read

Aya 1 – 5: Tumekupa Ushindi

Maana

Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri.

Neno ‘ushindi’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ‘Fat-h’ ambalo lina maana nyingine zaidi ya hiyo. Lakini Makusudio yake hapa ni ushindi, kwa sababu ndiyo yanayokuja akilini mwanzo, na pia kwamba Nabii (s.a.w.) alisema: “Nimeteremshiwa Aya inayopendeza zaidi kwangu kuliko dunia na yaliyomo. Kisha akasoma: “Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri”. Maana ni kuwa tumekupa ushindi ewe Muhammad ushindi wa dhahiri.

Wametofautiana wafasiri kuhusu aina ya ushindi wenyewe. Tabariy ameishilia na kauli nne na Razi akaishilia na tano. Wafasiri wengi wamesema kuwa Makusudio ya ushindi hapa ni ushindi wa Suluhu ya Hudaybiya. Kwa sababu sura hii ilishuka baada ya mkataba wa amani aliowekeana Mtume na watu wa Makka, sehemu ya Hudaybiya.

Hata hivyo kauli iliyo na nguvu kwetu ni kuwa Makusudio ya ushindi hapa ni kuwa juu Uislamu, kuwa na nguvu waislamu na kudhalilika maadui wake wanafiki na washirikina. Kwa sababu ushindi katika Aya ni wa kiujmla haukufungwa na Hudaybiya, kuiteka Makka, kuwashinda waroma na wafursi au kwengineko.

Kwa hiyo basi Aya hii itakuwa inarudufu ile isemayo:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki, ili ipate kushinda dini zote, ijapokuwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33).

Kwa maneno mengine ni kuwa ushindi ni wa kiujmla sio wa kiaina.

Ili Mwenyezi Mungu akughufirie dhambi yako iliyotangulia na ijayo.

Unaweza kuuliza: lini Nabii alifanya dhambi mpaka asamehewe na Mwenyezi Mungu? Iko wapi isma ya manabii ya kuepukana na dhambi? Itakuwaje ushindi ndio iwe sababu ya maghufira? Kuna uhusiano gani baina ya ushindi na maghufira?
Jibu: Makusudio ya dhambi hapa sio dhambi ya Mtume kiuhakika na kiuhalisi. Itakuwaje na hali yeye ni mwenye kuhifadhiwa na madhambi na makosa. Makusudio ni kuwa washirikina wlikuwa wakiamini kuwa Mtume ana dhambi kutokana na mwito wake wa Tawhid, mwito wa kutupiliwa mbali ushirikina na kupiga vita kuiga waliopita.

Ama Makusudio ya maghufira ni kuwa washirikina hawa walikuja kugundua kuwa Muhammad (s.a.w.) hana dhambi na kwamba yeye ni Mtume wa kweli na wa haki na wao ndio waliokuwa na dhambi kwa kumtuhumu na risala yake.

Yaani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alitoa mwito wa Tawhid akikosoa ibada ya masanamu na kupiga vita dhulma na unyanyasaji na mengine ya ufisadi wa kijahilia na maigizo yake. Ni dhambi gani iliyokubwa zaidi kwa jahili na wengineo kuliko kumkosoa na kumtia ila na vitu vyake vitakatifu vya kidini na ada ya mababu zake ambayo ndio desturi yake?

Lakini baada Mwenyezi Mungu kuidhihirisha dini yake na kumnusuru Nabii wake kwa dalili na hoja na kuingia watu kwenye dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi, wakiwemo washirikina waliokuwa wakimuona Mtume ni mwenye hatia kwao na kwa miungu yao, iliwabainikia kuwa Muhammad (s.a.w.) ni mkweli na wao ni wakosefu.

Kwa ufupi ni kuwa makusudio ya dhambi ya Mtume ni dhambi yake kwa madai ya maadui zake washirikina, sio dhambi halisi. Na makusudio ya msamaha ni msamaha wao kwa lile walilodai kuwa ni dhambi; yaani toba yao kwa walivyomdhania Mtume.

Ama kuinasibisha dhambi kwa Mtume, katika dhahiri ya maneno, na kunasibisha msamaha kwa Mwenyezi Mungu, hilo ni jambo sahali, kwamba majazi yanatoa upeo wa hilo na zaidi.

Kuhusu uhusiano wa ushindi na maghufira, uko wazi – kwamba ushindi ndio sababu ya kufichuka ukweli wa Mtume na kuepuka kwake dhambi – iliyodaiwa - waliyomtuhumu nayo washirikina kabla ya ushindi.

Na akutimizie neema zake kwa kukupa ushindi dhidi ya madui zako na kuinua shani yako duniani.

Na akuongoze katika njia iliyonyooka ambayo ni sharia ya Mwenyezi Mungu inayodhamini heri ya watu na masilahi yao, kila wakati na kila mahali.

Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu.

Nusura yenye nguvu ni ile inayokuwa kwa haki na kwa ajili ya haki na kwa jihadi iliyowekewa sharia sio kwa njama au mapinduzi wala kwa msaada wa waovu.

Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili wazidi imani juu ya imani yao.

Makusudio ya utulivu ni kuridhia na kutulia kimwamko. Kwa sababu matukio yametuonyesha kuwa utulivu wa kijahili unaishia pabaya. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameipa nguvu dini yake akampa ushindi Nabii wake ili wafurahi waumini, nyoyo zao zitulie, wazidi kuwa na yakini na Mola wao, wamtegemee Nabii wao na kuwa na nguvu katika dini yao.

Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi.

Hii ni kinaya cha ukuu wa uweza; vinginevyo Mwenyezi Mungu hahitajii walimwengu, kwa sababu Yeye ni kukiambia kitu kuwa kinakuwa.

Hapa kuna ishara kwamba lau Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaangamiza washirikina bila jihadi na vita, lakini ni kwa ajili ya kuwajaribu waja ili ajulikane nani mzuri zaidi wa matendo.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima katika kuumba kwake na kupangilia kwake.
Ili awaingize waumini wanaume na waumini wanawake katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake, wadumu humo, na awafutie maovu yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tabari anasema: iliposhuka “Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri,” waumini walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): Pongezi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu amekwishakubainishia atakavyokufanyia, je na sisi? Ndio ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ili awaingize waumini wananume na waumini wanawake…” mpaka mwisho.

Hata kama riwaya itakuwa si sahihi, lakini hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu anasamehe maovu ya wanaoutubia na kuwangiza waumini katika rehema yake na pepo yake. Na atakayeingia Peponi atakuwa amefuzu fungu lenye kutosheleza.

وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ الظَّانِّينَ بِاللَّهِ ظَنَّ السَّوْءِ ۚ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ ۖ وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ وَلَعَنَهُمْ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا {6}

Na awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.

وَلِلَّهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا {7}

Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima.

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا {8}

Hakika tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji.

لِتُؤْمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتُعَزِّرُوهُ وَتُوَقِّرُوهُ وَتُسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا {9}

Ili mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mumsaidie, na mumhishimu, na mumsabihi asubuhi na jioni.