read

Aya 6: Akiwajia Fasiki Na Habari Yoyote, Ichunguzeni

Maana

Enyi mlioamini! Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda.

Imekuwa mashuhuri kwa wafasiri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimtuma Walid bin Uqba bin Abu Muit kwa Bani Mustaliq kuchukua Zaka, wakampokea kwa shangwe ya kumzunguka, lakini akadhania kuwa wanataka kumzuia.

Akarudi kwa Mtume (s.a.w.) na kumwambia: wamenizuia na kunifukuza. Basi Mtume (s.a.w.) akakasirika na baadhi ya swahaba zake wakamwambia tuwashambulie? Ndio ikashuka Aya hii kuwaondolea tuhuma Bani Mustaliq. Kuna sababu nyingine ya kushuka Aya hii.
Sisi hatutegemei lolote katika sababu za kushuka Aya ila ikithibiti kwa nukuu ya Qur’an au Hadith mutawatir. Zaidi ya hayo ni kuwa kudhania Walid shari hakuwezi kusababisha ufasiki; isipokuwa ni kukosea na kutatizika. Mwenye kukosea haitwi fasiki.

Vyovyote itakavyokuwa sababu za kushuka, lakini Aya haishilii kwenye sababu hiyo, bali inaenda mbali zaidi, kwa vile sababu haiwezi kuhusisha isipokuwa inaenea. Itakuwa sababu inatajwa kwa ajili ya jambo fulani ambalo halihusishi tamko. Kwa hiyo niwajibu kuichukulia dhahiri ya Aya, ambayo inafahamisha uharamu wa kuyachukulia maneno ya fasiki bila ya kuchunguza na kuthibitisha habari yake, kuhofia kuingia kwenye hatari; kama kuwadhuru wengine na kujuta, na majuto ni mjukuu.

Tunapata tafsiri ya Aya hii katika kauli ya Imam Ali (as): “Mwenye kufuata njia iliyo wazi atakunywa maji, na mwenye kuacha atahangaika.”

Kundi la masheikh wa kisunni na kishia wameitumia Aya hii kuwa ni dalili ya wajibu wa kuchukulia kauli ya mwenye kutegemewa bila ya sharti la kuchunguza ukweli wake. Baadhi yao wameitolea dalili kwa maneno ya undani yaliyojifungafunga.

Iko wazi kuwa Aya imechukua msingi wa kiujumla wa kupima habari ambayo haifai kuitegema ila baada ya uthibitisho na hiyo ni habari ya fasiki. Vile vile habari inayotegemwa bila ya uthibitisho ambayo ni habari ya mwenye kutegemewa.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameshartiza kuitegemea habari ya fasiki kwa ubainifu na uthibitisho, lakini hakuitaja habari ya mwenye kutegemewa. Lau ingelikuwa ni wajib kuichunguza habari ya mwenye kuaminika basi angeliitaja. Kwa kuwa haikutajwa basi sharti hiyo haipo.

Tuanavyo sisi ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni,” inafahamisha tu wajibu wa kuichunguza na kuithibitisha habari ya fasiki wala haifahimishi wajibu huo kwa habri ya mwenye kuaminika. Sisi tuko na wale wasemao kuwa kuitegemea habari ya mwenye kuaminika bila ya uchunguzi ni njia wanayoitumia wenye akili wa kale na wa sasa.

Hata hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda,” inafahamisha kuwa habari yoyote ambayo hatuna wasiwasi nayo kuingia katika matatizo na haramu, basi inafaa kuitumia bila ya kumwangalia mtoaji habari.

Kimsingi ni kuwa tusiamini habari ila ikiwa inatoka kwa mwenye kuaminika au tuithibitishe na kuichunguza ikiwa inatoka kwa fasiki.

وَاعْلَمُوا أَنَّ فِيكُمْ رَسُولَ اللَّهِ ۚ لَوْ يُطِيعُكُمْ فِي كَثِيرٍ مِنَ الْأَمْرِ لَعَنِتُّمْ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ {7}

Na jueni kuwa yuko kati yenu Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lau angeliwatii katika mambo mengi, bila ya shaka mngelitaabika. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akauchukiza kwenu ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka.

فَضْلًا مِنَ اللَّهِ وَنِعْمَةً ۚ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {8}

Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.