Aya 1 – 11: Naapa Kwa Qur’an Tukufu
Maana
Qaf.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Naapa kwa Qur’an tukufu!
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa Qur’an kudhihirisha ukuu wake, na ameisifu ni tukufu kwa wingi wa manufaa na faida zake.
Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!
Ndio, ni ajabu katika mantiki ya wale wanaoona kila kitu ni mali, wala hawaoni ubora wowote isipokuwa benki na ardhi.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 11(10:2). Juz. 23 (38:4-5).
Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!
Walikana ufufuo kwa sababu wao wanashindwa kuuelewa. Sisi tunaamini kushindwa kwao kuuelewa, lakini je, kushindwa kwao kulitambua jambo, ni dalili ya kutokuweko?
Ni mwenye akili gani anayechukia kushindwa kwake kuelewa kitu kuwa hakipo?
Kutatizika kwao kulikotokana na kutojua huku, walikokubainisha kwa kusema: “Ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imemung’unyika? Mwenyezi Mungu naye akawajibu:
وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَنْ يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ {78}
قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنْشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ {79}
Juz. (36:78-79).
Maana haya yamekaririka kwenye Aya kadhaa.
Hakika tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinachohifadhi.
Kitabu kinachohifadhi ni kinaya cha kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amekizunguka kila kitu kwa ujuzi. Aya hii ni jawabu la kutatizika kulikofanya wakanushe ufufuo. Ufafanuzi wake ni kuwa mwili wa mtu unaliwa na ardhi baada ya mauti na unakuwa chembechembe zinazotawanyika mashariki mwa ardhi na magharibi yake. Vipi zitakuswanywa na kurudishwa ulivyokuwa?
Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba Yeye anajua kwamba ardhi inakula mili ya wafu na kwamba inatawanyika mashariki mwa ardhi na magharibi yake, lakini pamoja na hayo Yeye anaweza kuikusanya na kuirudishia uhai wake.
Mwenye Kula Na Mwenye Kuliwa
Wanafalsafa na wanatheologia wanakuita kutatizika huku ni kutatizika kwa ‘mlaji na mwenye kuliwa.’ Mulla Sadra amekutaja katika Juzuu ya nne ya kitabu chake, Al-asfar akasema: “Wametoa hoja kuwa: Ikiwa mtu atamla mtu mwingine, sehemu zilizoziliwa zikirudishwa kwenye mwili wa aliyekula hazitakuwa ni za aliyeliwa, na hapo atakuwa aliyeliwa ama ataadhibiwa au ataneemeshwa kutegemea na aliyemla.
Hayo yamejibiwa katika vitabu vya theologia kwamba ufufuo utakuwa kwa viungo vyao vile vilivyoanza kuumbwa ambavyo ni viungo vya asili kwao; na Mwenyezi Mungu anafihifadhi wala havifanyi ni viungo vya mwingine.”
Anaendelea kusema Mulla Sadra kwamba jawabu hili halitoshi. Ukweli ni kuwa kila linalowezekana kiakili na likafahamishwa na wahyi, ni wajibu kuliamini. Na ufufuo ni jambo linalowezekana kiakili na limethibiti kiwahyi. Kwa hiyo niwajibu kulisadiki na kuliamini. Ama wanafalsafa na watu wa mantiki sio maasumu.
Haya ndiyo aliyoyasema mwenye Al-asfar, nayo ndiyo tuliyoyategemea na kuyataja mara kdhaa huko nyuma. Masheikh wamejaribu kuthibitisha ufu- fuo wa kimwili kwa hukumu ya kiakili bila ya kuangalia wahyi, lakini hawakuzidisha ispokuwa uzito na kutatiza.
Lakini waliikadhibisha haki ilipowajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.
Makusudio ya haki ni Qur’an. Mwenyezi Mungu ameita, mkorogo hali ya wale waliomwambia Mtume kuwa ni mwenda wazimu, mara ni mchawi, tena ni kuhawani na hata pia wakamwita mshairi. Huko ndikokukorogeka na kuchanganyikiwa hasa.
Je, Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazi- pamba wala hazina nyufa.
Makusudio ya kujenga hapa ni kuwa sayari za mbinguni zimepangiliwa kihekima katika kutengenezwa kwake, zimetulia kwenye nidhamu yake na zinakwenda kwa uhakika. Makusudio ya kuzipamba ni uzuri. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Hazina nyufa’ ni kuwa kila sayari katika sayari zake hakuna yenye kasoro; kama alivyosema:
هَلْ تَرَىٰ مِنْ فُطُورٍ {3}
Maana ni kuwa wakadhibishaji hawoni ufufuo kuwa jengo la sayari halifanani na jengo lolote la binadamu. Kwa sababu sayari kadiri itakavyokuwa kubwa, lakini inakuwa ni kitu kimoja kisichokuwa na maunganisho, lakini wajenzi huwa wanaweka tofali juu ya tofali jingine, kati yao kuna utengnisho na mistari, nao hawawezi kujenga jengo kubwa kama hilo la sayari.
Aya hii ni majibu wazi na hoja ya kumnyamzisha yule anayeiweka mbali na kuishangaa fikra ya ufufuo na kusema: “Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!”
Majibu yenyewe ni kuwa yule ambaye ameumba sayari bila maunganisho hawezi kushindwa kumfufua mtu baada ya kufa kwake. Kwa sababu hili ni jepesi zaidi kuliko hilo:
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ {57}
Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.
Yaani tumeitandaza na tukaifanya iwe sawa kwa ajili ya binadamu, tukaweka humo milima ili isiyumbe na tukaotesha aina mbalimbali za mimea inayopendeza kuiona na yenye uzuri wa kuliwa.
Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.13 (13:3).
Yawe ni busara na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ulimwengu na yaliyomo ikiwemo nidhamu na mpangilio ili iwe ni ishara ya ukuu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mwenye busara na mazingatio. Hapo kuna ishara kuwa mfungamano wa mtu na ulimwengu anaoishi hauishii kwenye maada tu, bali ni kwa moyo pia.
Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyaita maji yenye baraka, kwa vile hakuna uhai wa roho wala viwiliwili bila ya maji. Na ameiita mitende mirefu kuashiria kuwa wakati wa kuota mitende inakuwa midogo, kisha inakuwa kwa sababu ambazo Mwenyezi Mungu amezipa maumbile.
Imam Ali (as) anasema: “Haikufahamisha dalili ila kwamba muumba wa chungu ndiye muumba wa mtende kwa umakini wa kukipangila kila kitu.” Yaani umakini wa mpangilio wa kutengenezwa chungu na mtende mkubwa unajulisha kuwa muumba ni mmoja.
Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Kwa vile hawawezi kujiruzuku wenyewe. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyokuwa imekufa.
Hii ni mwanzo wa kusema Kama hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuo.
Kwa hiyo kufufua watu baada ya mauti ni sawa na kuufuua kwa maji mji uliokufa. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama vile Juz. 8 (7:57).
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ {12}
وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ {13}
وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ ۚ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ {14}
أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ ۚ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ {15}
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ {16}
إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ {17}
مَا يَلْفِظُ مِنْ قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ {18}
وَجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ۖ ذَٰلِكَ مَا كُنْتَ مِنْهُ تَحِيدُ {19}
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْوَعِيدِ {20}
وَجَاءَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَعَهَا سَائِقٌ وَشَهِيدٌ {21}
لَقَدْ كُنْتَ فِي غَفْلَةٍ مِنْ هَٰذَا فَكَشَفْنَا عَنْكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ {22}