale anapoiweka nafsi yake kwenye ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na kuinyima radhi zake na thawabu zake. Tazama kifungu; ‘Mali ndio sababu ya ugomvi’ mwanzo wa Juz. 4 (3:92).

Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, na nyinyi ndio wahitaji wa fadhila zake na rehma zake. Hakupata ukwasi mja yeyote ila kwa sababu inayotoka kwake. Ama Yeye Mwenyezi Mungu ni mkwasi kwa dhati yake sio kwa kufaidika, ni mtendaji sio kwa kutumia ala, na ni mkadiriaji sio kwa kufikiria.

Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.

Kama mkiupinga mwito wa Mwenyezi Mungu na mkang’ang’ania uasi na ujeuri basi atawaondoa na awalete wengine watakaomsabihi na kumsifu bila ya kumuasi na lolote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14:19) na Juz. 22 (35:16).

  • 1. Jina hili lilikuwa likitumiwa na nchi mbili za kiarabu Misr na Syria zilizoungana mwaka 1958 ikiwa ni mwanzo wa umoja wa wa nchi za Kiarabu; kama ilivyokuwa ndoto ya Jamal Abdulnasser na kuvunjika mwaka 1961 kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Damscus. Hata hivyo Misr iliendelea kutumia jina hili hadi 1970, ilipobadilisha na kujiita Jamhuri ya Kiarabu ya Misr. Mauji ya watoto yalitokea upande wa Misr mkoa wa mashariki katika mji wa Husseynia. –Vyanzo vya habari za tovuti.