Aya 12: Dhana, Ujasusi Na Kusengenya
Maana
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekataza dharau, kutia ila, kubeza na kuitana majina ya kuchukiza. Na akamkemea mwenye kufanya moja katika hayo. Katika Aya hii anakataza dhana mbaya, ujasusi na kusengenya. Ufafanuzi ndio huu ufuatao:-
Dhana
Enyi ambao mmeamini! Jiepusheni na dhana nyingi. Hakika baadhi ya dhana ni dhambi.
Sehemu hii ya Aya inawezekana kufanyiwa muhtasari kwa jumla moja tu: “Kila mtu hana hatia mpaka lithibitike kosa lake.”
Inawezekana jumla hii kuifafanua kwa urefu, tuweke mpaka wa linalopelekea asili ya dhana, kuwa je, inafaa kuichulia dhana au kuna wajibu wa kujieupusha wakati wote au wakati wa kuweko udhuru na wa kutokuweko ilimu? Na je, kuna udhuru wa kutojua au hakuna?
Ikiwa inafaa kuichukulia dhana, je, tuichukulie dhana vyovyote ilivyo sababu yake na mfungamano wake? Na ikiwa haifai kuichukulia dhana kwa namna yote ile, je ni nyenzo gani za ilimu kwenye hukumu ya sharia na mengineyo katika ilimu ya usul (misingi ya sharia) ambayo tumeimalizia miaka si kidogo kuisoma?
Ni vizuri tuchuke tafsiri ya wastani si kurefusha wala kufupiliza. Kabla ya lolote ni lazima tufanye maandalizi ya kujua toafauti baina ya shaka, dhana na ilimu. Shaka ni kuwa sawa uthibitisho na ukanusho. Dhana ni kuwa na nguvu upande mmoja baina ya hizo mbili, lakini bado kunakuwa na uwezekano kwa upande ule usio na nguvu. Ilimu ni kubainika upande mmoja unaofunga kabisa njia ya upande mwingine.
Unaweza kumdhania mtu heri au shari, ukawa umepatia au umekosea katika dhana yako. Hakuna ubaya kabisa ikiwa utamdhania mwenzako heri, iwe umepatia au umekosea; au iwe litajitokeza hilo kwenye kauli yako na vitendo vyako au lisijitokeze.
Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Wadhanieni waumini heri.” Imam Ali (as) anasema: “Liweke jambo la nduguyo kwenye heri.” Tazama Juz. 1 (2:83) kifungu cha ‘Kuchukia usahihi.’
Kwa hiyo basi inatubainikia maana ya kuwa kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: “Jiepusheni na dhana nyingi,” na wala asisema ‘jiepusheni na kila dhana.’
Neno wingi huwa pia linatumiwa kwa maana ya baadhi; na haya ndiyo Makusudio yake kwenye Aya hii; yaani jiepusheni na dhana mbaya.
Dhana mbaya yenyewe sio haramu ikiwa haitajitokeza kwenye kauli au kitendo, wala mwenye dhana hiyo hana majukumu yoyote. Lakini ni lazima asiitolee maamuzi yoyote na aifanye kama haiko. Akiitolea uamuzi na ikajitokeza athari yake kwenye kauli au kitendo, basi atawajibika na atastahili lawama na adhabu.
Hii ndio dhana aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema: “Hakika baadhi ya dhana ni dhambi.”
Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Mambo matatu hasalimiki nayo yeyote: Kisirani, hasadi na dhana: Ukiona kisirani endelea, ukiona husda usiitake, na ukidhania hakikisha. Kwa hiyo basi maana ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Jiepusheni na dhana nyingi’ nikuwa msizitolee maamuzi wala msizitumie; sawa na kauli yake “Asiwafitini shetani.”
Ujasusi
Wala msipeleleze.
Kupeleleza ni kuchunguza siri na makosa kwa njia ya kujificha. Ni haramu kwa Kitabu, Sunna, Ijmai (kongamano la maulama) na kiakili. Na kauli yake:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا {27}
فَإِنْ لَمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ ۖ {28}
Katika Sunna ni Hadith ya Mtume mtukufu (s.a.w.): “Mwenye kukuchungulia ukamtupia kijiwe na ukamtoboa macho yake, basi huna lawama.” Mafaqihi wamekubaliana kwa pamoja kuitumia Hadith hii. Ama akili inauona ujajusi ni vita dhidi ya maisha ya watu na kuingilia uhuru wao na mambo yao yanayowahusu katika mila na desturi.
Nimekumbuka, wakati nikiandika maneno haya, makala ndefu kuhusu maudhui haya, iliyotolewa na gazeti Al-Ahram la 27-6-1969, nililisoma wakati huo, kisha nikalihifadhi katika mafaili ya magazeti. Nililihifadhi na kuliweka akiba ya kulitumia nikilihitajia. Basi nikalisoma tena, mara nikaona mambo ambayo hata kuyawaza tu ni muhali; baadhi yake ni haya yafuatayo:
“Wamarekani hivi sasa wanajua kuwa sio kuwa kuta zao zina masikio tu, bali zina macho na mboni vile vile, kama lilivyosema gazeti la Times. USA wametengeneza kifaa kidogo cha ukubwa wa milimita, kinachoweza kusajili mazungumzo; na mtu anaweza kukiweka kwenye jaketi kama kifungo. Kila mtu anaweza kukitumia na kinagharimu kati ya dola 10 na 15.
Huko New York, wafanyabiashara wameweka matangazo ya biashara kwenye magazeti kuuza vifaa vya kurikodi mazungumzo ya watu majumbani mwao na wanaviuza madukani kama michezo ya watoto. Bei yake haizidi dola 18.
Mtu akiweka kifaa hiki kwenye gari kikielekezwa kwenye jengo basi kitarikodi kila neno linalosemwa kwenye jengo lile. Bali kuna kifaa cha kusikilizia maneno kisichozidi ukubwa wa punje ya choroko, kinachoweza kuwekwa kwenye kalamu nk, kinatumia betrii ya masaa 18 hadi 50.
Pia wametengeneza kifaa kidogo cha kutuma, kinachoweza kutangaza yanayopita kwenye majumba kwa umbali wa futi 50 na bei yake ni dola 400.
Ajabu ya yote ni kamera zinazopenya ukutani na kupiga picha mambo yote anayoyafanya mtu chooni na hata kwenye giza. Vile vile inawezekana kuchora chale (tattoo) katika mwili wa mtoto wakati anapozaliwa ambayo itafuatilia harakati zake katika maisha yake yote.
Kuna shirika katika Marekani yote linalokusanya habari na harakati binaf- si za watu mashuhuri wa siasa, elimu, uandishi uchumi na wengineo na kurikodi maneno yao, na kupiga picha ya vitendo vyao, hata wanapofanya tendo la ndoa na wake zao na wengineo. Mtu anaweza kupata habari hizi kwa dola moja tu. Shirika hili linaitwa Benki ya habari.
Yote hayo yanatokea ikiwa serikali inajua kila kitu, bila ya kufanya lolote, kwa sababu imekuwa ni jambo la kawaida kama vile kuuza magazeti tu.” Mwisho wa nukuu ya gazeti.
Haya ni machache katika mengi. Watunzi wameandika vitabu maalum kuhusiana na maudhui haya. Lau wamarekani wangeliyafanya haya kwao tu wenyewe kwa wenyewe, tungeliwaambia wao na wanowatawala: “shauri yenu, kila mji una uhuru wa kujichagulia unavyotaka.” Lakini wamarekani wamevuka mipaka, wanafanya ujasusi kwenye nchi nyingine kwa ndege na satalaiti.
Usishangae msomaji. Marekani ni nchi ya maendeleo, demokarasia, bwana mkubwa wa uhuru, na polisi wa ulimwengu.
Tena zaidi ya hayo wanaamini Mwenyezi Mungu… Dalili kubwa kuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ni mauaji ya kinyama waliyoyafanya kwenye kijiji kimoja katika Vietnam ya kusini1, na kuwasheheneza silaha za kisasa mayahudi ili kuwamaliza wananchi wa Palestina, kuwaua watoto kwa ujumla na kutupa mabomu kwa kutumi ndege za Phantoum kwa watoto wa shule wa Misr! Kweli kabisa USA ni dola kubwa kwenye uwanja huu wa mauaji!
Kusengenya
Wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Kusengenya ni kumtaja mtu kwa jambo asilolipenda. Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Kusengenya ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia. Ikiwa jambo hilo analo huko ni kusengenya na ikiwa hana itakuwa ni kumsingizia.” Na kusingizia ni kukubwa zaidi kuliko kusengenya na kumeharamishwa kwa Kitabu Sunna na Ijmai (kongamano la maulama).
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemfananisha mwenye kusengenywa na maiti kwa vile anakuwa hayupo na akaifananisha hishima yake na nyama yake na kumtaja kwa uovu kuwa ndio kula.
Maana ya mnalichukia hilo ni kuwa ikiwa mnaona kinyaa kula nyama ya maiti basi pia muone kinyaa kumsengenya asiyekuwepo, kwa sababu yote mawili hayo yako sawa.
Hakuna jambo linalofahamisha kupungukiwa na udhalili kuliko kusengnya. Imam Ali (as) anasema: “Kusengenya ni juhudi ya asiyejiweza.” Na Mwenyezi Mungu hasamehi kusengenya mpaka asamehe aliyesengenywa. Mafaqihi wameuvua uharamu wa kusengenya kwa wafuatao:-
Mpagani, hakimu dhalimu, mwenye kuudhihirisha ufuska wake, kwa sababu mwenye kulitupa joho la haya hana cha kuficha, kumpa ushauri mwenye kutaka ushauri katika kushirikiana na mtu au kumwakilisha kwenye jambo muhimu, kumtengua shahidi kwa kadhi, na mwenye kudhulumiwa kwa yule aliyemdhulumu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
لَا يُحِبُّ اللَّهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَنْ ظُلِمَ ۚ وَكَانَ اللَّهُ سَمِيعًا عَلِيمًا {148}
Juz. 6 (4:148).
Katika Kitabu Al-Makasib cha Sheikh Ansari, imesemwa kuwa sehemu zinazoondolewa uharamu wa kusengenya hazina idadi. Kwa sababu kusengenya kunakuwa haramu ikiwa kutangaza huko hakuna masilahi yenye nguvu. Vinginevyo, basi itakuwa wajibu kutangaza na kueneza kwa kuangalia masilahi yenye nguvu zaidi, kama ilivyo katika kila maasi ya haki za Mwenyezi Mungu na haki za binadamu.Tazama mwanzo wa Juz. 6
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنْثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ {13}
قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا ۖ قُلْ لَمْ تُؤْمِنُوا وَلَٰكِنْ قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ ۖ وَإِنْ تُطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُمْ مِنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {14}
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ {15}
قُلْ أَتُعَلِّمُونَ اللَّهَ بِدِينِكُمْ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {16}
يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا ۖ قُلْ لَا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُمْ ۖ بَلِ اللَّهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {17}
إِنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {18}
- 1. Kijiji kisichokuwa na hatia kilichokuwa na wakazi 500, wengi wao wakiwa ni wazee, wanawake na watoto. Wanajeshi wa Mareknai waliwaua wote kwa unya- ma bila ya kubakia yoyote. Hatia hii ilifanyika mwezi wa tatu 1968.