Aya 10 – 14: Baia Ya Ridhwan Chini Ya Mti
Kisa Kwa Ufupi
Hakika wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hakika anaivunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anayetekeleza aliyomuahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atampa ujira mkubwa.
Aya hii inaashiria Baiatur-ridhwan Baia iliyoridhiwa iliyokuwa chini ya mti. Kisa chake ni kama ifuatavyo:
Hadi kufikia mwaka wa sita wa Hijra, washirikina ndio waliokuwa wakitawala Makka na Nyumba takatifu. Mwishoni mwa mwaka huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alitoka Madina Munawwara pamoja na waislamu 1400 kuelekea Makka Mukkarrama kufanya Umra wakiwa hawana fikra yoyote ya vita.
Walipofika sehemu inayoitwa Hudaybiyya, Abu Sufyani alipata taarifa ya kufika kwao. Kwa hiyo akawakusanya makuraishi na wakapitisha azimio la kuwazuia waislamu wasiingie Nyumba takatifu (Al-Ka’aba) kwa nguvu ya silaha. Wakawakusanya wapanda farasi wakiongozwa na Khalid Bin Al- Walid.
Wakapishana wajumbe baina ya Mtume (s.a.w.) na wao. Ujumbe wa makuraishi ulimtaka Mtume arudi Madina wala asiingie Makka, Mtume naye akawajibu kuwa sisi hatukuja kupigana na yoyote, tumekuja kuzuru Nyumba takatifu tu na atakayetuzuia tutapigana naye.
Urwa Bin Mas’ud alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa makuraishi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), akaona maswahaba wakionyesha aina kwa aina ya mapenzi kwa Mtume, hakutawadha ila waligombania mabaki ya udhu wake na hakutema mate ila waliyachukua mate yake; hata unywele wake ukianguka tu walikuwa wakiugombania.
Basi akarudi akiwa ameshangaa sana kwa aliyoyaona akasema: “Enyi makuraishi jamani! Mimi nilimuona Kisra kwenye Ufalme, Kaizari na Najashi, lakini sikuona kwao ufalme kwa watu wao unaonafana na Muhammad kwa sahaba zake. Mimewaona hawawezi kumwacha kwa jambo lolote. Hebu fikirieni vizuri!”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimtuma Uthman kwa Makuraishi kwa vile yuko karibu na Abu sufyan na akamwambia: ‘’Waambie sisi hatukuja kwa vita; tumekuja kuzuru hii nyumba tukitukuza heshima na miko yake. Tuna wanyama tutawachinja kisha twende zetu.’’
Uthman alipowapelekea habari hii wakasema: ‘’Haiwezekani kabisa.’’ Ikawa hakuna habari za Uthman, ukatokea uvumi kuwa ameuawa. Mtume aliposikia uvumi huu akasema: Hatuondoki mpaka tupigane na watu hawa.
Akatoa mwito wa kuungwa mkono akiwa amekaa chini ya mti. Basi saha- ba zake wakambai (kiapo cha utii) haraka sana kwamba watamtii na wako tayari kufa katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliisifu baia hii kuwa ni bai yake hasa, na kwamba ameichukua kwa mkono wake, atakayevunja ahadi hii atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu na kujiletea hasira zake na atayeiteleza kikamilifu atakuwa karibu na Mola na mwisho mzuri.
Jina maarufu la baia hii ni Baia iliyoridhiwa (Baiatur-ridhwan) au Baia ya mti (Bai’atu-shajara). Pia inaitwa Baia iliyoridhiwa chini ya mti kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya sura hii tuliyo nayo: “Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti.”
Makuraishi walipoona ukakamavu wa Mtume walikuja chini kufanya suluhu. Wakakakubaliana kwamba waislamu wasiingie Makka mwaka ule mpaka mwaka unaofuatia wakaingia kufanya Umra na kukaa siku tatu bila ya kuwa na silaha isipokuwa panga kwenye ala zake.
Mtume (s.a.w.) akamwita Ali bin Abi Twalib na akamwambia: ‘’Andika Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.’’ Mjumbe wa makuraishi akapinga ana akesema: Andika kwa jina lako ewe Mola wangu. Akakubali Mtume na Ali akaandika. Nabii akaendelea kusema: Andika, haya ndiyo waliyokubaliana Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mjumbe wa makuraishi akapinga tena, na kusema: Andika jina lako na la baba yako. Ali akasita.
Mtume akamwambia na wewe yatakupata mfano wake; akiwa anamwashiria suala la mahakimu wawli katika vita vya Siffin. Na hiyo ni miongoni mwa ilimu ya ghaibu aliyompa wahyi Mwenyezi Mungu Mtume wake mtukufu, ambayo ni miongoni mwa nguvu ya hoja ya utume wake na ukweli katika utume wake.
Walipomaliza kutiliana sahii mkataba wa Hudaybiyya, Mtume na maswahaba walitoa Ihramu zao, wakachinja na wakanyoa vichwa vyao. wakabaki siku kadhaa pale Hudaybiyya kisha wakarudi zao Madina.
Mwaka uliofuatia Nabii na Maswahaba walieleka Makka kufanya Umra. Wakaingia huku wakipiga Takbira hii kwa sauti: la ilaha illa Allah, nasara abdah, waazza jundah, wakhadhalal-ahazaba wahdah (hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa pekee yake, amemnusuru mja wake, amelipa nguvu jeshi lake, na amevidhalilisha vikosi hali ya kuwa peke yake).
Wakabakia Makka siku tatu wakitufu na kuchinja. Umra huu unaitwa Umra wa kulipa, kwa sababu unachukua nafasi ya umra ule waliozuiliwa na washirikina. Ilishuka Aya kwa umra huo kama ilivyoelezwa katika Aya ya 28 ya sura hii tuliyo nayo: “Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya ya haki. Bila ya shaka mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza. Hamtakuwa na hofu.”
Mabedui Waliobaki Nyuma
Watakuambia mabedui waliobaki nyuma: Imetushughulisha mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha.
Mtume (s.a.w.) alipotaka kutoka kwenda Makka mwaka ule wa Hudaybiyya. Waislamu walimhimiza wasafiri naye, lakini baadhi ya mabedui wanaoishi kando kando ya Madina na wanafiki wengine walikataa kutoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), wakidhania kuwa Makuraishi hawatamruhusu Muhammad (s.a.w.) kuingia Makka. Wakaambiana: Hatuna haja ya kujiingiza kwenye hatari hii.
Bada ya kutimia mkataba, Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake: utakaporudi Madina wale waliobaki nyuma watatoa visababu, kuwa kuangalia familia zao na mali zao ndiko kulikowazuia kufuatana nawe na watakuomba msamaha wa uongo na wakinafiki. Pia watakutaka uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu awaridhie na kuwasamehe yaliyopita.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawakadhibisha kwa kusema: Wanasema kwa ndimi zao yasiyokuwamo nyoyoni mwao; kama ilivyo kawaida ya wanafiki.
Sema: Ni nani awezaye kuwasaidia na chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka kuwadhuru au akitaka kuwanufaisha?
Mnamwambia uwongo Mwenyezi Mungu na hali Yeye anajua siri zenu na dhahiri zenu? Tena heri yenu na shari yenu iko mikononi mwake. Ni nani atakayemzuia akiwatakia heri au shari?
Bali Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda na tena anamjulisha Mtume wake kuwa nyinyi mnadhihirisha yasiyokuwa nyoyoni mwenu.
Lakini mlidhani kwamba Mtume na waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu.
Mlimwacha Mtume mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hatamnusuru Nabii wake na wale waliokuwa pamoja naye na kwamba ushindi utakuwa wa maadui wa Mwenyezi Mungu dhidi ya vipenzi vyake.
Na mkadhania dhana mbaya kuwa waislamu wanakwenda kwenye mauti tu. Wala hakuna tegemeo la dhana isipokuwa wasiwasi wa shetani tu, kwamba Mwenyezi Mungu hataitia nguvu dini yake na kumnusuru Mtume wake. Na mmekuwa watu wanaoangamia. Kila mwenye kukubali uongozi wa shetani basi ataongozwa kwenye maangamizi.
Na asiyemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa hakika tumewaandalia makafiri Moto mkali. watadumu humo wala hawatapata wa kuwasaidia.
Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi.
Hakuna mfalme mwingine asiyekuwa Yeye wala hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwake. Mwenye kumfanyia ikhlasi na akamtegemea Yeye basi atamtoshea. Na mwenye kuelekea kwa mwinginewe basi atamwachia huyo.
Humsamehe amtakaye yule anayestahiki maghufira, kwa sababu ni hakimu, ni muhali kwake kumsamehe anayemwga damu kidhulma, akavunja mashule ya watoto wadogo na akapora vyakula vya wenye njaa. Na humwadhibu amtakaye anayestahiki adhabu; wala Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu yule anayejihurumia yeye na mwingine; vinginevyo asiye na huruma naye hahurummiwi. Na madhalimu hawana wa kuwanusuru.
سَيَقُولُ الْمُخَلَّفُونَ إِذَا انْطَلَقْتُمْ إِلَىٰ مَغَانِمَ لِتَأْخُذُوهَا ذَرُونَا نَتَّبِعْكُمْ ۖ يُرِيدُونَ أَنْ يُبَدِّلُوا كَلَامَ اللَّهِ ۚ قُلْ لَنْ تَتَّبِعُونَا كَذَٰلِكُمْ قَالَ اللَّهُ مِنْ قَبْلُ ۖ فَسَيَقُولُونَ بَلْ تَحْسُدُونَنَا ۚ بَلْ كَانُوا لَا يَفْقَهُونَ إِلَّا قَلِيلًا {15}
قُلْ لِلْمُخَلَّفِينَ مِنَ الْأَعْرَابِ سَتُدْعَوْنَ إِلَىٰ قَوْمٍ أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ تُقَاتِلُونَهُمْ أَوْ يُسْلِمُونَ ۖ فَإِنْ تُطِيعُوا يُؤْتِكُمُ اللَّهُ أَجْرًا حَسَنًا ۖ وَإِنْ تَتَوَلَّوْا كَمَا تَوَلَّيْتُمْ مِنْ قَبْلُ يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا {16}
لَيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ ۗ وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَمَنْ يَتَوَلَّ يُعَذِّبْهُ عَذَابًا أَلِيمًا {17}