read

Aya 27 – 29:mRuiya Ya Mtume

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya ya haki. Bila ya shaka mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza. Hamtakuwa na hofu.

Dhahiri ya Aya na Hadith mutawatir zinafahamisha kuwa Mtume (s.a.w.) aliota kuwa yeye na swahaba zake wameingia Makka kwa amani, wakatufu nyumba kongwe; vile wanavyotaka, wengine wakiwa wamenyoa na wengine wamepunguza. Basi Mtume akawaelezea swahaba zake alivyoona usingizini. Wakafurahi na kufikiria kuwa mwaka huhuo wataingia Makka. Mtume akaenda nao Makka lakini wakazuiliwa Hudaybiyya na wakarudi Madina; kama tulivyokwishaeleza.

Hapo wanafiki wakawa wamepata la kusema: “Haya iko wapi ndoto? Hatukunyoa, hatukupunguza wala hatukuona Msikiti? Wakasahau au wakajitia kusahau kuwa Mtume hakutaja muda. Mmoja akamuuliza Mtume: si umesema hakika utauingia Msikiti Mtakatifu kwa amani? Akasema ndio, lakini sikusema ni mwaka huu.

Mwaka uliofuatia, ambao ulikuwa ni mwaka wa saba wa Hijra, waislamu waliingia Makka kufanya Umra, wakatufu Al-Ka’aba wanavyotaka, akanyoa mwenye kunyoa na kupunguza mwenye kupunguza. Wakabaki hapo siku tatu kisha wakarejea Madina. Ndio ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya,” yalipojitokeza yale aliyoota Mtume na kuwaambia:

Alijua msiyoyajua.

Mwenyezi Mungu alijua masilahi ya kuuahirisha umra baada ya mkataba wa Hudaybiyya, jambo ambalo waislamu hawakulijua; ambayo ni kuepusha vita, kusilimu washirikina wengi waliomzuilia Mtume na maswahaba.

Mbali na haya aliwapa ushindi ulio karibu.

‘Haya’ ni kuhakika ndoto ya kuingia Makka kwa amani. Makusudio ya ushindi ni mkataba wa Hudaybiya au ni huo na kuichukua Khaybara. Maana ni kuwa suluhu hii na kuiteka Khaybara kulikofanyika baada siku kidogo, kulifanyika kabla ya kuhakikika ndoto. Mambo hayo mawili ni ushindi mkubwa sawa na kuingia Makka.

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi.

Makusudio ya Mtume ni Muhammad (s.a.w.). Uwongofu na dini ya haki ni Uislamu. Ulitukuka na kuenea mashariki mwa ardhi na magharibi yake. Kwa sababu unatoa mwito wa kutenda kwa ajili maisha bora na kukataza kila ambalo litakuwa ni kikwazo katika njia ya kufikia hilo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9:33).

Maswahaba Na Qur’an

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesimulia katika Kitabu chake Kitakatifu kuwa Musa Bin Imran aliwalingania wana wa Israil kwenye vita wakamwambia:

 فَاذْهَبْ أَنْتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ {24}

“Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa.” Juz. 6 (5:24).

Pia alisimulia kuwa watu wa Bwana Masih walijaribu kumuua na kumsulubu na wanafunzi wake wakamwambia: Je Mola wako anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni; aliposema: Mcheni Mwenyezi Mungu. Wakasema: Tunataka kula katika hicho Tazama Juz. 7 (5:111-112).

Na akateremsha Sura nzima mbali ya Aya nyinginezo kadhaa kuwashutumu maswahaba wanafiki, lakini vile vile aliteremsha Aya nyingi za kuwasifu maswahaba wema wenye takua; miongoni mwa Aya hizo ni ya 18 ya sura hii tuliyo nayo, tuliyoifasiri punde tu na ile isemayo:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنْصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُمْ بِإِحْسَانٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {100}

“Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Ansari, na wale waliowafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu yuko radhi nao na wao wako radhi naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” Juz. 11 (9:100).

Na pia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye, wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.

Waovu huungana katika kutafuta windo, na wanapolipata wanauana wao kwa wao kugombania kulila. Lakini wenye ikhlasi wao wako wako pamoja tu wakati wote, hawatofautiani. Ni ndugu katika dini wakihurumiana na kusaidiana; ni kama familia moja, wanasaidiana kwenye haki na watu wake na wanapiga vita ubatilifu na wanachama wake.

Hii ndio sifa halisi ya swahaba wa Muhammad (s.a.w.) kwa ushahidi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu pale alipowasifu wao na Mtume kuwa wanakasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wanaridhia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Haya ameyatambua Dkt. Twaha Hussein, mwanafasihi ambaye huwa anafahamika kwa ishara na dalili. Anasema katika kitabu chake: Mir-atul-islam (Kioo cha uaislamu): “Uislamu wa manabii haukuwa ni twaa ya dhahiri isipokuwa uaislamu wao ulikuwa mpana wenye kina na wa ukweli zaidi ya inavyowezekana kuwa Uislamu. Na Uislamu wa waliokuwa wema katika Maswahaba haukuwa na ufinyu unaosimama mbele ya utii ulio dhahiri, isipokuwa ulikuwa ni mpana na wenye kina zaidi ya hivyo.”

Kisha Dkt. akampigia mfano Ammar Bin Yasir kwa Uislamu huu wa kina, akasema: “Ammar bin Yasir alikuwa akipigana pamoja na Ali katika Siffin kwa hamasa, naye akiwa ni mzee wa miaka tisini au kupita. Alikuwa akipigana kwa imani, yaani kwamba yeye anaitetea haki. Siku alipouawa alikuwa akiwahimiza watu huku akisema: Ni nani atakayekwenda Peponi? Leo nitakutana na wapenzi Muhammad na kikosi chake.”

Anaendelea kusema: “Kuuawa kwa Ammar kulikuwa ni kumthibitisha Ali na walio wema katika maswahaba zake na kumuweka kwenye shaka Muawiya na waliokuwa pamoja naye. Hiyo ni kwa sababu Wahajiri wengi na Answar walimuona Mtume (s.a.w.) akipapasa kichwa cha Ammar na kumwambia: Masikini ewe mwana wa Sumayya, kitakuua kikundi kiovu.”

Utawaona wakirukuu na kusujudu.

Yaani mandhari yanamfanya muangaliaji awaone kuwa wao ni watu wa kurukuu na kusujudu, hata kama wakati huo hawako hivyo.

Wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu.

Makusudio ya athari ya kusujudu hapa sio ile alama nyeusi inayoonekana kwenye paji la uso, hapana kwa sababu alama hizi nyingi ni za kinafiki na ria; isipokuwa makusudio yake ni usafi na uangavu unaonekana usoni kutokana na athari ya ibada.

Maana ni kuwa maswahaba walirukuu na kusujudu kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kuhofia ghadhabu zake na adhabu zake. Athari hiyo, ukiichunguza, inajitokeza katika nyuso zao kiuhakika, kwa sababu ibada ya ikhlasi ya Mungu inaleta utwahara na usafi katika nafsi ya mja mwenye ikhlasi na kujitokeza kwa ukamilifu usoni; sawa na inavyojitokeza huzuni na furaha.

Huu ndio mfano wao katika Tawrat na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya shina lake.

Hiki ni kinaya cha maswahaba wa Mtume (s.a.w.); mwanzo wanakuwa wachache kisha wanazidi na kuwa wengi. Ufafanuzi wa mfano huu ni kuwa Tawrt na Injili zimetoa bishara ya Muhammad (s.a.w.), zikawasifia maswahaba zake kama mmea unaokuwa, ukazaa matunda na yakawa mengi pamoja na matawi yake, yakashikana vizuri na ukawa una nguvu. Ukawapendeza wakulima kwa uzuri wake na kukua kwake.

Ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri.

Sio mbali kuwa makusudio ya wakulima hapa ni Mtume, maadamu mmea ni swahaba zake, kwa sababu yeye ndiye aliyewainua kufikia mahali walipo; na kwa fadhila yake wameshinda vita wakati wake na baadae. Na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja wakulima badala ya mkulima kwa kumtukuza Mtume (s.a.w.).

Ikumbukwe kwamba tunayasema haya kwa njia ya uwezekano tu wa kukisia

Mwenyezi Mungu amewaahidi walioamini na wakatenda mema katika wao maghufira na ujira mkubwa.

Maana yake yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 6 (5:9).

Je, Shia Ithanaasharia Wana Tafsiri Ya Ndani?

Mwanafasihi wa Misr, Dkt Mustafa Mahmud, alitoa mfulululizo wa makala 13, katika jarida la Sabahul-khayr. Katika makala hizo alizungumzia muujiza wa Qur’an, kisa cha kuumba1 na maudhui mengine ya ghaibu.

Kisha yakakusanywa makala katika kitabu kilichoitwa: Muhawalatu lifahmi asriy lilqur’an (Kujaribu kuifahamu Qur’an kisasa). Kikachapishwa na kutolewa mnamo mwezi wa tatu au wa nne mwaka 1970.

Katika makala ya ‘Mungu mmoja na dini moja,’ mtungaji aliwachanganya Shia Ithnaashariya pamojana vikundi vinavyofasiri Qur’an kwa undani, na kwamba wao ni sawa na Al-babiyya na Al-khawarij, wakifasiri Qur’an kwa tafsiri ya undani.

Basi nikamwandikia barua kwamba Shia Ithanaasharia, wako mbali zaidi ya watu wote na fikra hii ya uzushi na upotevu na kwamba vitabu vyao vinashudia hilo na vimejaa kwa watu. Nikamtajia baadhi ya vitabu hivyo na jinsi masheikh wa Azhar wenye insafu walivyosema kuhusu Shia Imamia; kama vile marehemu Sheikh Shaltut na wengineo waliounukuliwa na jarida la Al-islam, linalotolewa Misr na Darut-taqrib.
Katika jioni ya 15-4-1970, nilisikia mlio wa simu, akawa ni Dkt. Mustafa Mahmud akizungumza kutoka Triumph Hotel ya Beirut…Tukawa pamoja kwa mara ya kwanza. Tukazungumza kuhusu kitabu chake Allahu wal-insan (Mwenyezi Mungu na mtu) na majibu yangu Allahu wal-aql (Mwenyezi Mungu na akili).

Basi nikamwalika nyumbani kwangu siku iliyofuatia. Mazungumzo yetu yalikuwa juu Uislamu na tafsiri za ndani. Miongoni mwa maneno aliyoyasema mwana fasihi huyu ni: “Baadhi ya Shia wanafasiri “Amezichanganya bahari mbili kwa kuzikutanisha.2” kuwa ni Ali na Fatima.”

Nikwambia: Je, ni mantiki na ni sawa kweli kulihusisha kundi lenye mamilioni ya wafuasi kwa kauli ya mmoja wao, anayejiwakilisha yeye mwenyewe tu? Je, ni lazima ikiwa sheikh mmoja atafasiri Aya ya Qur’an kwa undani, ndio taifa zima lihisabiwe wanafasiri Qur’an kwa undani? Ikiwa malenga mmoja wa Misr atafasiri ubeti wa shairi kialama, je, ni sawa kusema kuwa malenga wote wa Misri wanafasiri mashairi kialama? Niliendelea kumwambia: “Hakika Shia Ithnaasharia wana vitabu vya kiitikadi vinavyokubalika; kama vile Awail al-maqalat cha Sheikh Mufid, Qawaidul-aqai cha Nasruddin Attusi na sherehe yake cha Allama Hill na yaliyoelezwa katika Sharhut Tajrid minat Tawhid…”

Nilikuwa nikikutana na Tafsiri ya kiundani ya masheikh wa kisunni wakati nikifanya utafiti wa rejea, lakini nilikua nikizipuuza, kwa vile zilikuwa haziendani na malengo ya tafsiri yangu. Basi Dkt. Alipotoa hoja ya bahari mbili, nilijaribu sana kukumbuka angalau tafsiri moja tu ili nipinge manaeno ya Dkt. Lakini kumbukumbu zangu ziliniangusha wakati nilipokuwa nazihitajia sana. Basi tukaendelea na maudhi mengine.

Ilikuwa ni sadfa wakati tukijadilina, kuwa ninafasiri sura hii ya Al-fat-h. Siku iliyofuatia nikafika kwenye Aya isemayo: “Ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya shina lake,” Mara nikasoma tafsiri za Kissuni: Ruhul-bayan ya Isamil Haqqi na Ats-hil ya Alhafidh bin Ahamd Al-Kalabi. Wote ni wa kissuni, ninawanukuu: “Ni kama mmea uliotoa chipukizi lake Kwa Abu Bakr, kisha ukalitia nguvu kwa Umar, ukawa mnene kwa Uthman, ukasimama sawa juu ya shina lake kwa Ali.”

Basi niliyoyaona katika tafsiri hizi yakanikumbusha niliyoyasoma zamani katika kitabu Hayatu Al-imam Abu Hanifa (Maisha ya Imam Abu Hanifa) cha Sayyid Afifi, kwamba Suyut amesema: “Wamesema maulama kwamba Mtume (s.a.w.) alimbashiria Imam Malik katika Hadith isemayo: “Inakurubia watu kupiga matumbo ya farasi wakitafuta ilimu, hawatapata mwanachuoni aliye mjuzi zaidi kuliko mwanachuoni wa Madina.”

Akambashiria Shafii katika Hadith: “Msiwatukane makuraishi kwani mwanachuoni wake ataijaza ardhi ilimu.” Akambashiria Abu hanifa kwenye Hadith: “Lau kama ilimu itakuwa imeangikwa juu ya Thureya wangeliifuata watu katika wafursi.”

Basi hapo hapo nikampigia simu Dkt, nikamsomea tafsiri mbili na kumuuliza: je, utaniruhusu nizinasibishe tafsiri hizi kwa masunni wote, niwafanye wao na Wahabiy kuwa ni sawa, kama ulvyofanya wewe kwa Shia kwa kuwa tu mmoja wao amesema?

Basihakunijibukituisipokuwa:Tamam tamam.(sawasawa).

  • 1. Pia aliwahi kuzungumzia mdundo wa ndani wa Qur’an. Tazama Juz. 22 (36:1-6).
  • 2. Sura 55:19