Aya 9 – 10: Na Ikiwa Makundi Mawili Katika Waumini Yanapigana
Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatan- isheni.
Uaislamu una mafunzo na miongozo ya kujenga jamii na kuitengeneza; miongoni mwayo ni wajibu wa kumlinda binadamu damu yake, mali yake, hadhi yake na uhuru wake wa kusema na kutenda. Hakuna yeyote mwenye utawala wa hayo isipokuwa haki. Akitoka kwenye haki na akaingilia haki ya wengine, basi hapo atakuwa amejiondolea kinga ya hayo yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema:
وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ {70}
Amesema tena kumwambia Mtume wake:
لَسْتَ عَلَيْهِمْ بِمُصَيْطِرٍ {22}
Akasema tena:
إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ {42}
Mafunzo mengine ya Uaislamu ni kuhurumiana na kusaidiana katika yale yaliyo na heri na masilahi kwa wote. Ikiwa itatokea uhasama baina ya makundi mawili ya waumini, basi wajibu wa waumini ni kusuluhisha kwenye misingi ya haki na uadilifu na kuchunga umoja usivunjike.
Kuna Hadith tukufu inayosema: “Je, niwaambie jambo lililo na daraja kubwa zaidi kuliko kufunga, kuswali na kutoa sadaka? Wakasema: Naam! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Ni kuwaunganisha waliotengana”
Na likiwa moja la hayo linadhulumu jingine, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu.
Ikiwa kundi moja litakataa kurudi kwenye haki na likang’ang’ania uchokozi, basi ni juu ya waumini wengine kulihami na dhulma lile kundi linaloonewa, kwa hekima na mawaidha mazuri. Ikiwa lile kundi ovu halitakoma ila kwa vita, basi lipigeni katika mipaka ya sharia inayohakikisha amani ya wote.
Na likirejea basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.
Likitubia lile kundi linaloonea na likaacha kabisa, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu, na hakuna atakayeruhusiwa kulifanyia lolote. Lililobaki ni wajibu wa waumini, kwa juhudi zao waondoe, yaliyotokea kwenye nafsi za pande mbili.
Al-Jassas Al-Hanafi, anasema katika Kitabu Ahkamul-Qur’an akiwa anazungumzia Aya hii: “Ali Bin Abi Twalib alipigana na kundi ovu kwa upanga akiwa pamoja na maswahaba wakubwa wa Badr (Ahlu Badr) waliojulikana. Na alikuwa ni mwenye haki. Hakuna aliyehalifu katika kundi kabisa isipokuwa kundi ovu na wafuaisi wake aliokuwa akipigana nao.”
Na akasema Abu Bakr Al-Malik, Maaruf kwa jina la Ibn –Al-Arabi Al- Muafiri, katika Ahkamul - Qur’an: “Imethibiti kwa maulama wa Kiislamu na imethibiti kwa dalili ya dini kwamba Ali Bin Abu Twalib alikuwa Imam na kwamba kila mwenye kupigana naye ni muovu na kupambana na mtu huyo ni wajibu mpaka arudi kwenye haki.”
Udugu Wa Kidini Na Udugu Wa Kibinadamu
Hakika Waumini tu ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
Hii ni kusisitiza kuleta suluhu baina ya pande mbili zilzigombana, pamoja na kuashiria kuwa upatanishi huu ni lazima kwa mfungamano wa udugu. Kuna Hadith isemayo: mwislamu ni ndugu wa mwislamu, hamdhulumu, hamtelekezi wala hamtii aibu.
Unaweza kuuliza: Kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: Hakika waumini tu ni ndugu, na asiseme: Hakika watu wote tu ni ndugu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) naye akasema:
“Mwislamu ni ndugu wa mwislamu.” Na asiseme: Mtu ni ndugu wa mtu? Tunajua kuwa Mola ni mmoja, asili ni moja, umbile ni moja na usawa baina ya watu ni wajibu. Kwa hiyo upendo unatakikana uwe ni wa jumla sio mahsusi; sawa na rehe- ma ambayo imekienea kila kitu?
Basi mgawanyo huu utakuwa na tofauti gani na ule unaowagawanya binadamu kwa misingi ya kiuchumi; walivyofanya wamarksi, au kuwagawanya kwa misingi ya kijinsia; kama walivyofanya wanazi au kwa misingi ya vita na silaha kama ilivyo siasa ya kimarekani?
Kisha nini kilichosababisha matatizo na maangamizi haya yanayomkabili binadamu leo, hadi kufikia kumalizana, baada ya binadmu kuweza kumiliki nguvu mbaya ya silaha za maangamizi? Je, hii imesabishwa na binadamu kama binadamu au imesabishwa na aina kwa aina za migawanyo?
Hatimaye sasa binadamu wasaidiane kwa misingi ya dini au asasi za kibanadamu?
Jibu: Maswali yote haya ni haki, na jibu lake ni moja tu litakoloweza kutosheleza maswali yote haya; nalo ni: Kusaidiana ni wajibu baina ya binadamu wote bila ya kubagua. Huu ndio mwito wa uaislamu hasa, unaofahamishwa na makumi ya Aya na riwaya. Tutatosheka kutaja Aya moja na riwaya moja.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 13 ya sura hii: “Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane. Hakika mtukufu zaidi yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi yenu.
Kwa hiyo mwito wake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Enyi watu!’ pamoja na kusema kwake: ‘Kutokana na mwanmmke na mwanamume’ na ‘aliye na takua zaidi’ ni dalili mkataa na wazi kuwa mwito wa Qur’an ni wa kiutu na wa mataifa, unamzingatia mtu ni ndugu wa mtu kwa namna yoyote itakvyokuwa itikadi yake, utaifa wake na jinsia yake.
Mfano wa Aya hii na ufafanuzi wake ni kauli yake Mtume mtukufu (s.a.w.): “Watu wote wako sawa kama chane za shanuo. Jueni kuwa hakuna ubora wa mwarabu kwa mwajemi wala wa mwajemi kwa mwarabu, wala wa mwekundu kwa mweusi wala wa mweusi kwa mwekundu isipokuwa kwa takua … nyote mnatokana na Adamu na Adam ametokana na mchanga.”
Zaidi ya hayo katika Juz.21 (30:30) kuna Aya inayosema kuwa uislamu ni dini ya maumbile na katika Juz. 9 (8:24) kuna Aya inayofahamisha kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni dini ya maisha.
Kwa hali hiyo basi inatubainikia kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake zinazingatia kuamini utu ni sehemu inayokamilisha kumwamini Mwenyezi Mungu, mitume wake na Vitabu vyake.
Kwa hiyo Makusudio ya mumin katika Aya na mwislamu katika Hadith ni yule anayeamwamini Mwenyezi Mungu na mtu kwa kuwa ni mtu.
Kwa maneno mengine ni kuwa hakuna mzozo wala kupingana baina ya udugu wa kibinadamu na udugu wa kiislamu; huu wa kiislamu unauongeza nguvu ule wa kibinadamu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِنْ قَوْمٍ عَسَىٰ أَنْ يَكُونُوا خَيْرًا مِنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِنْ نِسَاءٍ عَسَىٰ أَنْ يَكُنَّ خَيْرًا مِنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنْفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَنْ لَمْ يَتُبْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {11}