read

Aya 13 – 18: Mtukufu Zaidi Yenu Ni Mwenye Takua Zaidi

Maana

Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane. Hakika mtukufu zaidi yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari.

Watu wanajua kuwa baba yao ni Adam na mama yao ni Hawa, lakini lengo la kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Tuewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke, ni kuwa watu wote wajue kwamba wao ni ndugu ni udugu wa usawa katika haki na wajibu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu; “Ili mjuane,” ni kuwa Makusudio ya kutofautiana kwenu katika miji, nasaba na rangi, sio kuwa muwe vikundi, mchinjane na mjifaharishe kwa mataifa yenu, baba zenu na jinsi zenu, hapana! Sivyo kabisa.

Lengo ni muhurumiane na msaidiane katika yale yaliyo na heri yenu na masilahi yenu. Na mbora kabisa atakuwa yule anayemuogopa Mwenyezi Mungu zaidi na akawanufaisha waja wake.

Aya hii ni mwito kutoka kwenye Qur’an kuwa watu wawe umma mmoja wa kiutu na ulimwengu mmoja unaokusanywa na uadilifu na upendo. Ulimwengu huu ni tegemeo la wenye fikra safi na ni ndoto ya walio wema.
Tuna uhakika kuwa makubaliano ya haki za binadamu, yatabakia kwenye karatasi na yatakuwa ni nadharia tu, ikiwa hautapatikana umoja wa ubinadamu uliotolewa mwito na Qur’an, zaidi ya mika 1300 liliyopita. Amerika na Israil zilitia saini makubaliano ya haki za binadamu, lakini bado ndio za kwanza kuangamiza watu Vietnam na Palestina.

Leo ninapoandika maneno haya 22 April 1970, kamati ya umoja wa mataifa imehakikisha kuwa Israil imevunja haki za binadamu, ikasema waziwazi kuwa Israil imevunja majumba ya wakazi ikaacha miili ya wanaume, wanawake na watoto kwenye kifusi na ikakataa isizikwe. Pia imevunja sehemu takatifu na mahospitali1 na kuwaadhibu wenyeji kwa umeme. Watu wazima wanawang’oa viungo, watoto wanawakata mikono na kupasua matumbo yao mbele ya baba zao na mama zao na mengineyo ya kinyama na mauji ya maangamizi.

Mabedui walisema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatawapunguzia chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Makusudio ya uaislamu hapa ni kutamka shahada mbili. Katika Juz. 1 (2:82), tumetaja tofauti baina ya mumin na mwislamu. Hapa tutamnukuu Dkt Twaha Hussein katika kitabu Mir’atul-islama (Kioo cha uaislamu).

Yeye ni mwanafasihi anayefahamika kwa siri za fasihi, ninamnukuu: “Wakati wa Mtume kulikuweko waumini na waislamu. Basi, niipi tofauti baina imani na Uislamu? Imani kwa dhahiri ya Aya hii ni jambo lilio moyoni ambalo mihimili yake ni ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na kusadikisha, kwa kina ndani ya dhamiri, kila aliloletewa wahyi Mtume.

Natija ya imani hii ni kumwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume katika kila wanalolitolea mwito, bila ya kigugumizi, kugwazagwaza, wala kutaradadi, kwa hali yoyote ile itakavyokuwa; iwe kuna matukio au majanga. Mhimili mwingine wa imani hii ni kumwogopa Mwenyezi Mungu kiundani kabisa likitajwa jina lake na kumtegemea kwa undani zinaposomwa Aya zake.

“Ama Uislamu ni twaa ya dhahiri ya kutekeleza wajibu na kujiepusha na yaliyokatwaza; hata kama haitafikia imani ya kweli. Kuna watu wanaosilimu kuhofia ubaya; kama walivyosilimu makuraishi walioachwa bila ya kutekwa nyara siku ya kutekwa Makka. Wengine walasilimu kwa hofu na tamaa; kama walivyofanya mabedui aliowataja Mwenyezi Mungu katika Aya hii.”

Hakika Waumini ni wale tu waliomamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasiwe na shaka, na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.

Waumini wa kwelikweli kabisa ni wale wasiokuwa na shaka yoyote kwenye itikadi zao na wanaojitolea kihali na mali, kuihakikisha haki na kuibatilisha batili. Umetangulia mfano wake mara kadhaa; miongoni mwazo ni Juz. 10 (9:88).

Sema: Je, mnamjulisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu?

Mabedui walisema tumeamini, ndio Mwenyezi Mungu anawajibu, kuwa hivi mnamjulisha Mwenyezi Mungu imani yenu na hali Yeye anajua siri na yaliyofichika; kila kitu amekizunguka. Tena je imani inakuwa kwa kudai? Inatosha kuwa mtu ni mjinga kuwa hajui uweza wake Mwenyezi Mungu.

Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye anayewasimbulia kwa kuwaongoza kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.
Makusudio ya kusimbulia kwake Mwenyezi Mungu ni kuwafanyia hisani, kwa sababu Yeye amekataza masimbulizi, na hawezi kukataza jambo kisha alifanye. Makusudio ya kuongoza kwake kwenye imani ni kutoa mwongozo wa haki na kuipendekeza.

Maana ni kuwa mabedui na walio mfano wao wanaona kuwa wamemfanyia hisani Mola wao na mtume wao kwa dini yao na wanataka walipwe; hali yakuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewafanyia hisani wao, pale alipowaongoza kwenye haki na kuwahimiza kupitia Mtume wake.

Kwa hiyo wao ndio wamshukuru kwa alivyowafanyia hisani na kuwaneemesha; sio wao wasimbulie na kutaka kulipwa; ikiwa kweli wameamini dini yao na wakafanya ikhlasi kwenye imani yao. Vinginevyo watakuwa wanastahili kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale aliyowaandalia waongo na wahaini.

Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua imani ya kweli na ya uwongo na kuzipamabanua amali zilizokusudiwa dunia na zile zilizokusudiwa radhi ya Mwenyezi Mungu. Aina zote za amali pamoja na imani au kufuru ndio kipimo cha uadilifu wa hisabu na malipo.

  • 1. Na leo ninapofasiri maneno haya January 2009. Israil imeyarudia hay ohayo huko Gaza. - Mtarjumu