read

Aya 18 – 24: Walipokubai Chini Yamti

Maana

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashira Baia iliyoridhiwai chini ya mti, kwamba Yeye yuko radhi nayo na watu wake. Yamekwishatangulia maelezo ya Baia hii katika Aya 10 ya Sura hii.

Na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa

Wanaelezewa watu wa baia. Nyoyo zao zilijaa ukweli na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Makusudio ya utulivu ni raha na utulivu wa moyo. Ushindi wa karibu ni mkataba wa Hudaybiyya ambao miongoni mwa athari zake ni kuingia waislamu Makka kufanya umra, pamoja na kuchukia makuraishi. Kuna riwaya isemayo kuwa Umar bin Al- khattwab alimuuliza Nabii (s.a.w.): “Ni ushindi huu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Mtume akasema: “Ndio.”

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya ngawira nyingi, ni ngawira za Khaybara. Kwa sababu Khaybara ilikuwa mashuhuri kwa ngawira nyingi na mashamba. Lakini kauli yenye nguvu ni kila ngawira walizopata watu wa Baia iliyoridhiwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema ngawira kiujumla bila ya kuifunga na jambo maalum.

Maana yake kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaneemesha watu wa Baia iliyoridhiwa kwa utulivu na neema nyingi, kwa sababu Yeye alijua kuwa wao wana ikhlasi katika dini yao na ukweli wa azma yao ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Kila mafanikio waliyoyapata waislamu na kuwapeleka mbele ni katika Athari za nguvu za Mwenyezi Mungu, uweza wake na hekima yake katika mipangilio.

Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira nyingi mtakazozichukua.

Ngawira nyingi hapa ni kila nyara walizozipata waislamu zama za Mtume (s.a.w.). Kwa hiyo basi tofauti ya ngawira zilizotajwa kwenye Aya iliy- otangulia ni kuwa zile zilizowahusu watu wa Baia iliyoridhiwa na hizi ni za waislamu wote kila mahali na kila wakati.

Basi amewatangulizia hii.

Hii ni ishara ya suluhu ya Hudaybiyya. Kwa sababu suluhu hii ndiyo iliy- otangulia. Ama ngawira za Khaybara zilikuwa baada ya suluhu. Lau si neno hii, tungelisema iliyotangulia ni suluhu pamoja na Khaybar.

Na akaizuia mikono ya watu isiwafikie.

Tabari anasema, wametofautiana watu wa taawili kuhusu neno ‘watu’ hapa. Ikasemekana ni mayahudi wengine wakasema ni makuraishi. Tuonavyo sisi makusudio ni maadui wa Uislamu waliojaribu kuumaliza na kuwamaliza Waislamu. Hakuna lililowazuia isipokuwa udhahifu.

Na ili hiyo iwe ni Ishara kwa Waumini.

Hiyo’ ni suluhu ya Hudaybiyya. Mwenyezi Mungu ameifanya ni alama kwa waumini kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao na anawanusuru na maadui zao. Hazikupita siku ila ikawabainikia waumini kuwa mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa ni heri kwao na shari kwa washirikina.

Na akawaongoza njia iliyonyooka kwenye kila yaliyo na manufaa yenu ya dunia na Akhera.

Na nyingine hamjaweza kuzipata, Mwenyezi Mungu amekwishazizingira.

Yaani Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira mnazoweza kuzipata hivi sasa, vile vile amewaahidi nyingine msizoweza kuzipata hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu amewahifadhia, na mtazipata baadae, iwe karibu au mbali.

Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hashindwi kuwapa nyara zaidi ya mnavyofikiria na kutegemea.

Na lau makafiri wangelipigana nanyi basi bila ya shaka wangeligeuza migongo, kisha wasingelipata mlinzi wala msaidizi.

Kama kwamba muulizaji aliuliza itawezekana vipi waislamu wapate nyara za makafiri, na hali wao wana nguvu na ni wengi wanaopigania nafsi zao?

Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akajibu kuwa Yeye yuko pamoja na wau- mini na anawakinga. Mwenyezi Mungu hashindwi na jambo. Ama makafiri hawana kimbilio isipokuwa upanga au kukimbia.

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokwishapita zamani, hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mitume waliopita kuwashin- da maadui zao. Kama muulizajai atauliza, mbona hii haiafikiani na Aya zinazoelezea waziwazi kuwa mayahudi walikuwa wakiwaua manabii bila ya haki? Majibu yake yako kwenye Juz. 17 22: (38 – 41).

Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kuwapa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.

‘Yeye’ ni Mwenyezi Mungu. Waliozuiwa mikono ni makafiri. Imesemekana kuwa Makusudio ya bonde la Makka ni Hudaybiyya, kwa vile mji huo uko karibu na Makka.

Wengine wakasema ni Makka yenyewe. Maana haya ndiyo yanayokuja haraka kwenye fahamu, kutokana na neno bonde.

Maana ni kuwa enyi waislamu mmeingia Makka, uliokuwa mji mkuu wa shirki na kitovu cha washirikina mkiwa washindi bila ya vita.

Hii ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu na neema yake kubwa kwenu. Kwa sababu Yeye ndiye aliyewazuia kupigana kwa kuwatia hofu katika nyoyo zao na akawazuia nyinyi kupigana nao kwa kuwakataza.

Suluhu ya Hudaybiyya ilikuwa mwaka wa sita wa Hijra, Umra ya kulipa ukawa mwaka wa saba na kuiteka Makka kukawa katika mwaka wa nane.

هُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَالْهَدْيَ مَعْكُوفًا أَنْ يَبْلُغَ مَحِلَّهُ ۚ وَلَوْلَا رِجَالٌ مُؤْمِنُونَ وَنِسَاءٌ مُؤْمِنَاتٌ لَمْ تَعْلَمُوهُمْ أَنْ تَطَئُوهُمْ فَتُصِيبَكُمْ مِنْهُمْ مَعَرَّةٌ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۖ لِيُدْخِلَ اللَّهُ فِي رَحْمَتِهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ لَوْ تَزَيَّلُوا لَعَذَّبْنَا الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا {25}

Hao ndio waliokufuru na wakawazuia msiingie Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao pa kuchinjwa. Na lau si wanaume waumini na wanawake waumini msiowajua kuwa mtawasaga na mkaingia matatani kutokana nao bila ya kujua. Ili amuingize amtakaye katika rehema yake. Lau wangelipambanuka bila ya shaka tungeli waadhibu waliokufuru kwa adhabu chungu.

إِذْ جَعَلَ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي قُلُوبِهِمُ الْحَمِيَّةَ حَمِيَّةَ الْجَاهِلِيَّةِ فَأَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَلْزَمَهُمْ كَلِمَةَ التَّقْوَىٰ وَكَانُوا أَحَقَّ بِهَا وَأَهْلَهَا ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا {26}

Pale wale ambao wamekufuru walipotia katika nyoyo zao hasira, hasira za kijinga, Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya waumini, na akawalazimisha neno la takua. Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.