Aya 36 – 45: Siku Atakaponadi Mwenye Kunadi
Maana
Na karne ngapi tuliziangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Nao walizunguka katika miji. Je, yako makimbilio?
Karne ni watu wa zama moja. Maana ni kuwa katika zama zilizopita kulikuwa na uma nyingi zilizokuwa na maendeleo, nguvu na idadi ya watu wengi kuliko wale waliokukadhibisha wewe Muhammad! Pia walikuwa na mawasiliano na miji mingine. Lakini yote hayo hayakuwafaa waliposhukiwa na adhabu, wala hawakupata pa kuikimbia amri ya Mwenyezi Mungu. Je, watu wako hawaogopi kuwasibu yaliyowasibu waliopita?
Maana haya yamekaririka kwenye Aya nyingi; ikiwemo: Juz. 21 (30:9).
Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.
Hayo ni hayo ya kukumbushwa maangamizi ya waliopita. Mwenye moyo ni moyo salama. Kutega sikio ni kusikiliza kwa makini. Shahidi ni yule aliyepo kimoyo na kiakili. Maana ni kuwa yale tuliyoyataja ya maangamizi ni mawaidha tosha kwa mwenye busara na akazingatia.
Na hakika tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita; na wala haukutugusa uchovu
Siku sita ni kinaya cha mikupuo au maendeleo ya kugeuka ulimwengu kutoka hali moja hadi nyingine. Tazama Juz. 8 (7:54).
Basi vumilia kwa hayo wasemayo, ya ubatilifu na usafihi. Kwa sababu mwisho ni wa wenye kuvumilia uvumilivu wa kiungwana.
Na msabihi Mola wako kabla ya kuchomoza jua. Hiyo ni ishara ya swala ya Alfajiri. Na kabla ya kuchwa, ni swala ya adhuhuri na alasiri.
Na katika usiku msabihi, ni swala ya magharibi na isha. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:130). Na baada ya kusujudu, ni ishara ya uradi baada ya swala na swala za sunna baada ya kumaliza za wajibu.
Na sikiliza siku ataponadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu. Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.). Siku atakayonadi, hapo kuna maneno ya kukadiriwa; yaani sikiliza masimulizi ya siku atakayonadi; na wala sio kusikiliza mnadi. Makusudio ya mahala karibu ni kuwa huo mwito watausikia wote; kama kwamba mnadi yuko karibu nao, ingawaje ukelele unatoka mbinguni.
Hapa ndio inatubainikia njia ya kuchanganya na kuafikiana baina ya Aya hii na ile isemayo:
أُولَٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِنْ مَكَانٍ بَعِيدٍ {44}
Maana ni kuwa, sikiza tunayokusimulia ewe Muhammad kuhusiana na ukulele wa ufufuo kwa ajili ya hisabu na malipo. Ukulele huu uko mbali, ukitokea mbinguni na uko karibu kwa kuwa unafika kwenye masikio yote, mpaka ya wafu, watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika:
هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَا أَسْلَفَتْ ۚ وَرُدُّوا إِلَى اللَّهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۖ وَضَلَّ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ {30}
Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
Uhai na mauti yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye ndio marejeo ya viumbe. Umetangulia mfano wake mara nyingi; kama vile katika Juz. 11(10:56).
Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
Ardhi itawapasukia wa kwanza na wa mwisho, watoke makaburini mwao upesi upesi; wakiwa ni wengi kuliko chunguchungu na machanga. Atakayekuwa na hali nzuri kuliko wengine ni yule atakayepata mahali pa kuweka unyayo wake na pa kuvutia pumzi zake; kama alivyosema Imam Ali (as).
Sisi tunajua sana wayasemayo, ya kumkadhibisha Mtume na kukana ufufuo. Wala wewe si jabari juu yao, kuwalazimisha kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Wewe ni muonyaji tu.
Basi mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa kiaga na yule asiyeogopa pia ili utoe hoja. Mwenyezi Mungu amemuhusisha kumtaja anayeogopa kwa kuashiria kuwa yeye ananufaika na ukumbusho zaidi kuliko asiyeogopa:
فَذَكِّرْ إِنْ نَفَعَتِ الذِّكْرَىٰ {9}
سَيَذَّكَّرُ مَنْ يَخْشَىٰ {10}
وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى {11}
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Atajiepusha nako muovu,’ ni dalili mkataa kuwa amri ya kukumbusha ni ya ujumla, iwe kutafaa au hakutafaa.