read

Aya 1 – 5: Msinyanyue Sauti Zenu Kuliko Sauti Ya Nabii

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakumbusha waumini mambo haya yafutayo:-

1. Enyi ambao mmeamini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Msifanye haraka kusema au kufanya tendo lolote linaoamabatana na dini na masilahi ya uma, mpaka alipitishe Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake mtukufu.

Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Katika Nahjul-balagha imeandikwa: “Mche Mwenyezi Mungu kwa baad- hi ya takua hata kama ni kidogo. Na weka sitara baina yako na Mwenyezi Mungu hata kama ni nyembamba.”

Kwa uchache kabisa wa mtu kumcha Muumba wake ni kujizuia kusema: Lau Mwenyezi Mungu angelihalalisha hili ambalo ameliharamisha au angeliharamisha lile alilolilihalalisha. Au kusema afadhali Nabii angeli- fanya hivi au asingelifanya vile alivyofanya na mengineyo ya ujeuri na ujinga.

2. Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii.

Si jambo zuri kuinua sauti bila ya dharura. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema: “Na uinamishe sauti yako. Hakika sauti mbaya zaidi ni ya punda.” Juz. 21 (31:19). Sikwambii tena ikiwa ni kuinua sauti mbele ya wakubwa na kwenye vikao vyao. Na Mtume mtukufu (s.a.w.) ni bwana wa manabii na mtukufu wa viumbe wote.

3. Wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaanguka, na hali hamtambui.

Mnapozungumza na Nabii msizungumze kama mnavyozungumza nyinyi. Mwenye kufanya hivyo atakuwa amebatilisha imani yake bila ya kutaka wala kujua. Na mwenye kubatilika imani yake ndio vimebatilika vitendo vyake na atakuwa mikononi mwa waliopata hasara.

Kwa hakika ambao wanateremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amezitia mtihani nyoyo zao kwa takua – yaani amezisafisha nyoyo zao kwa matendo mema - Hao watakuwa na maghufira na ujira mkubwa.

Mwenyezi Mungu huwajaribu waja wake kwa aina mbalimbali ya mitihani, ili apate mawaidha mwenye kuwaidhika na ajikanye mwenye kukanyika. Mwenye kuwaidhika na akawa na subira Mwenyezi Mungu humtakasa, humuongoza njia ya usawa na humneemesha kwa maghufira na ujira wa wenye kuwa na subira.

Aya inaashiria kwamba kuzungumza kwa adabu na kwa inavyotakikana ni katika imani. Imam Ali (as) anasema: “Imani ya mja hainyooki mpaka unyooke moyo wake na moyo haunyooki mpaka unyooke ulimi wake.

Hakika ambao wanakuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawana akili.

Mtume (s.a.w.) alikuwa na wake tisa, kila mmoja alikuwa na chumba chake kilichojengwa kwa makuti ya mtende, mlangoni kukiwa na pazia ya manyoya.

Wafasiri wanasema kuwa mabedui walikuja Madina na wakasimama nyuma ya vyumba vya Mtume wakaanza kuita kwa sauti: Ewe Muhammad (s.a.w.) tutokee! Mtume akangoja kidogo; kisha akawatokea. Mwenyezi Mungu amewataja kuwa wengi wao hawakujua walichokuwa wakikifanya, kutokana na ubedui na ushamba.

Na lau wao wangelingojea mpaka uwatokee ingelikuwa kheri kwao, kwa sababu kungoja na kutofanya haraka kuna malipo na thawabu, kumwdhimisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuchunga adabu.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu. Rehema yake inaenea kwa washamba, walalahoi n.k.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ {6}

Enyi mlioamini! Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda.