read

Aya 7 – 8: Mwenyezi Mungu Amewapendekezea Imani

Maana

Na jueni kuwa yuko kati yenu Mtume wa Mwenyezi Mungu na mtukufu wa wa mwanzo na wa mwisho. Basi ni juu yenu kumwadhimisha wala msimpe habari isipokuwa ya ukweli.

Lau angeliwatii katika mambo mengi, bila ya shaka mngelitaabika.

Hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ikielekezwa kwa wau- mini kuwa wamsikilize Mtume na wamtii, wala wasimshauri lile analolijua kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambalo wao hawalijui. Lau angeliwaitikia kwenye mambo mengi wanayomwambia wangelitaabika na kuingia kwenye tabu na dhambi.

Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akauchukiza kwenu ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka.

Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake wamwamini Yeye na wamtii, akawabainishia uzuri wa imani na utiifu, akatumia kila njia kuwahimiza hilo na akamwahidi malipo na thawabu kubwa mwenye kuamini na akatenda mema. Vile vile amewakataza ukafiri na uasi, akabainisha hasara zake na akamtishia kwa adhabu mwenye kukufuru na kuasi na akazisifia adhabu hizo kwa namna ambayo haiwezi kufikirika akilini ila baada ya kubainishwa. Ni mtu gani anayeweza kufikiria adhabu ambayo si mauti wala uhai.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatuma Mitume wake kwa watu ili wafikishe amri, makatazo ahadi na kiaga chake. Kuna wale wanaoitikia kihaki na kiukweli, wengine wakapinga na kufanya inadi na kuna wale waliotikia kuhofia masilahi yao na tamaa ya ngawira.

Wale waliomwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume kihaki na kiukweli ndio aliowakusudia katika kauli yake: “Amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu.” Yaani ameipendekeza na kuipamba kutokana na kueleza uzuri wa imani na kivutio cha thawabu nyingi. Akauchukiza ukafiri kwa kueleza mabaya yake na tishio la adhabu chungu. Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelibainisha hilo kwa waumini na makafiri, kwanini amehusisha kuwataja waumini, kinyume na wengineo?

Jibu: Ndio, lakini sio kila mwenye kusikia ubainifu wa Mwenyezi Mungu anauamini na kunufaika nao, wala sio kila mwenye kunasihiwa na Mwenyezi Mungu anakubali nasaha zake. Bali wema wamekubali na waovu wakakataa. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamtaja na kumsifu mwenye kusikia maneno akafuata mazuri yake na akampuuza mwenye kupinga na akaachana nayo.

Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kuchagua uongofu badala ya upotevu ana fadhila na malipo, lakini fadhila kubwa ni ya yule aliyemwandalia njia ya uongofu, akamwongoza na akampa uweza wa kuifuata. Walisema wakale: “Kama si sababu asingelifaulu msababishaji”

وَإِنْ طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِنْ بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّهِ ۚ فَإِنْ فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ {9}

Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hayo linadhulumu jingine, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirejea basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {10}

Hakika Waumini tu ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemiwe.