read

Aya 12 – 22: Kwani Tulichoka Kwa Kuumba Kwa Kwanza?

Maana

Walikadhibisha kabla yao yaani kabla ya Muhammad (s.a.w.) kaumu ya Nuh

Kimetangulia kisa cha Nuh katika Juz. 12 (11:27-31).
Na watu wa Rassi.

Rassi ni kisima. Imetangulia ishara yao katika Juz. 19 (25:30-40).

Na Thamudi.

Hao ni watu wa Swaleh. Kisa chao kiko Juz. 12 (11:61-68).

Na A’di.

Hao ni watu wa Hud. Yametangulia masimulizi yao kwenye Juz. 12 (11:50-56).

Na Firauni.

Kisa chake pamoja na Musa na wana wa Israil, kimekaririka mara nyingi; miongoni mwazo ni Juz. 9 (7:103-112).

Na ndugu wa Lut.

TazamaJuz.8(7:80-84).

Na watu wa Machakani.

Imetangulia ishara yao katika Juz. 19 (26:176-191).

Na watu wa Tubbaa’.

Yametangulia maelezo yao katika Juz. 25 (45:37).

Wote waliwakanusha Mitume, kwa hivyo kiaga kikathibitika juu yao.

Hiyo ni adhabu ambayo Mwenyezi Mungu aliwaahidi kupitia Mitume wake.

Kwani tulichoka kwa kuumba kwa kwanza mpaka tuchoke na kuumba kwa pili?

“Kama tulivyoanza umbo la kwanza, tutalirudisha tena.” Juz. 17 (21:104).

Bali wao wamo katika shaka juu ya umbo jipya.

Umbo jipya ni ufufuo. Shaka ni nzuri, bali wakati mwingine ni dharura, ikiwa ni ya kufanya utafiti na kuchunguza, lakini kukanusha bila ya dalili na kutia shaka tu, huo ni ujinga na upotevu.

Na hakika tumemuumba mtu, na tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingo.

Mwenyezi Mungu yuko karibu na kila kitu kwa kujua kwake, kwa sababu hakuna chochote ila kimetokana na Yeye. Kwa hiyo hakuna kitu kilicho mbali naye. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja mshipa wa shingo kwa vile uko karibu na mtu kuliko kiungo chochote kingine; kuongezea kuwa ni mhimili wa maisha.

Wanapopokea wapokeaji wawili, walioko kuliani na kushotoni. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu anamwekea mtu waangalizi wawili; mmoja akiwa upande wa kulia na mwingine wa kushoto wakisajili kila analolitamka. Wafasiri wengi wamesema kuwa waangalizi hawa wawili ni malaika na kwamba yule wa kulia anaandika mema na yule wa kushoto maovu.
Pia inafaa kufasiri kuwa wawili hao ni kinaya cha kuwa mtu ataulizwa anayoyasema na anayoyafanya na kwamba yeye wakati wa hisabu hawezi kuficha au kupinga lolote katika uovu wake, kwa kuweko hoja juu yake.

Tumesema kuwa inafaa tafsiri hii kwa vile inaenda pamoja na ile ya kwanza inayofahamika kutokana dhahiri ya Aya, na natija zao ni moja.

Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu kwa ilimu yake hana haja ya waangalizi na waaandishi. Sasa kuna Makusudio gani ya kuwaweka waangalizi?

Jibu: Makusudio ni kuwakabili Mwenyezi Mungu wakosefu kwa lile ambalo hawatakuwa ni hila wala njia ya kulikana. Na kwa mbali Aya inaashiria kuwa haifai kwa kadhi kuhukumu kwa kulijua kwake jambo. Tazama Juz. 24 (41:20).

Na uchungu wa mauti utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.

Uchungu wa mauti ni uchungu wa kutoka roho. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ‘kwa haki,’ inaashiria kuwa wakati wa kufa, uhakika utamfunukia yule mwenye kukata roho na atajua kwa uhakika kwamba ufufuo ni kweli isiyo na shaka. Neno ‘hayo’ ni ishara ya hayo ya kufufuliwa. Maneno hapa yanelekezwa kwa yule anayekana ufufuo. Makusudio ya kukimbia ni kukana.

Maana ni kuwa ataambiwa yule anayekana ufufuo wakati anapokata roho: huu ndio ufufuo uliokuwa ukiukana. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

هَٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ الَّذِي كُنْتُمْ بِهِ تُكَذِّبُونَ {21}

“Hii ndiyo Siku ya upambanuzi mliyokuwa mkiikadhibisha.” Juz. 23 (37:21).

Na itapulizwa parapanda. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria Kiyama:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُمْ مِنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنْسِلُونَ {51}

“Na itapulizwa parapanda mara watatoka makaburini wakikimbila kwa Mola wao.”
Juz. 23 (36:51).

Na itakuja kila nafsi pamoja na na mpelekaji na shahidi.

Mpelekaji ni wakuipeleka kwenye mkusanyiko na shahidi ni yule atakayeshuhudia matendo yake.

Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

‘Haya,’ ni haya ya hisabu na malipo. Ama kuona kukali makusudio yake ni kuwa uhakika, kwa anayekana ufufuo, utajitokeza wakati wa kufa na baadae; atajua aliyoyakana na atayakana aliyoyajua.

Maana ni kuwa kesho ataambiwa mkanushaji: Ewe muovu! Uliikana siku hii ya leo na ukafuata hawa yako, ukaghafilika na uliyokusudiwa. Basi batili imekuondokea leo, umejua uhakika, lakini ni wakati ambao hakuna kimbilio la kujiepusha na kuungua.

وَقَالَ قَرِينُهُ هَٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ {23}

Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.

أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ {24}

Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi.

مَنَّاعٍ لِلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُرِيبٍ {25}

Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka.

الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ {26}

Ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.

قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَٰكِنْ كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ {27}

Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.

قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُمْ بِالْوَعِيدِ {28}

Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.

مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِلْعَبِيدِ {29}

Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.

يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِنْ مَزِيدٍ {30}

Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ {31}

Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.

هَٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ {32}

Haya ndiyo mnayoahidiwa. Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae.

مَنْ خَشِيَ الرَّحْمَٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُنِيبٍ {33}

Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.

ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ {34}

Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima.

لَهُمْ مَا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ {35}

Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.