Aya 23 – 35: Anayekataza Heri
Maana
Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.
Mwenzake ni yule aliyetajwa katika Aya ya 17- Malaika anayeandika matendo ya yule aliye naye. Maana ni kuwa. Mwandishi huyu atamwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
Hiki kitabu cha yale uliyonituma. Ndani yake mna mambo yote vile yalivyokuwa: “Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo. Na watasema:
وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ
وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا {49}
Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi, Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka, ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Katika Aya 21, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: “Na itakuja kila nafsi pamoja na mpelekaji na shahidi,” na katika Aya tuliyo nayo, anasimulia kuwa atamwambia mpelekaji na shahidi, mchukue kwenye Jahannam aliyenishirikisha, akaikufuru haki na akaifanyia inadi, akaipinga heri na akawazulilia watu nayo.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atarudia na kusisitiza: Basi mtupeni katika adhabu kali.
Ilivyo ni kuwa hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa sifa ya mwenye kuzuia heri yule mwenye kuruka mipaka, anayetia shaka. Na mahali pengine amempa sifa ya mwenye dhambi:
مَنَّاعٍ لِلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ {12}
Tukiunganisha Aya hizi na ile isemayo:
إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ {43}
طَعَامُ الْأَثِيمِ {44}
كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ {45}
كَغَلْيِ الْحَمِيمِ {46}
Tukiunganisha zote hizo inatubainikia kuwa kosa la kuzuia heri halina mfano na kosa lolote na kwamba adhabu yake haina kipimo.
Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.
Mwenzake huyu sio yule mwenzake wa kwanza. Yule wa kwanza alikuwa ni katika waandishi wema, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.”
Ama huyu rafiki wa pili ni katika maibilisi ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake: “Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.” Juz. 25 (43:36).
Dalili ya kuwa marafiki ni tofauti ni kauli ya rafiki wa pili: “Sikumpoteza.” Kwa sababu yule rafiki wa kwanza haiwezekani kupoteza, kwa hiyo hawezi kukana, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemchagua kuandika kutokana na uaminifu wake.
Zaidi ya hayo ni kuwa kubishana kesho kutakuwa baina ya wakosefu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Msigombane mbele yangu.” Pia kauli yake: “Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.” Juz. 25 (43:67).
Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.
Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu akiyaelekeza kwa mkosefu na rafiki yake shetani. Maana ni kuwa msianze kuambiana, wewe umenipoteza na mwingine naye aseme sikukupoteza. Kwani leo ni siku ya hisabu na malipo; wala mtu hatanufaika na maneno wala na mengine isipokuwa matendo mema tu; nami niliwawapa mwito wake na nikawahadharisha na siku ya leo kwa atakayehalifu, lakini mkakataa isipokuwa ukafiri.
Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.
Makusudio ya kauli hapa ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mpelekaji na shahidi: “Mtupeni katika Jahannam kila kafiri mwenye inadi.”
Kutupwa huku kutakuwa tu na ni uadilifu. Kutakuwa, kwa vile ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) wala hakuna mabadiliko katika amri yake. Ni uadilifu kwa sababu mkosefu anastahiki hivyo.
Unaweza kuuliza: maulama wengi wamesema kuwa inawezekana kwa Mwenyezi Mungu kuhalifu kiaga (ahadi ya kuadhibu), lakini haiwezekani kuhalifu ahadi; (ahadi ya mazuri) kama ilivyo katika Hadith, aliposema: “Mwenye kumwahidi yoyote kumlipa uzuri, ni lazima atekeleze, na mwenye kumwahidi ubaya, basi ana hiyari.”
Zaidi ya hayo ni kuwa kiakili ni vizuri kutekeleza ahadi, lakini si vibaya kuhalifu kiaga. Sasa kuna wajihi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Kwangu haibadilishwi kauli?’
Baadhi ya maulama wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu hasamehi hivi hivi tu, bali ni kwa sababu. Pia kusamehe si kubadilisha kauli. Nasi tunaongezea kwenye jawabu hili kuwa makusudio ya kiaga hapa ni kiaga cha adhabu ya mwenye kuzuia heri, na sio kila kiaga. Kwa sababu mruka mipaka huyu mwenye dhambi, tunavyodhani, ni kuwa hana kafara wala muombezi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?
Hiki ni kinaya cha ukali wa muwako wake na ukali wa adhabu yake, na kwamba haiwi na msongomano wa wenye hatia kwa idadi yoyote watakayokuwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameipa Jahannam sifa kadhaa za kutisha zinazosisimua ngozi za wale wanaomwogopa Mola wao. Ama wale walio na maradhi nyoyoni mwao, wanadharau sifa hizo na wale wanaoziamini.
Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.
Hii ni njia ya Qur’an, inaunganisha malipo ya muovu na mwema. Huko ni shida na machungu na hapa ni raha na nema na Pepo. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Haitakuwa mbali,’ ni kutilia mkazo neno kuletwa karibu.Makusudio ya kuletwa karibu Pepo kwa wenye takua ni kuwa ni yao na wao ni wa hiyo.
Haya ndiyo mnayoahidiwa.
Mlijua enyi wenye takua ahadi ya Mwenyezi Mungu naye ameitekeleza. Basi chukueni neema hii isiyokuwa na mpaka wa sifa wala kufikiwa na akili.
Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.
Sifa hizi nne ni alama za kujulisha mwenye takua: kuwa ni kutubia akijiweka mbali na maasi, kumhofia Mwenyezi Mungu na kudumu kumtii kwa kutumai thawabu zake, akiwa kwenye imani yake na ikhlasi yake kwenye njia moja; ni sawa awe mbele ya watu au akiwa mbali; kinyume na yule mwenye kujionyesha, mwenye ria.
Anakuwa mvivu akiwa peke yake na na anakuwa mchangamfu mbele ya watu. Huyo ndiye mwenye takua ambaye anamwelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo ulio salama.
Kwa maneno mengine ya Imam akimsifu mwenye takua:
“Amemtii anayemwonogoza na akaijiepusha na anayempoteza; akapata njia salama kwa busara ya anayemuonyesha na kutii amri ya anayemwongoza. Akaharakisha kwenye uongofu kabla ya kufungwa milango yake na kuisha nyenzo zake.”
Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima. Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.
Nyinyi wenye takua mtakuwa katika Pepo isiyokatika neema yake, hachoki mkazi wake, hazeeki anayedumu wala hakati tamaa mkazi wake. Mtapata zaidi ya manyoyatamani na kuyapendekeza.
Baada ya hayo, ni kuwa tofauti hii baina ya Pepo na Moto inafichua tofauti iliyopo baina ya wenye takua na wenye hatia na kwamba tofauti yao mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na tofauti ya Pepo na Moto.
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُمْ مِنْ قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُمْ بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِنْ مَحِيصٍ {36}
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ {37}
وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِنْ لُغُوبٍ{38}
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ{39}
وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ {40}
وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِنْ مَكَانٍ قَرِيبٍ {41}
يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ {42}
إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ {43}
يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ۚ ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ {44}
نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنْتَ عَلَيْهِمْ بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَنْ يَخَافُ وَعِيدِ{45}