read

Aya 11: Kaumu Isidharau Kaumu Nyingine

Enyi ambao mmeamini! Kaumu isidharau kaumu nyingine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake kwa wanawake wengine, huenda wakawa bora kuliko wao.

Imesemekana kuwa neno Qawm, tulililofasiri kwa maana ya kaumu, kwa maana yake ya kiarabu huwa halitajwi ila kwa wanaume tu, kwa dalili ya kuunganishwa wanawake baada ya neno hilo.

Katika Juz. 19 (25:55-62) tulisema kuwa dhalimu kesho atachukuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni kafiri ingawaje duniani anachukuliwa kuwa ni mwislamu kama akitamka shahada mbili.

Na mwenye kuwadharau wema atakuwa ni dhalimu na safihi.

Hili Mwenyezi Mungu amelikemea kwa ukali sana; kama aliposema:

 فَيَسْخَرُونَ مِنْهُمْ ۙ سَخِرَ اللَّهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {79}

“…Wakawafanyia maskhara; Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo. Juz. 10 (9:79).

Pia kauli yake:

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ {29}

وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ {30}

وَإِذَا انْقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انْقَلَبُوا فَكِهِينَ {31}

وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ {32}

وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ {33}

فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ {34}

“Hakika wale walio na hatia walikuwa wakiwacheka wale ambao wameamini. Wakiwapitia wanakonyezana na wakirudi kwa watu wao walirudi wakishangilia… Basi leo wale ambao wameamini wanawacheka makafiri” (83: 29-34).

Vile vile amesema:

وَيْلٌ لِكُلِّ هُمَزَةٍ لُمَزَةٍ {1}

“Ole wake kila mtia kasoro mwenye kusengenya.” (104:1).

Vipi Utapata Marafiki?

Nimekumbuka, wakati nikifasiri Aya hii, kwamba kiasi cha mika 16 au zaidi iliyopita nilisoma tarjuma ya kitabu: How to win friends and influ- ence people (vipi utapata marafiki na kuathiri nafsi) cha Dayl Karengi.

Vile vile nimekumbuka hekima ya hali ya juu ya Imam Zainul’abidin, inayohusiana na maudhui hii ambayo ina athari zaidi ya kitabu nilichoki- taja pamoja na kuwa kimeenea sana na kufasiriwa kwenye lugha nyingi.

Imam, kwenye hekima yake, alikuwa akikusudia kauli yake Mwenyezi Mungu: “Kaumu isidharau kaumu nyingine, huenda wakawa bora kuliko wao.” Hekima yenyewe ni hii:

“Jihadhari na kuzungumza ambayo moyo unayakanya hata kama una udhuru. Kwani sio kila utakayemwambia shari unaweza kumfafanulia udhuru. Aliye mkubwa kuliko wewe muweke daraja ya mzazi, mdogo daraja ya mtoto, na aliye marika daraja ya kaka. Ni nani katika hawa unapenda kumvunjia heshima yake?

“Ikiwa shetani atakuingilia kujiona kuwa u mbora zaidi ya mwingine, angalia haya yafutayo: Ikiwa ni mkubwa zaidi yako, sema: amenitangulia kwa imani na matendo mema, kwa hiyo ni bora kuliko mimi. Ikiwa ni mdogo kuliko wewe, sema: nimemtangulia kwa maasi, kwa hiyo yeye ni bora kuliko mimi. Akiwa ni marika yako sema: mimi nina uhakika nimefanya dhambi, lakini nina shaka kuwa yeye amefanya dhambi, basi kwanini niache uhakika nichukue shaka?

“Ukiwaona watu wanakutukuza, sema: wamechukulia wema, na ikiwa wanakutenga, sema: kuna makosa nimefanya.”

Imam anaendelea kusema: “Ukiyafanya haya maisha yako yatakuwa mepesi, utakuwa na marafiki wengi na utakuwa na maadui kidogo, na utafurahi kwa wema wao wala hutasikitika kukutenga.”

Vyovyote watavyosema maulama na wenye hekima kuhisiana na maudhui haya, hawatazidisha kitu kwenye hekima hii fasaha ya hali juu.

Hilo si ajabu kwa vile aliyeisema ni mtoto wa wahyi, hazina ya ilimu ya wahyi na aliyekulia kwenye malezi yake.

Wala msitiane kasoro.

Msitiane ila wala msiwambie wengine lile ambalo hampendi kuambiwa.

Wala msiitane majina ya kejeli.

Mtu asimwite mwenzake kwa jina analolichukia. Mafaqihi wamesema kuwa ikiwa jina halikukusudiwa kasoro wala dharau na ni mashuhuri wa hilo, basi halina ubaya; kama vile Hassan Madafu, n.k.

Ni uovu kutumia jina baya baada ya imani.

Hapa kuna tafsiri mbili: Ya kwanza ni msimwite mumin ewe kafiri! Ya pili, ni uovu huko kumwita mwingine kwa jina asilolipenda. Tafsiri hii ina ngvuvu, kwa wafasiri wengi kuliko ile ya kwanza.

Na wasiotubu, hao ndio madhalimu.

Mwenye kutubia ni kama asiye na dhambi na mwenye kung’ang’ania dhambi atakuwa ameidhulumu nafsi yake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu atawaadhibu wenye dhambi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَبْ بَعْضُكُمْ بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَنْ يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ رَحِيمٌ {12}

Enyi ambao mmeamini! Jiepusheni na dhana nyingi. Hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipeleleze, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.