read

Aya 15 – 17: Tuacheni Tuwafuate

Maana

Waliobaki nyuma watasema: Mtapokwenda kuchukua ngawira, tuacheni tuwafuate!

Ni wale wale waliokataa kutoka na Mtume alipoelekea Makka mwishoni mwa mwaka wa sita, ambao amewakusudia Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia. Mtume aliwahimiza wafuatane naye, lakini wakawahofia makuraishi kwa visingizio vya familia na mali.

Baada ya Mtume kurudi Hudaybiyya alikaa Madina hadi mwanzo mwanzo wa mwaka wa saba, akaenda kupigana Khaybara. Huko waislamu walipata ngawira nyingi sana, zilzioamsha tamaa ya waliobaki nyuma. Wakamwambia Mtume na wale aliokuwa nao: tuchukueni na sisi kwenye ngawira hizo. Leo wanataka kutoka na jana walipoitwa walijitia kushughulika na watu wao na mali wakihofia jihadi. Haya ndiyo mantiki ya kila aliyetekwa na tamaa na asione jingine ila hiyo tu.

Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu.

Wanaotaka ni hao hao waliobaki nyuma. Makusudio ya maneno ya Mwenyezi Mungu hapa ni ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwanyima ngawira waliobaki nyuma, ambayo ameiashiria kwa kusema: “Mtapo kwenda kuchukua ngawira.”

Lakini Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hikima yake, hakutubain- ishia ngawira yenyewe.

Je, ni ngawira za Khaybara au yinginezo. Hata hivyo wafasiri wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaahidi watu wa Baia iliyoridhiwa kuwa ngawira ya Khaybara itawahusu wao tu. Razi anasema: Hii ndio kauli mashuhuri kwa wafasiri. Maraghi naye akasema: “ni habari sahaihi.” Hili haliko mbali, kwa sababu vita vya Khaybar ndivyo vya kwanza baada ya mkataba wa Hudaybiyya.

Vyovyote iwavyo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Nabii wake awaambie waliobaki nyuma: Sema: Hamtatufuata kabisa kuchukua ngawira kwa sababu nyinyi mlikataa kufuatana nasi Makka mkihofia vita. Mwenyezi Mungu alikwishasema hivi zamani kuwa hamna fungu la ngawira.

Hapo watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu.

Hapana, sivyo kabisa! Mwenyezi Mungu hakutunyima ngawira bali nyinyi ndio mnaotunyima kwa chuki na husuda kwetu.

Bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.

Hili ni jawabu la Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na kauli yao ‘bali mnatuhusudu.’ Sio kama mlivyodai, ni kutojua kwenu na uasi wenu kwenye hukumu nyingi.

Waambie walioachwa nyuma katika mabedui ambao walikataa kutoka na Mtume kwenda Makka: Mtakujaitwa kwenda pigana na watu wakali kwa vita.

Aliyewaita ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Baada ya vita vya Khaybar, Mtume aliwaita kwenye vita vya Hunayn, Taif na Tabuk.

Mpigane nao au wasalimu amri.

Yaani wakali ambao mtaitwa mkapigane nao watahiyarishwa mambo mawili na Mtume: Upanga au Uislamu. Basi je, mtaitikia mwito wa Mtume au mtarudi kwenye visigino vyenu kama mlivyofanya hapo mwanzo? Kwa maneno mengine ni kuwa kupambana kwenu na wakali wa vita ndio uthibitisho wa ukweli wenu sio kuchukua ngawira.

Basi mkimtii, Mwenyezi Mungu atawapa ujira mzuri; ngawira duniani na Pepo Akhera. Au Pepo na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yule atakayeuawa.

Na mkigeuka kama mlivyogeuka kwanza, atawaadhibu kwa adhabu iliyo chungu.

Kuna adhabu gani chungu zaidi kuliko adhabu ya Jahannam?

Kipofu hana tabu, wala kiguru hana tabu, wala mgonjwa hana tabu.

Makusudio ya tabu hapa ni dhambi. Maana ni kuwa hakuna dhambi kwa watu wa aina zote hizi tatu kama wakibaki nyuma ikiwa ni vita vya kutoa mwito wa uislamu.

Ama jihadi ya kujikinga na adui na kumzuia na uchokozi wake, hivyo ni lazima kwa wote wanaume kwa wanawake, watu wazima kwa watoto, na wazima na walemavu. Kila mtu ni kwa kadiri ya nguvu zake.

Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitiwayo na mito chini yake. Na atakayegeuka atamuadhibu kwa adhabu chungu.

Maana yako wazi – ni Pepo kwa mtiifu na Moto kwa muasi.

Maana haya yamekaririka kwenye makumi ya Aya, kwa mnasaba wa kutaja heri na shari, kutanabahisha kwamba Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, kwamba mtu hataachwa bure na kwamba yeye atakutana na Mwenyezi Mungu kwa matendo yake. Ni matendo tu ndio yatakua maudhui ya hisabu na kipimo cha malipo.

لَقَدْ رَضِيَ اللَّهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنْزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا {18}

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa ushindi wa karibu.

وَمَغَانِمَ كَثِيرَةً يَأْخُذُونَهَا ۗ وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا {19}

Na ngawira nyingi watakazozichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

وَعَدَكُمُ اللَّهُ مَغَانِمَ كَثِيرَةً تَأْخُذُونَهَا فَعَجَّلَ لَكُمْ هَٰذِهِ وَكَفَّ أَيْدِيَ النَّاسِ عَنْكُمْ وَلِتَكُونَ آيَةً لِلْمُؤْمِنِينَ وَيَهْدِيَكُمْ صِرَاطًا مُسْتَقِيمًا {20}

Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira nyingi mtakazozichukua, basi amewatangulizia hii, na akaizuia mikono ya watu isiwafikie. Na ili hiyo iwe ni Ishara kwa waumini, na akawaongoza njia iliyonyooka.

وَأُخْرَىٰ لَمْ تَقْدِرُوا عَلَيْهَا قَدْ أَحَاطَ اللَّهُ بِهَا ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا {21}

Na nyingine hamjaweza kuzipata, Mwenyezi Mungu amekwishazizingira. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

وَلَوْ قَاتَلَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوَلَّوُا الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا {22}

Na lau makafiri wangelipigana nanyi basi bila ya shaka wangeligeuza migongo, kisha wasingelipata mlinzi wala msaidizi.

سُنَّةَ اللَّهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلُ ۖ وَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّهِ تَبْدِيلًا {23}

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokwishapita zamani, hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

وَهُوَ الَّذِي كَفَّ أَيْدِيَهُمْ عَنْكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ عَنْهُمْ بِبَطْنِ مَكَّةَ مِنْ بَعْدِ أَنْ أَظْفَرَكُمْ عَلَيْهِمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا {24}

Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kuwapa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.